NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAUMINI wa dini ya kiislamu wilaya ya Mkoani Pemba, wameombwa kuiunga mkono kamati ya kuhifadhisha qur-an ya kanda ya Wambaa wilayani humo, ili kufanikisha mashindano ya tano yanayotarajiwa kufanyika Wambaa mwezi mtukufu wa ramadhaman.
Katibu wa kamati ya tahfidhl-qura-n kanda ya Wambaa Abdalla Haji Ali, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha tatu cha maandalizi ya kazi hiyo, kilichofanyika Wambaa hapo jana.
Alisema, mambo ya kidini yanayoandaliwa inawategemea kwa kiasi kikubwa wazaliwa wa Wambaa na Chumbageni, ikiwa ni nafasi yao ya kushirikiana katika kuiendelea mbele dini ya kiislamu.
Alisema, mpango wa kukishindanisha kitabu cha Allah kwa wanafunzi, husaidia kuwazoesha watoto mapema kumtambua Muumba, na kuwa ni sababu ya kuongeza uchaji.
Alieleza kuwa, ni vyema kwa kila mwenye uwezo kuhakikisha anafikisha sadaka yake kwenye kamati hiyo, ili kuwatunza wanafunzi watakaoshiriki, kama sehemu yavivutizi.
Katibu huyo alieleza kuwa, wapo watu wamekuwa wakichangia fedha nyingi kwenye shughuli za kimichezo, harusi, mikutano, makongamano ingawa kwenye masuala ya ibada wamekuwa wazito.
‘’Niwaombe sana wazaliwa wa Wambaa, Chumbageni na waumini wingine, kuiunga mkono kamati yetu ya kuhifadhisha qur-an, ili kufanikisha mashindano ya tano mwaka huu,’’alifafanua.
Mapema Mwenyekiti wa kamati hiyo Hassan Othman Khamis, alisema kwa mashindano yote yaliopita, yaliendeshwa na wafanyabiasha, waalimu, wazazi na wanafunzi, ingawa huwepo kwa zawadi ndogo.
Hivyo, aliwasisitiza watu wingine wenye uwezo, kuhakikisha mashindano ya mara hii yanakuwa na aina yake, ili wanafunzi wavutike na kukipenda kitabu cha Allah (s.w).
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo mwalimu Awesi Abdalla Ali, alisema wamekuwa wakijitahidi kusambaaza barua za maombi ingawa, muitikio wa waumini ni mdogo.
Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wa shehia za Wambaa na Chumbageni, wamesema bado waumini waliowengi wamekuwa na mwamko mdogo wa kuchangia masuala ya kiibadati.
Khamis Ali Omar, alisema waumini wanavutika mno na kuchangia michezo, makongamano na starehe nyingine na kuacha kuchangia namna ya kumtukuza Muumba.
Mayasa Haji Said aliiomba kamati hiyo kwa msimu huu, kuongeza kasi ya kutoa taarifa, ili kila mmoja afahamu uwepo wa jambo hilo.
Zaidi ya wanafunzi 42 waliohifadhi juzuu moja, mbili, tatu, tano, saba, 10 na 15 wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo, yanayotarajiwa kufanyika mwezi mtukufu wa ramadhani mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment