Na Haroun Simai WMJJWW
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WMJJWW) imepokea msaada wa vifaa na chakula kutoka Chuo cha Polisi Zanzibar (ZPC) kwaajili ya matumizi ya Watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha kulea Watoto Mazizini Wilaya ya Magharibi ‘B’ unguja.
Msaada huo umepokelewa jana Januari 01, 2025 na mama mlezi wa kituo hicho ndugu Wahida Abdallah Hassan kwaniaba ya Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambapo msaada huo umetolewa na wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho.
Ndug. Wahida alieleza msaada uliyopokelewa ikiwemo Mchele, Sabuni, Maji safi na salama, biskuti, juisi za chupa, taulo za kile, zana za kusafishia fagio na dawa, n.k.
Aidha bi Wahida ameushukuru uongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kuridhia wanafunzi wa chuo hicho kufika katika kituo cha kulea Watoto yatima na kuwasilisha msaada wa vyakula na vifaa kwani ni wazi kwamba wameonesha upendo na huruma ya kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu.
Nae Mkaruguzi Msaidizi wa ZPC, ambae ni Mkufunzi wa Chuo hicho ndug Omar Othman ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kupokea zawadi walizowasilisha kwa Watoto yatima wa kituo hicho.
Pia ameishukuru Kamandi ya Chuo hicho kwa kuwaruhusu wanafunzi hao na kuwapa kibali ili kuungana na watoto yatima siku ya mwaka mpya 2025.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa wanafunzi wa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kuendelea kuungana na jamii katika kutoa msaada kwani huo ni ubinaadamu utakaopelekea furaha kwa jamii na kuongeza nguvu za mashirikiano na Jeshi la Polisi.
Akizungumza moja kati ya Wanafunzi hao Koplo Peter Mwakabenga amesema lengo kuu la Jeshi la Polisi ni kukakikisha kuwa wanatoa mchango mkubwa katika jamii pamoja na kurudisha wema na fadhila kwa jamii ambayo ndio wanayoitumikia .
Pia na kuitaka jamii kuondoa muhali na kushirikiana na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa hali na mali katika kuripoti matukio ya vitendo viovu ikiwemo uhalifu.
Comments
Post a Comment