IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JAJI wa Rufaa mstaafu
Mbarouk Salim Mbarouk amewataka wadau wa uchaguzi kuwahamasisha wananchi
kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate haki
yao ya msingi ya kupiga kura ifikapo Oktoba mwaka 2025.
Akizungumza na wadau
hao katika mkutano wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura
lililofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi Chake Chake,
Jaji huyo alisema, kila mmoja alifikia vigezo ana haki ya kushiriki zoezi hilo.
Alisema kuwa, ipo haja
kwa wadau hao kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anawahamasisha wananchi
waliokaribu yake kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili
kumuwezesha kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
"Tume inathamini
sana mchango wenu na ndio maana imewaita hapa kushirikiana na nyinyi, kujadili
namna ya kuifikia jamii kwenda kuwaelimisha na kuwahamasisha ili wasikose haki
yao ya kujiandikisha katika daftari hili la wapiga kura," alisema Jaji
huyo mstaafu.
Aidha alieleza kuwa,
nchi ipo katika maandalizi ya uchaguzi na imetoa mamlaka kwa Tume ya uchaguzi
kutekeleza majukumu ya kusimamia na kuratibu shughuli mbali mbali kwa mujibu wa
Sheria ya uchaguzi ilivyoelekeza na ndio maana imeanza na zoezi la uboreshaji
wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Akiwasilisha mada ya
Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi
NEC Giveness Awile alisema, viongozi wa vyama vya siasa hawapaswi kuingilia
utekelezezaji wa majukumu ya watendaji wa vituo wakati wote wa uandikishaji wa
daftari la wapiga kura vituoni.
Aidha alisema kuwa,
wanatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wote watakaoboresha zoezi hilo la
uandikishaji, ili wafanye kazi kwa ufanisi na utaalamu zaidi.
"Tunatarajia kuwa
na wapiga kura 5,586,433 sawa na asilimia 18 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo
kwenye daftari kwa sasa, mwaka 2019/2020, ambapo kwa sasa Pemba tuna vituo vya
kupiga kura 140 kati ya 135 vya zamani," alieleza Kaimu huyo.
Alisema kuwa, Tume ya
Uchaguzi imeongeza upeo mpana kwa kumeongeza vituo vya kupiga kura kwa wananchi
walipo kwenye vyuo vya mafunzo, ili na wao wapate haki yao kupiga kura kwa kila
aliekidhi vigezo vinavyokubalika kisheria.
Nae mwasilishaji
Martine Mnyenyelwa alisema kuwa, vifaa mbali mbali vitakavyotumika katika zoezi
hilo vitaboreshwa kwa ajili ya ufanisi zaidi katika kazi.
Akifunga mkutano huo
Balozi Omar Ramadhan Mapuri aliwasisitiza wadau hao kuwa, kila mmoja atumie
nafasi yake kuelimisha ili wananchi washiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
Balozi huyo pia
aliwataka wadau wa Uchaguzi kuzingatia katiba, Sheria na kanuni katika zoezi
hilo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment