NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘MICHEZO
kwa wote ‘or sport for all’’.
Michezo kwa maendeleo endelevu,
michezo ni ajira, afya, udugu na kujenga uhusiano wa kudumu.
Wapo walioinadi kuwa, michezo
ni sehemu ya maisha ya mwanadamu yeyote yule, bila ya kujali rangi, kabila wala
jinsia.
Kwa mfano sheria 17 za mpira wa
miguu, hazijambagua mtu yeyote, chamsingi awe anajimudu kufikia miundombinu husika.
Miongoni mwa vifungu vya sheria hiyo, ili kandanda ifanyike
moja ni uwepo wa uwanja, pili ni mpira, idadi ya wachezaji, vifaa vya michezo,
mwamuzi pamoja na sheria ya 17 ya pigo la kona.
Wapo wanawake warefu, wafupi, wanene, wembamba na hata kwa wanaaume,
wapo katika maeneo kama hayo, wakishiriki michezo mbali mbali.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwenye sura yake ya tatu na
hasa kifungu cha 11, kimebainisha usawa wa binaadamu.
Hata kile cha 12, kikaendelea kuweka usawa mbele ya sheria,
cha 13 haki ya kila mmoja kuwa hai, 14 haki ya uhuru wa mtu binafsi pamoja na
kila cha 18 cha haki ya kutoa maoni.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, ibara ya
5 imekataza ubaguzi, ukisema watu wote ni sawa mbele ya sheria.
Kubwa zaidi mkataba huu, ibara ya 30, ukachambua haki ya
kushiriki katika utamaduni, burudani na michezo kwa watu wenye ulemavu.
Ukaenda mbali zaidi, ukisema lazima nchi zilizoridhia mkataba
huu Tanzania ikiwemo, ‘kuhakikisha watu wenye ulemavu, wanafurahia upatikanaji
vifaa vya michezo’.
Kifungu 30 (b) kikaeleza jingine, ambalo ni haki watu wenye
ulemavu kuhakikisha wanajengewa uwezo wa kushiriki michezo, na (e) watoto wenye
ulemavu wanapata haki sawa kushiriki michezo kadhaa.
Kumbe hata sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar nambari 8 ya
mwaka 2022, kifungu cha 28 (1), (f) kimesisitiza haki moja wapo kwao, ni kushiriki
michezo na burudani.
Sheikh Said Ahmad Mohamed wa Chake chake, anasema Qur-an
haijambagua mtu kwa sababu ya ulemavu wake, ngozi, jinsia wala eneo analotoka.
‘’Umeweka wazi dhana ya mtoto wa kike wa kiislamu, kushiriki
michezo, na hasa ikiwa kwa umri wake ameshakuwa mtu mzima, moja ni kivazi na
kutojichanganya na wanaume,’’anasema.
Kumbe dini, mikataba, sheria, kanuni, katiba na maazimio yote
ya ulimwenguni, hayajambagua mtoto wa kike mwenye ualbino, kushiriki michezo.
WAZAZI WA WATOTO WENYE UALBINO WANASEMAJE
Omar Hassan Omar (58) wa Wawi mwenye mtoto wa kike mwenye
ualbino, anasema mtoto wake alianza unyanyapaa akiwa skuli, na kushindwa
kushiri hata mchezo mmoja.
Anasema, alikuwa akisoma skuli ya Bububu kisiwani Unguja,
ingawa mwaka 2019, aliamua kuhama nae kumleta kisiwani Pemba.
‘’Alikuwa mzuri kwenye mchezo wa kuruka chini ‘long jump’
ingawa wenzake walimpa majina mabaya mingi, na kujiskia mnyonge,’’anasema.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Aisha Mwadini Ali, anasema hata
kwenye utunzi wa mashairi, alitokea mshindi wa kwanza wa kitaifa.
‘’Alipewa majina mabaya ambayo sipendi kuyatamka, na kisha
yalimkatisha tamaa kuendelea na masomo,’’anafafanua.
Ameir Haji Omar (40) mkaazi wa Mkanjuni Chake chake, anasema,
watoto wa kike wenye ualbino, wanauwezo mkubwa wa kushiriki michezo, ingawa
unyanyapaa unadidimizi vipaji vyao.
