NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
SHEHA wa Chumbageni wilaya ya Mkoani,
Mgeni Othman Shaame, jioni ya leo anatarajiwa kuwaongoza wanachi wa kijiji cha
Kidutani, kuzipitisha sheria ndogondogo, zitakazowaongoza wananchi hao, ili
kujenga tabia njema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa
kamati ya elimu na maadali ya kijiji hicho Machano Ali Makame, alisema jioni ya
leo, kijijini hapo watakuwa na ugeni wa shehia yao.
Alisema kuwa, sheha huyo pamoja na ujumbe wake
akiwemo askari wa shehia, watakutana na wananchi hao, na kuzijadili kwa mara ya
mwisho kanuni, hizo kabla ya kuzipitisha rasmi.
Alieleza kuwa, kijiji hicho kimeamua kuanzisha kanuni
hizo, ili kuwasawaidia vijana kuwaelekeza kwenye maadili mema, ili wawe raia
bora wa taifa hili.
‘’Ni kweli jioni ya leo, Sheha wa Chumbageni
ataungana na wananchi wa kijiji cha Kiduatani, ili kuzipitisha kanuni, ambazo zilianzishwa
na wananchi wenyewe,’’alisema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mwalimu Saleh Abdalla
Mohamed, alisema moja ya kanuni ambazo zitarajiwa kupitishwa, ni kusitisha muda
wa kuranda ovyo mitaani hapo nyakati za usiku.
Alieleza kuwa nyingine ni kupiga marufuku matumizi
ya sigara kwa watoto, pombe, upigaji ngoma, wizi, uvaaji wa nguo za mbano,
ukataji nywele usio wa maadili.
‘’Kanuni nyingine ambayo jioni ya leo sheha atazikagua
na kuzipitisha pamoja na wananchi wenyewe, ni uvaaji za suruali juu ya magoti
kwa wanaume, vigenge hatarishi na kuwarejesha masomoni walioacha,’’alifafanua.
Kwa upande wake Katib wa sheha wa shehia hiyo, Abdalla Salim Juma, alisema maandalizi
yote kwa ajili ya mkutano huo wa jioni ya leo, yameshakamilika.
Alisema, tayari wajumbe wa sheha, askari wa shehia
na sheha mwenyewe, wameshaarifiwa kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa leo.
‘’Ni kweli wananchi wenzetu wa kijiji cha Kidutani,
waliamua kuanzisha kanuni, ambazo leo uongozi wa shehia ya Chumbageni,
unakwenda kukutana na wananchi na kuzipitisha kwa pamoja,’’alifafanua.
Baadhi ya wananchi wa Kidutani, akiwemo Juma Abassi
Ali, alisema wanatamani haraka mkutano huo, ufanyike na kanuni hizo, zianze
kazi.
Nae Time Pandu Makame, alisema kijiji hicho ingawa
kina wananchi kidogo, lakini kimekuwa kikitumbukia kwenye wizi wa mifugo, utoro
wa wanafunzi pamoja na tabia nyingine chafu.
Hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan
Faki, aliwataka wananchi, kuendelea kuzifufua polisi jamii, ambazo huwa ni
masaada mkubwa wa kuzuia uhalifu.
Mwisho
Comments
Post a Comment