KHAULAT SULEIMAN, PEMBA@@@@
MKAGUZI wa Polisi Inspekta Khalfan Ali Ussi, amewataka wazee wa watoto wenye ulemavu wa ualbino kisiwani Pemba, kutojiweka pembeni katika kusimamia malezi ya watoto wao.
Alisema kuwa jeshi la polisi, limeanda mpango maalumu wa kuwasajili watu wenye ulemavu ualbino Tanzania nzima, ili kuweza kufuatilia na kubaini changamoto zinazowakabili.
Aliyasema hayo katika skuli ya Pandani mkoa wa kaskazini Pemba, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea na kusikiliza changamoto mbali mbali, zinazo wakabili makundi maalum katika shehia ya Pandani.
Aidha alisema kuwa jeshi la polisi limeweka mikakati madhubuti wa kuhakikisha usalama kwani jeshi hilo linahakikisha linalinda raia na mali zao.
"Wananchi ondoweni hofu na kuishi kwa amani, kwani nyinyi ni raia wema wenye haki sawa na wingine,’’alisema Mkaguzi huyo.
Hata hivyo, amewakumbusha wazazi na walezio hao, kuhakikisha watoto hao wanapatia haki zao zote za msingi ikiwemo elimu, afya na kuchangamana na watoto wenzao wakati wote.
‘’Watoto hawa wana haki sawa kama ilivyo kwa watoto wingine, hivyo wazazi mnapoombwa ruhusa ya kucheza msiwanyime haki yao hiyo,’’alisisitiza.
Naye mzazi Sultan Ahmad Issa alisema kuwa, watu wenye ualbino wanahitaji mazingira mazuri, ili kujikinga na changamoto ya kupata magonjwa ya ngozi ikiwemo saratani
"Serikali kuweza kuwasaidia kwa kuweka mikakati ambayo, itawezesha kujikwamua kimaisha kwa kuweka mfumo maalum, kwajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ualbino,’’alisisitiza.
Kwa upande wake Fatma Ali Suleiman ambaye ni mlemavu wa ualbino, alisema wanawakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kusomewa, kofia maalumu kwajili ya kujikinga na jua.
Alitaja vifaa vyingine kuwa ni, viatu rafiki kwajili ya kukanyagia pamoja na mafuta ambayo yanawasaidia katika kuboresha ngozi zao.
Naye mwakilishi wa shehia hiyo Haji Abdalla Ali amesema kuwa licha ya ukaribu na ufuatiliaji wa jeshi la polisi, lakini bado wazazi wanajukumu la kusimamia maadili na malezi ya watoto wao.
"Kufanya hivyo kutawasaidia jeshi la polisi kuweza kufanya kazi zao kuwa urahisi, hivyo kuendelea kuwa pamoja na wanajamii wa makundi mbali mbali katika shehia hiyo.
Nao wazazi wa watoto hao walilishukuru jeshi la polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kwa kuwapatia elimu ya ushirikishwaji kwa watu wenye ulemavu wa ualbino.
"Sasa tutaishi kwa amani huku tukiendelea kuchukuwa tahadhari, juu ya imani potofu iliyojengeka juu ya watu wenye ulemavu wa ualbino,’’walisema wazazai hao.
MWISHO.
|
Comments
Post a Comment