WAZAZI na walezi wenye watoto wenye
ulemavu wametakiwa kuwaandikisha watoto hao skuli kwa mwaka wa masomo unaotarajiwa kuanza 2026, ili
kuhakikisha upatikanaji wa haki ya msingi ya elimu kwa watoto hao.
Wito huo umetolewa na Afisa mdhamini
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Pemba Mohamed Nassor Salim wakati akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, alisema zoezi la uandikishaji wanafunzi wapya kwa mwaka wa masomo 2026
linaendelea kwa watoto wote waliofikia umri wakiwemo wenye ulemavu.
Alisema wakati umefika kwa wazazi,
walezi jamii na serikali za shehia kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata
haki yao ya msingi ya elimu, kwa kuhakikisha wanandikishwa skuli bila kujali
mahala wanapoishi au aina ya ulemavu walionao.
Aliongeza serikali kupitia wizara ya
elimu imeandaa mazingira rafiki kwa watoto wenye ulemavu ambao wanaishi katika
mazingira magumu, kwa kuwajengea skuli maalumu inayotoa elimu mjumuisho ili
kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya elimu kama ilivyo kwa watoto
wengine.
" Ili kuhakikisha kila mtoto wa
Zanzibar anapata haki yake ya msingi ya elimu kama zinavyoeleza sheria na sera,
serikali inaendelea kuweka mazingira
rafiki kwa watoto wote wakiwemo wenye ulemavu, na tumejenga skuli ya elimu
mjumuisho na tunaendelea kusajili wanafunzi wenye sifa, hivyo ni muhimu jamii
kuunga mkono hili kwa kuhakikisha watoto
hao wanaandikishwa, " alieleza.
Alisema kwa mwaka wa masomo 2026
ambao uandikishaji wake unaendelea, skuli ya elimu mjumuisho iliopo pujini kwa
mara ya kwanza itakua na darasa la elimu ya maandalizi, huku lengo likiwa ni
kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa ya elimu.
Aidha alisema kua, ili kuhakikisha
jamii inakua na muamko zaidi kuhusu ulazima wa upatikanaji elimu kwa watoto
wenye ulemavu, wizara imeanzisha kampeni ya kushajihisha jamii kulitimiza hilo
kwa kushirikiana na viongozi wa shehia.
Alisema ni vyema wazazi kitumia fursa
hiyo ya uwepo wa skuli ya elimu mjumuisho ya Pujini Chake chake Pemba kwa
kuwaandikisha watoto wenye ulemavu, kwani kuna miundombinu rafiki kwa ajili ya
kufundishia na kujifunzia.
Nae Mwalimu wa wanafunzi wenye
ulemavu wa uoni na uoni hafifu kutoka skuli ya Elimu Mjumuisho Pujini Hanifa Abeid Ali alisema, kuelekea mwaka wa
masomo 2026 wameshasajili wanafunzi wapya 30 ambao wanaulemavu wa aina mbali
mbali.
Akitoa wito kwa wazazi wenye watoto
wenye ulemavu ambao hawajawaandikisha na umri umesharuhusu mwalimu huyo alisema, ni vyema kuwaandikisha watoto wao
skuli ili kupata haki yao ya msingi ya elimu, kwani ulemavu si sababu ya mtoto
kutosoma.
Nae mwalimu Anipae Amiri Manallah
kutoka skuli hio aliiomba wizara ya
elimu kuendelea kuboresha miundombinu ya skuli hiyo kwa kuongeza vifaa vya
kujifunzia na kufundishia pamoja na waalimu ili lengo la utoaji elimu bora
liweze kufikiwa.
Skuli ya elimu Mjumuisho Pujini
imajumla ya wanafunzi 76 wenye ulemavu wa aina tano, ukiwemo ulemavu wa uoni
/uoni hafifu, Uziwi, Viungo, Albino na Matamshi, na hadi sasa inawanafunzi wa
darasa la kwanza hadi la tano.
Aidha kwa mujibu wa sera ya elimu ya
Zanzibar inasema wizara ya Elimu itahakikisha haki na fursa za elimu inazotoa
kwa wazanzibari wotewote, zinatolewa kwa
misingi ile ile kwa watu wenye ulemavu.
MWISHO

Comments
Post a Comment