NA HABIBA
ZARALI, PEMBA@@@@
‘HAMASA
kubwa ilifanyika tokea pale ilipoanzishwa timu ya Mkoani Queens mwaka 2014 na
hadi sasa kuweza kusimama’.
‘Pamoja na dharau, kejeli ambazo tumepewa lakini bado
tunaendelea mbele kuhakikisha timu yetu inakata mawimbi na kusonga mbele’.
Ni kauli ya baadhi ya wachezaji wa timu ya mpira wa miguu
wanawake Mkoani qunes, walipokuwa wakizungumza na makala haya kuhusiana na uhai
wa timu yao.
Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka huo wa 2014, ikiwa na wachezaji
26, imepitia madhila makubwa kwa jamii husika ila bado inaonekana kuwepo.
Wanasema pamoja na wanajamii kuwachukulia wanawake wanaocheza
soka, wanafanya uhuni wao hawakujali hilo, maana nia walikuwa wanaijua wenyewe.
Wachezaji hao wanatumia fursa ya vipaji vyao kuhakikisha
wanaingiza kipato na kuhudumia familia zao, kujiajiri na kufanya mambo mengine
ya kimaendeleo kutokana na kipato
wanachopata kupitia vipaji vyao.
Mmoja wa muanzilishi wa timu hiyo ambae sasa ni kocha wa timu hiyo
ya Mkoani Qunes Ramla Juma Khamis, anasema soka la wanawake kwa sasa, limekuwa
ni tofauti na pale zamani, ambapo jamii ilikuwa inasema kujishirikisha katika
michezo kwa watoto wa kike ni uhuni.
‘Nakumbuka wakati naanza kuchezesha timu hii, nilibezwa na
jamii mimi na wenzangu, hadi kuambiwa mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto wa
kike, hakuna mafanikio, tuliambiwa mengi lakini leo hii faida tujionea,’’anasema.
Wazazi walitaka nishughulikie masomo tu na hawakutaka kusikia
kwa mtoto wa kike, kucheza mpira wa miguu ingawa sikukata tamaa.
“Sasa nimekuwa kocha wa
timu hii ya Mkoani Qunes, ambapo najipatia riziki kupitia michezo ni jambo la
kujivunia”anasema.
WACHEZAJI
WANASEMAJE
Tatu Mohamed Ngwali ambae ni mchezaji wa timu hiyo anasema,
hamasa kwenye soka la wanawake imeanza kuonekana ushahidi wa hilo nipale timu
yao inavyoendelea kuwepo tokea ilipoanza.
Kupitia timu hiyo, tayari ameshapata mafunzo mbalimbali
yanayohusiana na mchezo huo, ambapo kwa sasa anajiamini kuucheza popote.
“Kusema kweli tunahitaji pongezi hadi tulipofikia kwani
hatukufikiria kama timu yetu hii ingeweza kudumu tulikuwa na chanagamoto kubwa
kwa jamii ya Mkoani,’’anaeleza.
Hamida Juma Amani,
anasema pamoja na gumzo kubwa kuanzishwa timu ya wanawake Mkoani na kufanikiwa
kuwepo, bado kuna chanagamoto ya timu ya wanawake kucheza ligi.
Anaona kumekuwa na mabadiliko kwa jamii, kuhusiana na mchezo
huo kwa wanawake kwani ni tofauti na zamani sasa wanacheza kwa amani.
“Tunalolihitaji ni usawa wa kijinsia kwenye michezo lakini,
ili usawa huo uweze kupatikana ni lazima serikali, itusaidie lakini na jamii ipate
elimu ya kutosha”,alisema.
Riziki Ali Khamis ambae alipata nafasi ya kushiriki kuchezea
timu ya taifa ya Zanzibar, anasema wanawake wanaweza kucheza mpira wa miguu
sawa na wanaume, hakuna haja ya kubaguliwa.
Anasema kipaji cha michezo kwa watoto wa kike ni vyema
vikaendelezwa, kwani huwezi kujuwa ni wapi ndiko kutakakomg’arisha maisha yake.
Kuwepo kwa timu moja kwa wilaya ya Mkoani, inawaweka katika
hali ngumu, kwani inabidi wacheze na wanaume chini ya miaka kati ya 15,17 na18.
