27/11/2025
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taasisi za kutetea haki za wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watoto Zanzibar, zinaungana kwa pamoja kuadhimisha Siku 16 za Kupinga udhalilishaji.
Maadhimisho haya yameanza rasmi tarehe 25 Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza udhalilishaji dhidi ya Wanawake, na yatahitimishwa tarehe 10 Disemba,
Siku ya Haki za Binadamu Duniani. Taasisi hizo ni pamoja na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF), Pamoja Youth Initiatives (PYI) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania , Zanzibar (TAMWA -ZNZ).
Mfululizo wa shughuli za maadhimisho unajumuisha kutayarisha makala na jumbe za kuelimisha jamii, kushiriki maadhimisho ya Siku ya watu wenye ulemavu tarehe 3 Disemba, maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji itakayofanyika tarehe 6 Disemba pamoja na kutoa taarifa ya pamoja ya hitimisho tarehe 10 Disemba ambayo ni Siku ya Haki za Binadamu. Shughuli ya tarehe 6 Disemba 2025 itakua ni maalum kwa ajili ya kujadili masuala ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa mtazamo wa usawa wa kijinsia.
Kikao hiki kinalenga kuonesha mafanikio, changamoto na mwenendo wa haki za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mazingira ya kisiasa na ya kidijitali, sambamba na kutoa mapendekezo yanayolenga kuimarisha ushiriki jumuishi kwa makundi haya.
Kwa upande mwengine, taasisi hizi zinaeleza wasiwasi wake kutokana na kuwepo vitendo vya udhalilishaji wa mitandaoni, ikiwemo kusambaza picha na video za faragha bila ridhaa, udukuzi wa taarifa, lugha ya chuki na vitisho vinavyolenga kuwanyamazisha wanawake katika siasa, uongozi, na majukwaa ya umma.
Vitendo hivi vimeripotiwa kusababisha madhara makubwa ya kijamii na kisaikolojia, huku baadhi ya waathirika wakikumbana na unyanyapaa, kuacha masomo au kukosa fursa za kiuchumi kutokana na unyanyasaji huu wa mtandaoni.
Tafiti mbalimbali na ripoti kutoka vyombo vya habari zinaonesha kuwa waathirika wengi, hasa wanawake na wasichana, hurekodiwa au husambaziwa taarifa za faragha bila ridhaa, jambo linalopelekea aibu ya hadharani na kuongezeka kwa vitendo vya kuwatapeli mtandaoni (cyberblackmail).
Taasisi hizi zinatoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha kesi zinachunguzwa kwa ufanisi, na kuanzisha mifumo rafiki ya utoaji taarifa inayowalinda waathirika kwa usiri, usalama na heshima. Sambamba na hilo, jamii inahimizwa kukuza utamaduni wa kuheshimiana na matumizi salama ya teknolojia ili kujenga mazingira jumuishi yanayowawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika majukwaa yote.
Kaulimbiu ya Kimataifa mwaka huu ni “TUUNGANE Kukomesha Ukatili wa Kidijitali Dhidi ya Wanawake na Wasichana”, huku ujumbe wa kitaifa ukiwa ni “Mitandao Salama ni Haki: Maliza Ukatili wa Kimtandao kwa Wanawake na Watoto.”
Kwa zaidi ya miongo mitatu, Kampeni ya Siku 16 za Kupinga udhalilishaji imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa serikali, asasi za kiraia na wadau mbalimbali kuhamasisha mabadiliko ya sera, elimu ya jamii, tafiti na hatua za pamoja ili kukomesha aina zote za udhalilishaji ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili, kiuchumi, kisaikolojia, kijinsia na sasa ukatili wa kidijitali unaozidi kuongezeka.
Imetolewa na:
Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF) Pamoja Youth Initiatives (PYI) Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA) Zanzibar
Comments
Post a Comment