NA FATMA HAMAD, PEMBA@@@@
UTELEKEZAJI ni ile hali ya wazazi
kukwepa majukumu yao ya kutoa matunzo kwa familia zao.
Wengi wa wananchi wanadai kwamba, sababu kubwa
inayopelekea utelekezaji ni baadhi ya akinababa wanapoamua kuoa mke zaidi ya
mmoja, maranyi huwa hawatimizi wajibu wao.
Ingawa wapo wengine, hudai kukumbwa na sababu, ya
kutafuta maisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mfano wa wavuvi au
wafanyabiashara.
Hayo yakifanyika, mafundisho ya dini yanafundisha
kuwa, mzazi wa kiume ndio mwenye jukumu kubwa la kutoa matunzo kwa familia yake.
Lakini ulimwengu wetu wa leo, kumeibuka wimbi kubwa
la baadhi ya wanaume kukwepa majukumu
yao na kuwabebesha mzigo wa malezi wanawake peke yao.
Hali hiyo ya wanaume kutokushughulikia familia zao, inasababisha
watoto kuishi kwa simanzi na huzuni, kana kwamba wamefiwa na wazazi wao na
kukosa familia ya kuwatunza.
Kiongozi wa Kanisa
Katoliki lililopo Mkungu Malofa Chakechake, Robert Miguwa Ndalami, anasema
dini imeelekeza kwamba, wanaume ndio wanaotakiwa kutoa huduma stahiki kwa
familia zao.
“Baba ndio kichwa cha familia, hivyo yeye ndie
anaetakiwa kuhudumia na sio kumuachia mama aleye peke yake,’’nanukuu.
Sheikh Said
Ahmed Mohamed anasema, kisheria mwanamme ndie mwenye jukumu la kutoa matunzo
kwa familia yake, na sio vyenginevyo.
Anasema ijapokua
wanandoa wameamua kuachana au kutengana, bali ni jukumu la mwanamme kuhakikisha
anawahudumia watoto, na sio kuwatia
adabu kwa sababu ya ugomvi wao.
‘’Hatakama mtaamua
kuachana ama kutengana kila mmoja kuishi sehemu yake, bado baba jukumu lake ni kuwahudumia
watoto, msiwaingize kwenye ugomvi wenu, wao hawahusiki,’’anasema.
"Inatosha
mtu katika dhambi kuwatupa wale ambao anawajibika yeye kuwapatia matumizi"
WATOTO
WANATHIRIKA VIPI WANAPOTELEKEZWA
Mwanafunzi wa darasa la tatu skuli ya Msingi
Micheweni anasema, anahamu ya kusoma na kufika hadi elimu ya juu, ingawa anashindwa,
kwani hana mtu wa kumuhudumia kupata vifaaa vya masomo.
Anasema kitendo cha kukosa huduma kutoka kwa wazazi
wake wawili, kimemuathiri, kwani anashindwa kupata huduma stahiki, ambazo
anaamini zingekuwa sababu ya kufika mbali.
Kumbe babayoa amewatelekeza, ameoa mke mwingine,
hawaulizi kwa chakula wala kwa matibabu, hivyo anashindwa kusoma kwa bidi.
Mtoto mwengine ambae ameshafikia umri wa kuanza
masomo ya mandalizi, anasema hajapelekwa kwani, mama yake hana uwezo wa
kumtafutia vifaa kwa ajili ya kusomea.
‘’Nimekaazangu
tu nyumbani sijapelekwa masomoni, nasubiri mama akipata uwezo anipeleke na mimi
ili nisome,’’anasema.
Bilali Mohamed
Rashid (16) anaesoma darasa la kumi, anasema ndoto zake ni kua waziri wa Fedha, hapo baadae.
Ingawa, kitendo
cha kukosa huduma kutoka kwa baba yake kinamuathiri, kwani anashindwa kupata
huduma anazotakiwa.
‘’Tunakwenda skuli
hatuna viatu mvua kama hizi, hatuli chochote, na tukirudi tunakuta hamna kitu,
kwa kweli hilo linaniathiri na kuvuruga ndoto zangu,’’anasema.