Pamoja na kuwa na ufinyu wa kucheza kirafiki timu hiyo
haijawahi kuwa ya mwisho, pale wanapocheza ligi ambapo wachezaji hao wanasema
timu ambayo imewahi kuwapa vikwazo ni timu ya New generation, iliwahi kuwafunga
mabao 3 ila nao walichungulia goli lao kwa kuingiza wavuni goli moja.
Timu hiyo imekuwa ikipata shida hasa pale inapopata mwaliko ama
inapofika wakati wa kuchezaligi kwani imekuwa na uhaba wa wafadhili.
Na ndio maana timu hiyo kwa mwaka 2024/2025 ikashindwa
kushiriki ligi kuu ya soka la wanawake Zanzibar, kwani ndio inajitegemea
wenyewe kujiendesha.
“Kwenye ligi kunahitaji kula, malazi, nauli ingawa niliomba
lakini sikufanikiwa kubahatika, kwani hatuna wafadhili huwa natowa fedha zangu
mkononi kuendeleza timu,”anasema kocha.
Wakitaja mafanikio katika timu yao kocha Ramla, anasema pamoja
nakuitambulisha jamii kama timu ipo lakini ni kujiunga na timu ya taifa, kupata
ajira kwa vijana wanne serikalini.
Mengine ni kutowa
vijana wawili kwenda Tanzania bara kwa kucheza mpira wa miguu katika timu za
huko, kupata mafunzo ya mpira wa miguu kupitia ZFF na kujiunga na timu ya taifa
ya Zanzibar.
MATARAJIO
YAO NI YEPI
Wachezaji wanasema ni kuendeleza timu ili kuweza kufikia mbali
kimichezo na kujipanga kwa msimu unaofata, kuunganisha watoto kujiepusha na
vishawishi ambavyo vimeikumba jamii.
Matarajio ya timu hii inakwenda sambamba na malengo ya mradi
wa michezo kwa maendeleo wa kuongeza
ushiriki kwa wanawake na watoto wa kike,
ambao unatekelezwa na jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA, kituo cha
mijadiliono kwa vijana CYD, pamoja na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa shirika la
maendeleo la Ujerumani.
Katika kuhakikisha timu hiyo inasonga mbele, ni jukumu la
viongozi wa Wilaya, Mkoa taasisi za maendeleo wajitokeze kusaidia ili
kuhakikisha inasonga mbele na isibaki nyuma .
ZFF
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu ZFF Mkoa wa Kusini
Pemba Nassor Hakim anasema ingawa kuna chanagamoto kubwa ya fedha kusimamia
ligi za wanawake katika Wilaya na Mikoa.
Inasema husaidia timu hiyo pale panapotokezea ruzuku ndogo
ndogo hata kuwaombea kwa wafadhili na wahisani.
Kwa vile huwa ni bahati nasibu kupata pale wanapoombewa na
ndio hufika mahala wakakosa na wao huwalazimu kusaidia kutoka mikononi mwao ili
mambo yaende sawa.
“Kutokana na hilo sasa ZFF iwe ni chombo kikuu kutowa motisha kwa
vilabu vya wilaya kwani wao wanapata ruzuku kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo
PBZ, FIFA, CAF na kwenginejambo amabalo sisi wilaya na mikoa
tunazikosa”alisema.
TAMWA
INASEMAJE?
Afisa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi kwenye
michezo unaofadhiliwa na shirika la maendeleo
la kimataifa la Ujerumani Khairat Haji, anasema kila mtu anayo haki ya kushiriki
katika michezo na hakuna sababu ya
wanawake kubakia nyuma.
Ndio maana anasema kupitia mradi huo TAMWA Zanzibar
itahakikisha usawa wa kijinsia, unapatikana katika michezo ya aina mbali mbali.
Pamoja na kuwa wanawake
wako nyuma katika ushiriki wa michezo, aliwataka wasirudi nyuma na washiriki
kwa hali ya kuridhisha.
Kubwa zaidi anasema pamoja na kucheza huko, ni vyema wakazingatia
mavazi ya stara, kama inavyoelekeza kanuni kwamba watoto wa kike wavae nguo za
heshima.
Ni jukumu la wazazi sasa katika jamii ya Mkoani na nyingine kutokuwa
na wasiwasi ya kuwa mchezo huo ni uhuni hasa ukizingatia wadada hao huvaa treki
na flana na vishungi wala hawavai bukta tupu.
mwisho
Comments
Post a Comment