NA MWANDISHI WETU, UNGUJA@@@@
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka wananchi kujiunga katika michezo mbali mbali ili kuimarisha afya zao pamoja na kuepukana na maradhi yasiyoambukiza.
Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uekaji jiwe la msingi katika Mradi wa ujenzi wa viwanja vya Michezo midogo midogo iitwayo "Michezo kwa Maendeleo (Sports for Development) katika viwanja vya Mwera Regeza Mwendo Wilaya ya Magharib A. Unguja.
Waziri Pembe alifahamisha kwamba hata viongozi wa dini na wataalumu wa Sekta ya Afya wamekua mstari wa mbele katika kuihamasiha jamii kufanya mazoezi au kujiingiza katika michezo mbali mbali ambapo hatua hiyo itasaidia kuimarisha afya na kuijiepusha na maradhi yasiyoambukiza ikiwemo kansa, kisukari na shindikizo la damu.
Aidha alisema pia michezo ni ajira na sehemu ya kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hasa kwa vijana wa jinsia zote, kwani michezo inawasaidia kujiepusha na vitendo viovu ambapo vinajitokeza katika jamii.
"Nitowe wito kwa wazazi na walezi kuwaruhusu mabinti zao kushiriki katika michezo kwani michezo sio uhuni, uhuni ni mtu mwenyewe, lakini tukizingatia nidhamu maadili mila na silka na utamaduni wa Kizanzibari" amesema Waziri Pembe.
Sambamba na hayo amemuomba Mkuu wa wilaya kuwahimiza wananchi kusafisha maboma na kukata misitu ili kuhakikisha usalama wa mazingira yaliyowazunguka yanakua salama.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Magharib "A" Sadifa Juma Khamis amesema azma yake kuwaona wananchi wa Magharib A wanaishi katika hali ya usalama na amani. Pia amesema yupo tayari kuwashughulikia wahalifu wanao haribu amani nchini ikizingatiwa yeye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama katika Wilaya hiyo.
Awali muakilishi WA SHIRIKA la kimataifa ya Ujerumani GIZ Lucy Moto amesema mradi wa ujenzi wa viwanja vya michezo midogo midogo umelenga kujenga viwanja sita Zanzibar ambapo viwanja vitatu vitajengwa Unguja na vitatu Pemba vyenye mnasaba na mpira wa kikapu, mpira wa pete na mpira wa wavu.
Amesema mradi huo utadhingatia usawa wa kijinsia na kuondosha mila potofu kwa wanawake na wasichana kwani mila potofu hukwamisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa wanawake na hata kwa taifa.
Uwekaji wa jiwe la msingi wa viwanja hivyo ni katika shamrashara za kuelekea Maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Comments
Post a Comment