NA MOZA SHAABAN, PEMBA
WASHIRIKI wa mafunzo ya uratibu wa Uchaguzi kisiwani Pemba wametakiwa kuzipitia na kuzifuata vyema sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi ili kutekeleza ipasavyo majukumu yao.
Wito huo umetolewa leo Julai 21, 2025 na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mbarouk Salim Mbarouk ambae pia ni mgeni rasmi katika mafunzo hayo yaliofanyika Wawi Chake chake Pemba.
Alisema ni vyema kwa waratibu hao kutumia muda wao kuzisoma na kuzifuata katiba, sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao katika kipindi chote cha usimamizi wa uchaguzi Mkuu.
Alieleza kua uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbali mbali za kisheria, zinazopaswa kufuatwa ili kuimarisha utendaji wa kazi hizo pamoja na kuimarisha amani nchi.
"uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbali mbali za kisheria zinazopaswa kufuatwa ili kuimarisha utendaji wa kazi na kujua na kuzifuata sheria hizo kutasaidia kuimarisha amani nchi, " alieleza.
Alisema kua jukumu la kusimamia ucjaguzi ni kubwa, hivyo aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuyafuata mafunzo hayo pamoja na sheria na miongozo ili kujipatia ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu uchaguzi.
Aidha aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na migogoro na kua vyanzo vya malalamiko, hivyo ni vyema kufuata kanuni na sheria zilizowekwa, huku akiwasisitiza kutoa taarifa za uchaguzi kwa tume ya uchaguzi na si sehemu nyengine isio husika.
Hata hivyo aliwataka washiriki hao kusimamia vyema jukumu la kusimamia shughuli zote za uchagazi kwa ngazi ya Uraisi na ubunge wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, ili kuhakikisha linamalizika kwa weledi.
Mapema akiongoza kiapo cha uadilifu kwa washiriki hao Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Chake chake Nassor Suleiman Nassor aliwataka washiriki hao kutunza siri, kua waadilifu, kujiamini na kujiepusha na migogoro ili kutunza amani iliopo.
Akieleza kaulimbiu ya Uchaguzi mkuu wa 2025 Kaimu Mkurugenzi Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi 'INEC ' Adam Mkina alisema, kaulimbiu ya mwaka huu inaeleza kua 'Kura yako haki yako jitokeze kupiga kura " alisema kua kaulimbiu hiyo inalenga kuwasisitiza wanachi wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi ili kutimiza haki zao za msingi.
Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema mafunzo hayo yatawawezesha kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yalioratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi INEC, yamehusisha jumla ya washiriki 59 wakiwemo waratibu wa Uchaguzi, waratibu wa uchaguzi wa Chuo cha mafunzo, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo kwa mikoa ya kusini na Kaskazini Pemba na yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu.
MWISHO
Comments
Post a Comment