NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKUU wa wilaya ya Wete Pemba, Abdalla Rashid Ali, amesema, uendelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluh Hassan, ni chachu ya upatikanaji haki kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Mkuu huyo wa wilaya ya aliyasema leo Mei 31, 2025 ukumbi wa Jamhuri Wete, alipokuwa akifungua mafunzo ya wataalamu wa masuala ya sheria, kabla ya kwenda kutoa msaada wa kisheria wananchi wa wilaya ya Micheweni na Wete kwa siku tisa.
Alisema, wazo la Mama Samia, ni jema ambalo pamoja na kuwasaidia wananchi kutambua haki zao za msingi, ni msingi wa kulinda na kuendelea amani iliyopo.
Alieleza kuwa, iwapo wananchi watafundishwa namna ya kujua haki zao, itasaidia mno kuheshimiana katika mambo mbali mbali, samba mba na kukuza na kuendeleza msingi wa amani na utulivu.
‘’Kwanza niwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yule wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa, kuanzisha jambo hili kwani, linafaida kadhaa kwa jamii ikiwemo kujua haki zao,’’alieleza.
Akizungumzia mafunzo hayo ya watalamu, Mkuu huyo wa wilaya ya Wete, aliwataka kuwa makini na wasikivu, ili baadae waweze kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa uweledi.
‘’Mbinu kubwa ya kufahamu mafunzo haya, kwanza ni kuwawatulivu na kuongeza umakini, ili sasa tunapokwenda kuwahudumia wananchi wetu, wapate ushauri na msaada wa kisheria wenye tija,’’alifafanua.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kwa kuendelea kusimamia vyema kampeni hiyo, na hadi kufikia mafunzo hayo.
Alifahamisha kuwa, umakini wa watendaji wa Idara hiyo umesaidia kuona kampeni hiyo, sasa inaendelea kuwafikia wananchi wote wa mkoa wa kaskazini Pemba, jambo ambalo linafaa kuungwa mkono.
Mapema Mkuu wa Divisheni ya Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba Bakar Omar Ali, alisema uzinduzi wa kampeni hiyo, ulishafanyika tokea Oktoba 17, mwaka 2024, kimkoa na sasa ni muendelezo.
Alieleza kuwa, tayari kwa mkoa wa kusini Pemba, uzinduzi ulioambatana na kambi umeshafanyika na kuwafikia wananchi wengi kupata haki zao.
Mkurugenzi Baraza la mji Wete Shuwena Hamad Ali, ameipongeza Idara ya Katiba na Msaasda wa Kisheria kwa kuendeleza kampeni hiyo.
Katika mafunzo ya siku moja, kwa ajili ujazaji wa taarifa, kwenye kambi ya siku tisa, washiriki ni pamoja na makadhi, wasaidizi wa sheria, watendaji wa ofisi ya mwansheria mkuu, waandishi wa habari, mawakili wa serikali na kujitegemea.
Mwisho
Comments
Post a Comment