IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@
WAZAZI
na walezi wa shehia ya Kambini Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa
kujitathmini na kuweka mikakati katika malezi, ili jamii iwe na vijana wenye
malezi bora na maadili mema.
Akizungumza na wanajamii hao katika
mkutano wa elimu ya udhalilishaji na kutambua haki zao, Msaidizi wa Sheria
Wilaya ya Wete ambae pia ni Mkaguzi wa Shehia hiyo kutoka Jeshi la Polisi Mkoa
wa Kaskazini Pemba, Khamis Shoka Ame alisema wazazi waliowengi wamefeli katika
malezi.
Alisema kuwa, mporomoko wa maadili
wameusababisha wenyewe wazazi kwa kukosekana kwa malezi ya pamoja, hivyo kuna
haja ya kujitathmini na kuweka mikakati imara ili kizazi chao kiweze kukuwa
katika maadili mema na malezi bora.
‘’Watoto tunawalea sisi lakini hawaendi
skuli wala madrasa, wanaingia ndani usiku mkubwa, halafu wanakwenda nae Jeshi
la Polisi kusema kuwa mtoto amemshinda, lakini tujue kwamba mwenye jukumu la
malezi ni wewe mzazi, hivyo tujitahidi sana kwani tunapofeli hapo ndipo
tunapofeli kwenye maisha,’’ alieleza.
Aidha Shoka alisema kuwa, wananchi
wana tabia ya kusuluhisha kesi wenyewe kutokana na muhali walionao, jambo
ambalo linasababisha matukio ya udhalilishaji na wizi kuongezeka kila siku.
''Kesi hizi sana zinafanyika wenyewe kwa wenyewe, hivyo kesi inakaa mahakamani au Polisi kwa muda mrefu huku ikisubiri maelezo kutoka kwa waathiriwa, lakini mwisho wa siku kumbe wameshakaa kikao cha kusuluhisha, hii haikubaliki na tunachangia kuongezeka kwa matendo maovu katika jamii yetu,’’ alieleza.
Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama ya
Wilaya Wete Maulid Hamad Ali alisema, kutokujua sheria ni changamoto kubwa
inayowakabili wanajamii, ambapo husababisha kukoseshwa au kuvunjiwa haki zao.
‘’Mtu yeyeyote hana kosa mpaka pale
mahakama itakapomtia hatiani, kwa hivyo huwa anatuhumiwa tu kutenda kosa na pia
Polisi inapokuja kufanya upekuzi ni lazima awe na kibali maalumu, hivyo
mnatakiwa kuzijua sheria zenu ili ziweze kuwasaidia,’’ alisema Hakimu huyo.
Nae sheha wa shehia hiyo Ali Omar Ali
alieleza kuwa, watu wengi wanaishi ingawa hawajui sheria ambazo ndizo zinazowasababishia
kufanya mambo maovu, hivyo wamefarajika sana kupata elimu hiyo kwani anaamini
itawasaidia katika utatuzi wa changamoto mbali mbali kwenye jamii.
‘’Nawaomba wananchi kuacha tabia ya
kuwakingia kifua wabakaji kwa sababu wanaendelea kudhalilisha watoto huku wakidunda
mitaani, tuwafikishe kwenye vyombo vya Sheria na tuwe tayari kutoa ushahidi,’’
alisema sheha huyo.
Mapema wakitoa malalamiko yao
wananchi wa shehia hiyo walieleza kuwa, waliomba kufahamishwa Sheria ili
wazielewe vizuri hali ambayo itasaidia kujua na kutetea haki zao kisheria
endapo zitavunjwa.
Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano
ya kutoa elimu kwa wananchi ili wajue haki zao kisheria, ambao umeandaliwa na
Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Wete (WEPO) chini ya ufadhi wa Shirika
la UNDP.
MWISHO.
Comments
Post a Comment