‘’Mimi nilikuwa nasomesha skuli moja ya binafsi hapa Pemba,
lakini hata waalimu wenzangu hawakuwa wakimpa kipaumbele watoto wa aina hii,’’anafafanua.
Maryam Himid Khalfan ‘anti mamu’ wa Mtambile anasema mtoto wa
kike wa jirani yake, ameshindwa hata kusafiri na wenzake, kushiriki sherehe za
elimu bila malipo Unguja.
‘’Ni mwanafunzi alikuwa mshindi wa mbio za mita 100, kimkoa,
lakini kutokana na unyanyapaa kwa wenzake, aliamua nafasi yake kumpa mshindi wa
pili asafiri,’’anahadithia.
Kaka wa kambo wa mtoto huyo Omar Ussi Hamad, anasema watoto
wa kike, bado wanakabiliwa na unyanyapaa wa kubandikwa majina mabaya kwa aina
walivyo.
‘’Mdogo wangu alikuwa muwekezaji mzuri kwenye mbio fupi,
lakini alikuwa anapewa majina mabaya, na kukatisha ndoto zake,’’anasema.
WAATHIRIKA
Mtoto huyo anasema, bado hawajatendewa haki na jamii iliyokubwa,
kwa kule kumpa majina nayoyakataa na kimsingi hayako kwenye ubinaadamu.
Anasema, wakati anasoma darasa la tisa, hakuwahi kushika nambari
ya pili, kwenye mbio za mita 100, daima alikuw amshindi, ingawa alikuwa anakabiliwa
na unyanyapaa.
‘’Sio kama hatuna uwezo wa kushiriki michezo kama riadha, kuogolea,
Sanaa, lakini jamii tena iliyotuzunguruka wanatunyanyapaa kwa kutubandika
majina ya hovyo,’’anasema.
Hamida Issa Mjaka (17) mwenye ualibino mkaazi wa Michekaini
Chake chake, anasema aliwahi mara moja akiwa darasa la nne, kushirki michezo na
alishinda.
‘’Eti yule niliyemshindwa anachekwa, kwamba unapitwa na hata
mwenye ualbino, sasa nikisikia hivyo, huwa napata aibu,’’anasema.
Mayasa Ibrahim Hamad wa Wesha, anasema wao wamekuwa
hawashirikishwi, kushiriki michezo kutokana na ulemavu wao walionao.
‘’Watu wanapenda kutupa majina tunayoyachukia, hivyo hata
pakianzishwa timu za wilaya, mkoa, taifa hutuingizwi na tukiingizwa tunakosa
amani,’’analalamika.
Mtumwa Khamis Nassor, anasema mwaka 2022, alitamani kuingia
kwenye mpira wa mikono, ingawa wachezaji wenzake wanawake hawakuwa wakimpa
nafasi.
JAMII INAMTAZAMO GANI?
Omar Khamis Omar wa Kengeja, anasema ni vigumu wao kushiriki
michezo, kutokana na hali zao, hasa kwa ile inayotumia nguvu.
‘’Mimi sioni umuhimu wa wao kushiriki michezo, maana ipo
mingine inatumia nguvu na wao wanashida ya ngozi, sasa labda wawe peke yao,’’anafikiria.
Aisha Said Khalfan wa Mtambile, anasema kama jamii
itawakubali na kuwapa nafasi, wanaweza kufanya vizuri watoto wa kike, wenye
ualbino hadi kimataifa.
‘’Tunaona kwa wenzetu ambao wanawaamini, wanashiriki michezo
mbali mbali na wanafanya vizuri,’’anasema.
Mohamed Mzale Mjaka wa Mwambe Mkoani, anasema watoto wa kike
wenye ualbino, ni sawa na wengine, ikiwa familia zao zitaamua kuekeza kwao,’’anasema.
Mwanamichezo mkongwe kisiwani Pemba Asha Nassor Sultan [TOP]
wa Chake chake, anasema hakuna uhusiano kati ya ualbino na michezo.
‘’Suala la michezo ni kwa jamii zote, wawe watu wenye ulemavu,
wafupi na wingine, kubwa zaidi ni jamii kuondoa unyanyapaa,’’anasema.
Maana anasema, kwao kuna unyanyapaa uliokithiri ikiwemo
kupewa majina mabaya, na wakiwa wakubwa wanaweza kuitwa wahuni.
Anaona bado suala la michezo kwa watoto wa kike,
linachukuliwa kinyume mbele na jamii, na kuvifanya vipaji vyao kufifia.
Mashavu Juma Mabrouk wa Baraza la taifa la watu wenye Ulemavu
Zanzibar, anasema kama jamii itaendelea na mtazamo mbaya, watoto hao wanaweza
kufa na vipaji vyao.
‘’Tunaendelea kuelimisha, lakini bado watoto wa kike wenye
ualbino, hawajaaminiwa kwenye kushiriki michezo, kuanzia skuli, mitaani hadi timu
za wilaya,’’anasema.
TAMWA ZANZIBAR INAFANYAJE?
Afisa Mradi wa
kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi kwenye michezo, Khairat Haji
anasema Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania-TAMWA- Zanzibar, wameona
ipo haja ya kushirikiana na vyombo vya habari, kuibua changamoto za aina
hiyo.
Kiujumla watoto wa kike na hasa
wenye ulemavu tena wa ualbino, wamezungurukwa na darzeni ya changamoto, zinazowarejesha
nyuma kushiriki michezo.
Kumbe kabla ya kuwa mradi huo,
walifanya utafiti mdogo, ambao waligundua kuwa, kuna mifumo dume na yale mawazo
mgando, ambayo ni vikwazo dhidi ya wanawake na watoto wa kike kushiriki michezo.
Kupitia mradi wa
michezo kwa maendeleo, unaodhaminiwa na shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani
(GIZ) wanakusudia, kila mmoja aweze kushiriki michezo.
Mradi huo kwa sasa, unatekelezwa na Jumuiya ya
wanasheria wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’ Kituo cha mijadiliano kwa vijana ‘CYD’
pamoja na TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili Shirika la Maendeleo la Kimataifa la
Ujerumani ‘GIZ’
Lengo ni kuongeza ushiriki wa wanawake na watoto
wa kike, katika mazoezi na michezo, kwani kila mtu, anayo haki sawa, katika
eneo hilo.
‘’Jukumu letu ni kuwawezesha waandishi wa habari
kimafunzo, na kisha wawe weledi wa kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi,
katika michezo, kupitia kazi zao,’’anaeleza.
Kwa sasa tayari
waandishi 30 wa Zanzibar, wameshawezeshwa namna bora ya kuandika habari na
kutengeneza vipindi, vinavyoelezea fursa sawa ya michezo na eneo la ujumuishi.
UPI MCHANGO WA WIZARA
HUSIKA KATIKA HILI
Kaimu
Mratibu Idara ya Utamaduni na Michezo Pemba, Khamis Hamad Juma, anasema
haijawahi kutokeza kuwepo kwa mashindano maalum ya mchezo wa aina yoyote, kwa
watoto wa kike wenye ulemavu.
‘’Hata bonanza la michezo, ambalo ni maalum kwa ajili ya watoto
wa kike wenye ulemavu, sijawahi kuliona wala kusikia,’’anafafanua.
Hapa
Waziri wa Habari Tabia Maulid Mwita, anasema moja ya mchango wa wizara katika
kuinua michezo kwa watu wenye ulemavu, baraza la michezo liliwa kuvisaidia
vyama vitatu (3) vya michezo ya watu wenye ulemavu, katika kuandaa na kushiriki
mashindano kadhaa.
Moja
na mashindano hayo yakiwemo kitaifa ya michezo ya watu wenye ulemavu wa akili,
yaliyofanyika mwaka 2022.
Hayo
yamefahamika wakati Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid
Mwita, akisoma bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Akasema
Zanzibar, ilifanikiwa kupata medali 20 zikiwemo dhahabu nane, fedha moja, na
shaba 11, katika michezo tofauti, kupitia timu za watu wetu wenye ulemavu wa
akili.
Kwenye
michezo ya watu wenye ulemavu wa mguu na mkono mmoja, wizara imelisaidia shirikisho
la mchezo huo, na kushiriki mashindano ya kitaifa yaliyofanyika Arusha.
Lakini
shirikisho la michezo ya viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA), limesaidiwa kuandaa
bonanza kwa ajili ya kuadhimisha siku ya viziwi duniani.
Mwisho
Comments
Post a Comment