NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’BILA ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na
maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari
kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi’’.
‘’Tena pia mtu huyo ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa
kati, na raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio ya nchini
na duniani kote, ambayo ni muhimi kwa maisha yake’’.
Ndivyo
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inavyoelekeza kifungu cha 18, juu ya
upatikanaji na utoaji wa habari kwa raia, tena bila ya kujali mipaka ya nchi.
Mwanasheria
wa kujitegemea Khalfan Amour Mohamed, anasema suala la kupata habari, au kutoa
ni haki ya kikatiba, ambayo inatofautiana na haki nyingine.
‘’Ukitaka
kuzigawa haki hizi, basi zipo haki za kikatiba na haki nyingine
zilizotengenezewa sheria yake mbali mbali, mfano haki ya elimu,’’anafafanua.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwajali wananchi wake, haikuishia tu ndani ya
Katiba kifungu cha 18 ya upatikanaji wa habari, bali kwa kutambua umuhimu huo,
ilianzisha sheria maalum.
Ikumbukwe
kuwa, miundombinu ya kupashana habari ni Magazeti, redio na tv, ingawa na kwa
sasa kumeibuka mitandao ya kijamii.
Kwa
Zanzibar, vyombo vya habari vya magazeti vinasimamiwa na sheria ya Magazeti,
Vitabu, na Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988.
Igawa
kwa redio na tv na hata sasa, uwepo wa vyombo vya habari mtandaoni, vyenyewe
vinasimamiwa na sheria ya Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997.
SHERIA YA MAGAZETI, VITABU NA MAWAKALA WA
HABARI NO 5, 1988
Sheria
hii yenye vifungu 81 na sehem 10, sasa inatimiza miaka 36 tokea kutungwa kwake,
na kwa maana nyingine, vipo vifungu zaidi ya 40 ambavyo vyengine vinahitaji
kufutwa.
Vyengine
vikihitajika kufanyiwa marekebisho na vyengine vilivyobeba maneno makali kama ‘uwezo
wa waziri, waandishi kudhibitiwa na kufanya uchochezi’.
Kwenye
sheria hii ambayo kwa sasa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar wanaharakishwa kufutwa, vipo vifungu kadhaa mabavyo vimepitwa na
wakati na kuwa na sheria mpya.
VIFUNGU KANDAMIZI KWA UHURU WA HABARI ZANZIBAR
Moja
ya kifungu ambacho kwa sasa wadau wanataka kifutwe, ni cha 39 ambapo chenyewe
kinaeleza ‘sharti la kukusanya na kutoa habari na vifaa vya habari’.
Kifungu
kimeanza vizuri, kuwa hakuna mtu atakayepewa kibali cha
maandishi cha kukusanya habari, isipokuwa awe (i) mwandishi wa
habari wa ndani au (ii) mwandishi huria wa habari.
Kifungu hicho cha 39 (2),
ikaeleza kuwa Mkurugenzi anaweza bila ya kutoa sababu, kukataa kutoa kibali
hicho, kukifuta au kukizuia.
Lakini
kifungu cha (3) kikatoa haki kwa mkono wa kulia na kupokonya kwa mkono wa
kushoto, kwa muathirika wa kibali hicho (mwandishi wa habari)
kwamba anaweza kukata rufaa.
‘’Muathirika anweza kukata rufaa ya kuzuialiwa, kukataliwa,
kufutwa kwa kibali chake moja kwa moja wa Waziri wa habari ndani ya wakati,’’kinafafanua kifungu.
Kifungu
cha (4) ambacho kinapokonya haki hiyo, kinaeleza kuwa ‘kila uamuzi wa
waziri kuhusiana na rufaa ya mwandishi wa habari, utakuwa ni wa mwisho na
hautafanyiwa mapitio (haukatiwi rufaa) na mhakamani’.
Kwamba
iwapo waziri amemkatilia mwandishi wa habari kumkosesha kibali, kukifuta,
kukizuia au kukikataa uamuzi wake huo utakuwa wa mwisho.
Lakini
hata mazonge mengine ya sheria hii yapo kwenye kifungu cha 40, kinachoelezea
uwezo wa waziri wa Habari wa kufuta kibali kilichotolewa na Mkurugenzi.
Kwamba
mwandishi wa habari ameshaomba kibali kwa Mkurugenzi, ameshalipa ada
itakayopangwa, lakini sheria inampa uwezo Waziri kukifuta kibali hicho.
‘Waziri anaweza
kufuta kibali kilichotolewa na Mkurugenzi ikiwa kwa maoni yake tu, ufutaji huo
utakuwa ni kwa maslahi ya umma au ni kwa maslahi ya usalama na utangamano wa
taifa’
Kwamba
sheria hii, imempa uwezo wa kupitiliza Waziri, na kwamba anaweza, kufuta kibali
kwa maoni yake tu, akihisi kukifuta huko, kwa faida kwa taifa.
WADAU WA HABARI WANASEMAJE?
Aliyekuwa
Afisa Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania MCT-Zanzibar Shifaa Said Hassan,
anasema sheria hiyo imeshapitwa na wakati na moja ya vifungu vibaya ni cha 39
na 40.
‘’Haiwezekani
suala la haki ya kikatiba ya kupata na kutoa habari, apewe uwezo wa kupindukia
waziri, juu ya kuona nani apewe au asipewe kibali,’’anasema.
Mchambuzi
wa sheria za habari Zanzibar Hawra Shamte anasema, kwenye nchi ya utawala wa
sheria na demokrasia kama ilivyo Zanzibar, sheria hiyo vifungu vyake kadhaa
vinapingana na katiba ya nchi.
