NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WATUMISHI wapya wa umma kisiwani Pemba, wametakiwa kuzingatia dhana ya uzalendo na kuifanyiakazi, kwani ndio msingi mkuu wa kufanikisha majukumu yao ya kila siku.
Hayo yameelezwa na Afisa kutoka Chuo cha Utawala wa Umma ‘IPA’ Zanzibar tawi la Pemba Nuhu Abubakar, wakati akiwasilisha mada ya mageuzi katika utumishi wa umma, kwa watendaji wapya kutoka taasisi mbali mbali wakiwemo wa ZAWA, uliofanyika ukumbi wa Manispaa ya Chake chake.
Alisema, suala la uzalendo ni jambo kubwa katika kufikia lengo la taasisi husika, na sio kwa mtumishi kufikiria maslahi yake binafsi na kuwasahau wingine.
Alieleza kuwa, watumishi waliowengi wamekuwa hawako vizuri kwenye eneo hilo, jambo ambalo huwapa changamoto wananchi wanaokwenda kutafuta huduma kwenye taasisi za umma.
Alifahamisha kuwa, moja ya msingi mkuu wa uzalendo la kuipenda kwa dhati nchi, wananchi wake, utamaduni na kulinda rasilimali za umma kwa gharama yoyote.
‘’Uzalendo pia unajumuisha matumizi mazuri ya muda wa kazi, rasilimali, miundombini na kutoa huduma kwa usawa kwa wananchi wote bila ya ubagauzi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Afisa huyo alisema, hoja ya kudai haki na stahiki kwa mtumishi kwa kutumia lugha sahihi na wakati husika, hakuondoi uzalendo kwake.
Mapema akiwasilisha mada ya uzalendo, Afisa kutoka ‘IPA’ Issa Ali, alisema dhana hiyo kwa sasa imekuwa ikipigwa teke na baadhi ya watumishi wa umma.
Aidha alifafanua kuwa, kila mmoja na kwa nafasi yake anaowajibu wa kuhakikisha taifa lake, linasongambele tena na kuondokana na viashiria vya kuhujuhumu uchumi.
Afisa kutoka Mamlaka ya Kuzuia rushwa na uhujumu wa Uchumi mkoa wa kaskani Pemba Kassim Yussuf Ali, alisema kwa sasa yapo mambo yameingizwa ndani ya sheria mpya ya ZAECA.
Katika hatua nyingine, aliwataka watumishi hao wapya, kuzisoma sheria na kanuni za utumishi wa umma, ili kujua haki na wajibu wao.
‘’Mnapojua haki zenu wakati wenu wa utumishi wa umma, moja ni kujikinga na uhujumu wa uchumi na rushwa pamoja na makosa mingine ya jinai,’’alifafanua.
Wakichingia mada kadhaa, watumishi hao wapya, walipendekeza kuwa mafunzo kama hayo yawe endelevu, kila baada ya muda.
Jamal Suleiman Jamal, alisema watumishi wa umma wanayomawazo mazuri, ingawa wasi wasi wao ni kutokusikilizwa na wakuu wao wa Idara zao.
Aidha alipendekeza kuwa, mafunzo kama haya wanapaswa kupewa waajiri, ili kutengeneza mazingira rafiki ya kazi kwa watumishi.
Nae Shafii Khamis Soud, alisema elimu zaidi inahitajika kwa kila wakati, ili kujua makosa ya madai na jinai, ambayo wanaweza kuyaepuka wanapokuwa kazini.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili mada kadhaa zimejadiliwa, ikiwa ni pamoja na uzalendo, usalama na afya kazini, kustaafu salama, maadili ya watumishi wa umma pamoja na uzalendo.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yanatarajiwa kufungwa mchana wa leo Januari 21, 2025 na Katibu Tawala mkoa wa kusini Pemba,
Mwisho
Comments
Post a Comment