WAZAZI NA JAMII WANALIPI
Bikombo Makame
Shaame wa Chamboni Michewni ambae ana watoto watano, anasema huduma zote anajitegemea
mwenyewe, licha kama bado yupo kwenye ndoa.
‘’Huu ni mwezi
wa sita, hajawaletea watoto chochote, amenifanya nimekua kama ombomba, nikimpigia
simu hanipi jawabu nzuri maana hivi karibuni aliongeza mke,’’anaeleza.
Anakiri kuwa, watoto
wanathirika kwani, wanaondoka asubuhi wanakwenda masomoni hawali chochote na
wakirudi ndio vivyo hivyo.
Bikombo Khamis
mkaazi wa Mjini wingwi anasema, mume wake huondoka kwenda uvuvini Dar -es Saalam
na kurudi kipindi cha mwezi wa ramadhani pekee.
‘’Ananiachia
watoto wanane, haniulizi kwa chochote, nivunje kokoto ndio nipate fedha kwa
ajili ya huduma za ndani, kinyume chake ni kulala na njaa,’’anasema.
Mwengine ni Rehema Salum
Issa mkaazi wa Madenjani wilaya ya Wete
Pemba, anasema mume wake, amemuacha na watoto saba, na kumuachia mzigo wa
malezi.
Salma Ali kutoka Machomane,
anasema kwa hakika, mwanamke anapotelekezwa na watoto wanahangaika, na hususani
akiwa hana shuguli za kujiingizia kipato.
‘’Mimi bado niko kwenye
ndoa, tunashirikiana, lakini kuna siku tunakosa kuwatimizia watoto wetu
mahitaji ya lazima, kama sare za skuli, inatubidi tuyazungumze,’’anaeleza.
Mohamed Rashid ni mstaafu wa JWTZ, ni miongoni
mwa mzazi anayedaiwa na mwenzake wake kuitelekeza familia yake, ingawa anasema
hali ngumu ya maisha ndio sababu.
‘’Ni kweli mimi mstaafu, ingawa
ninachokipata, hakitoshelezi kukigawa nyumba mbili, nilishamtaka watoto
anikabidhi, ingawa amegoma,’’anasema.
Said Kombo Kassim ni mkaazi wa Chakechake
anasema kuoa wake zaidi ya mmoja, haisababishi mtu atelekeze familia yake, bali
ni tabia mbaya walio nayo baadhi ya wanaume.
‘’Mimi nina wake wawili miaka 10 sasa, ila
sijawahi hata siku moja kunyima familia
zangu huduma, na nikikosa tunakaa chini kuyazungumza,’’anasema.
WANAHARAKATI
Amina Ahmed Mohamed ni
mwanaharakati kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA
Zanzibar Ofisi ya Pemba, anasema ipo haja kwa viongozi wa dini kushirikiana na
wanaharakati, kutoa elimu kwa wanaume.
Mratibu wa
wanawake na watoto shehia ya Chamboni Micheweni Bizume Omar Faki, anasema
watoto wengi wanaotelekezwa na wazazi wao, ndoto zao za kusoma huishia njiani.
‘’Wengi hujingiza
kwenye uvuvi, uparaji samaki na kuuza biashara, ili kujipatia mahitaji yao na
nyumbani kwao,’’anaeleza.
Dokta Rahila Salum Omar ambae ni msimamizi wa vituo vya kutoa huduma kwa
watu wenye ‘VVU’ anasema, watoto
wanapotelekezwa, huathirika kiakili na hukosa uwezo wa kufuatilia, haki zao ikiwemo
elimu.
SERIKALI
Mkuu wa wilaya
ya Micheweni Khatib Juma Mjaja, anasema katika wilaya yake, bado suala la utelekezwaji
wanawake na watoto, ninaendelea kuota mzizi siku hadi siku.
Anasema, jambo hilo
linasababisha kundi la watoto, kushindwa kutimiza malengo yao waliojiwekea,
ikiwemo haki yao ya elimu.
‘’Kwa hakika, wilaya
yangu bado hali si nzuri, watoto wanateseka na suala hilo la utelekezwaji, kwa kule
baadhi ya wanaume kuacha majukumu yao,’’anasema.
Juhudi
wanazozichukua ni kutoa elimu kwa jamii ili
wawe na subra katika ndoa zao, sambamba na kuwataka wanaume kuoa wake ambao watakua
na uwezo wa kuwahudumia.
Afisa Ustawi wa
jamii wilaya ya Michewebi Bizume Haji Zume, anasema suala la utelekezaji wa
watoto bado ni kilio katika wilaya yake.
‘’Baba wengi
huondoka na kuwaaga wake zao wanakwenda kutafuta maisha, lakini mwisho wa siku hawarudi
tena, na kuwaachia mzigo wa huduma,’’anasema.
WANASHERIA
Aliekua Hakimu
wa Mhkama maalumu ya kupambana na udhalilishaji Wete, Mumin Ali Juma anasema utelekezwaji
unachangia kwa watoto kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo ubakaji na
ulawiti.
‘’Unamuacha
mwanamke na watoto watano ama saba, humpi huduma yoyote, umetegemea nini afanye,’’aliuliza.
Anasema maranyingi
kesi zinazofikishwa Mahkamani za waliofanyiwa udhalilishaji ni watoto ambao
wamekosa malezi ya pamoja kati ya baba na mama.
Mwendesha Mashtaka
wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Juma Mussa Omar anasema,
sheria zote zinapinga utelekezaji watoto kutokana na msingi kwamba, bado
wanategemea malezi na huduma.
Anasema matunzo ya watoto au matendo mabaya dhidi ya watoto yanaongozwa
na sheria za kimataifa, za kikanda na sheria za nchi.
Akatoa mfano
kama Sheria ya mtoto Zanzibar, namba 6 ya mwaka 2011, Kifungu cha 9 (1)
kinaelekeza haki ya mtoto kuishi na wazazi wake, walezi au familia ili akue kwa
upendo na mazingira salama.
Kifungu cha 71, kinaelekeza kumtoza faini
mzazi atakaeshindwa kutoa matunzo kwa
mtoto, ikiwa amri hiyo ya matunzo
imetolewa chini ya kifungu cha 69 cha sheria hiyo.
Ripoti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee, na Watoto ya mwaka 2024/2025 inaarifu kuwa, kulipokelewa malalamiko 691 Unguja 313 na Pemba 378,
yanayohusu ukiukwaji wa haki za watoto, mivutano ya malezi.
Ambapo kwa upande wa Pemba kuanzia
mwaka 2022 hadi 2024 malalamiko 1013 ya utelekezwaji wa watoto yalirpotiwa
katika Idara ya Ustawi wa Jamii.
Wapo watoto waliotelekezwa ni 2183,
wanaume ni 1096 na wanawake ni 1087.
Kwengeneko, ripoti ya uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na shirika
la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto ulimwenguni (UNICEF), takwimu
zinaonyesha kwamba idadi kubwa ya watoto wanaishi katika mazingira magumu.
Inasisitiza
kwamba takriban watoto milioni 160 ulimwenguni kote, wanakabiliwa na hali ya
kutengwa au kutelekezwa.
Ambapo kwa idadi
hiyo, sawa na wastani wa watoto 13, 333 kwa mwezi, sawa na watoto 111 kwa siku
hutelekezwa duniani kote, kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya wazazi
kuacha familia moja na kutafuta nyengine.
MIKATABA
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 12 (1)
kinaeleza, watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi
wowote, kulindwa na kupata haki sawa.
Mkataba wa Kimataifa wa haki za Watoto duniani wa mwaka
1989, ulioanza kutumika mwaka mmoja baadae, kifugu cha 9, kinasisitiza nchi
wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuhakikisha watoto hawatelekezwi.
UNICEF
ikabainisha kuwa, wasitenganishwe na
wazazi wao, isipokuwa kwa amri ya mahakama au taasisi, inayohusikia
maslahi bora ya mtoto.
Mkataba wa haki na Ustawi wa Watoto wa Afrika wa mwaka
1999, kifungu cha 19, kikalazimisha kuwa, kila mtoto anayohaki ya kufurahia na
kunufaika na malezi bora kama msingi mkuu wa kupata haki
Mkataba
huu unasisitiza nchi wanachama kuhakikisha zinaondoa mila na tamaduni potofu zinazoathiri
ustawi, utu, makuzi na maendeleo ya mtoto Afrika.
MWISHO


Comments
Post a Comment