‘’Iweje
kuwe na sharti la kukusanya habari, tena moja ya sharti hilo uwe na kibali
ambacho hakitolewi na kamati wala bodi anatoa mtu mmoja,’’anaelezea.
Anasema
maajabu mingine ambayo yamo kwenye sheria hiyo ni kifungu cha 40, ambacho
kimempa uwezo mkubwa waziri, juu ya kukubali ama kukataa kutoa kibali.
‘’Kinachoonesha
udhaifu kuwa, hata mwandishi akikataliwa na waziri kuwa hawezi kuomba kibali,
hapo ndio mwisho wa kulalamika,’’anafafanu.
Kwamba
uamuzi wa Waziri hauwezi kukatiwa rufaa katika mahakama yoyote na hata
mwandishi hawezi kumshtaki waziri huyo wa kiongozi wa nchi aliyemteua.
Aliyekuwa mkuu wa Chuo
cha uandishi wa habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar ‘ZJMMC’ Dk. Saleh Yussuf
Mnemo, anasema ujio wa mapinduzi ya habari ya kidigitali, suala la kibali
halipo.
‘’Wanachotakiwa
mamlaka ni kufuatilia utendaji wa kazi wa waandishi wa habari na watoa taarifa,
lakini sio kuwabana na kuwawekea sheria ngumu,’’anasema.
Katibu
mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Pemba ‘PPC’ Ali Mbarouk Omar, anasema
vifungu ambavyo vinampa uwezo waziri, ni dhahiri vinapingana na katiba.
‘’Muda
wa kuwa na sheria inayotaja cheo cha mtu umepita, maana unaweza kuwakosesha
wananchi kupata habari, kwa kule waziri, kumchukia mwandishi wa habari
tu,’’anasema.
Mhariri
mtendaji wa shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar, Ali Haji Mwadini anasema,
ukuaji wa maendeleo ya taifa lolote hutegemea mno, uwepo wa waandishi huru wa
habari.
‘’Kama
bado kuna sheria inaelekeza kuwa waziri anaweza, mkurugenzi akiona,
kwa maoni yake au akihisi hiyo sio demokrasia,’’anasema.
WAANDISHI WA HABARI WANASEMAJE?
Abdi
Juma Suleiman, mwandishi wa habari wa shirika la Magazeti Pemba, anasema sheria
hiyo ya Magazeti, Vitabu na Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988, imekuwa
kikwazo kwao.
‘’Ilishawahi
kuwakumba waandishi wa habari wa vyombo binasfi, kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Chambani Mkoani Pemba, kwa kukoseshwa vibali,’’anasema.
Mwandishi
wa habari wa kituo cha tv na redio cha Zenj fm Is-haka Mohamed Rubea, anasema
sheria hiyo hasa kwenye upatikanaji wa kibali, imekuwa shida.
Mwandishi
wa redio Jamii Mkoani Said Omar Said, anasema sheria yenye vifungu kandamizi,
huwaumizi zaidi waandishi wa vituo binafsi.
Mwandishi
wa Shirika la Magazeti ya serikali Pemba Zuhura Juma Said, anasema sheria hiyo
kwa sasa inakwenda kinyume na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Fatma
Hamad Faki mmiliki wa blog ya Pemba ya leo 24, anasema kwa sasa na kwa ulimwengu
huu, hakutakiwi kuwa na sheria kandamizi kwa waandishi wa habari.
NINI KIFANYIKE?
Mkurugenzi
wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzur Issa Ali, anasema ujio wa sheria mpya ya habari,
vifungu vinavyompa uwezo mkubwa waziri vifutwe.
‘’Lakini
napendekeza kama habari ni haki ya kikatiba, sharti la kutoa kibali lisiwemo
mikononi mwa mtu, bali iwe ni bodi ya ushauri wa habari,’’anapendekeza.
Mchambuzi
wa sheria za habari Zanzibar Hawra Shamte, anasema maneno kama ‘uwezo wa
Mkurugenzi, Waziri, akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye
sheria mpya ya habari yasitumike.
‘’Sote
tunakubali kuwa kila mmoja anamapungufu yake, sasa kama waziri wa habari,
akipewa uwezo mkubwa wa kukubali au kukataa kibali, itafika wakati Zanzibar
kusiwe na waandishi wa habari,’’anaeleza.
Mratibu
wa uchechemuzi wa upatikanaji wa sheria ya habari Zanzibar kutoka TAMWA-Zanzibar
Zaina Mzee, anasema, wakati umefika Zanzibar kuwa na sheria rafiki.
‘’Ndio
maana TAMWA-Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, tumekuwa tukikosa
usingizi hadi pale sheria mpya ya habari itakapopatikana,’’anasema.
Aliyekuwa
Mwandishi wa kituo cha redio cha Sauti ya Istqama Salim Ali Msellem na mwenzake
wa tv ya mtandaoni jicho letu Amina Ahmed, wanasema rufaa ya kukataliwa,
kufutiwa kibali isiishie kwa Waziri kama ilivyo sasa.
‘’Suala
la habari ni haki ya kikatiba, basi ieleze wazi kuwa waziri akifuta, akikataa
kutoa kibali muathirika, sheria ielekeze hadi afike mahakamani,’’wanasema.
WANANCHI WANASEMAJE
Asha
Ali Haji mwenye ulemavu wa viungo wa Mtambile, anasema, waandishi wanapowekewe
vikwazo kwenye kukusanya, kutafuta na kuandika habari waathirika wakubwa wao wa
chini.
Hemed
Haji Omar wa Wambaa Mkoani anasema, sheria kandamizi kwa waandishi wa habari ni
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mwisho
Comments
Post a Comment