Skip to main content

FIDEL CASTRO, WANANCHI WAPIGA MARUFUKU UZURURAJI HOLELA ENEO LA SKULI

 

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

UONGOZI wa skuli ya sekondari ya Fidel Castro, wananchi kijijini hapo, pamoja na uongozi wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake, umekubaliana kupiga marufuku kuanzia sasa, kutoingia kwa mtu yeyote bila ya kazi ya halali, ndani ya eneo la skuli, ili kuepusha athari ambazo zimeanza kujitokeza.

Wakizungumza kwenye kikao cha pamoja, kilichofanyika skulini hapo, walisema tayari athari kama za wizi wa vifaa vya wanafunzi, umeanza kujitokeza, hivyo wamekubaliana kuanzia sasa kupiga marufuku, uingiaji kiholela.

Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Seif Hamad, alisema ameridhishwa na uamuzi uliofikiwa na pande mbili hizo, kwani wamekuwa na hofu kubwa ya kutokezea vitendo vya udhalilishaji hapo baadae.

Alieleza kuwa, uamuzi huo unaweza kusaidia sana kuondosha uingiaji holela ndani ya skuli hiyo, ambao kwa kiasi kikubwa, ulikuwa unaanza kutishia hata mali za skuli.

‘’Mimi nimeridhishwa na uamuzi ambao umefikiwa kati yetu, wazazi na uongozi wa shehia, kwamba sasa tuwazuie watu wote kuingia kiholela eneo la skuli,’’alieleza.



Katika hatua nyingine Mwalimu mkuu huyo, alisema jambo jingine ambalo limeanza kuwa tatizo, ni wafugaji sasa kukaribisha mifugo yao karibu na majengo ya skuli.

‘’Kwa mfano tulikuwa tumekubaliana kwamba, nje ya eneo la skuli wafunge mifugo yao, lakini sasa fursa hiyo inaonekana kutumiwa vibaya, maana mpaka maeneo ambayo wanafunzi wanakaa na kujisomea, wanaishi na mifugo,’’alilamika.

Hata hivyo Mwalimu mkuu huyo, alisema bado hakuna marufuku kwa wanafunzi wa nje ya skuli hiyo, wanaotaka usaidizi wa wenzao wanakaribishwa.

‘’Utaratibu ni ule ule wa zamani, mzazi anafika kwa uongozi wa skuli na anajaza fomu maalum na anakabidhiwa mwanafunzi mwenzake kwa utaratibu na anasaidiwa,’’alieleza.

Mapema sheha wa shehia ya Wawi Sharifa Abdalla Waziri, alisema uamuzi huo wa kupiga marufuku, sio wa waalimu pekee bali ni makubaliano pande zote.

‘’Sisi wananchi tunaoishi pembezoni mwa skuli ya Fidel Castro, uongozi wa shehia na uongozi wa skuli, tumekubaliana hili kwa pamoja na niletu sote,’’alieleza.



Aidha sheha huyo, aliutaka uongozi wa skuli hiyo kuhakikisha unakaa na wananchi wa shehia jirani ya Vitongoji, kwani wapo baadhi ya watoto hupendelea kuingia ndani ya eneo hilo.

‘’Inawezekana sio watoto wa shehia ya Wawi pekee wala wafugaji, lakini hata shehia jirani ya Vitongoji, sasa baada ya kikao hichi, nao muwaite ili kuwapa ushauri,’’alieleza.

Mapema msadizi wa sheha wa kijiji cha Fidel Castro Fatma Jaffari, alisema wazazi na walezi, ndio wenye jukumu kubwa la kuwazuia watoto wao kutoingia kiholela eneo la skuli.

Alieleza kuwa, kwa vile utaratibu upo, ni vyema ukafuatwa ukiwemo kuonana na waalimu kabla ya kuanza kufanya jambo lolote, ili kuepusha uharibifu skulini hapo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Msaidizi wa sheria shehia ya Wawi Fatma Hilali Salim, aliwashauri wazazi na walezi katika eneo hilo, kuwa walinzi wa mwanzo kwa skuli hiyo.

‘’Wananchi wanaoishi hapa Fidel Castro, muwe walinzi wa mwanzo kabla ya watu wengine, kwani uharibifu unapotokezea nyinyi mnaona kwa haraka, kuliko aliyeko nje ya hapa,’’alishauri.



Mwananchi Haji Mohamed Hamad, alisema wamefurahishwa na uongozi wa skuli kuwashirikisha katika kuzuia athari zaidi skulini hapo.

Asha Khamis alisema, jukumu la kuzuia watoto kutoingia kiholela skuli hapo, ni lao kama wazazi na kisha uongozi wa skuli ni kupiga marufuku kwa kuweka mabango.

Wakati huo huo, uongozi wa skuli hiyo umewataka wafanyabiashara wa aina mbali mbali, kwanza kusitisha uuzaji wa bidhaa zao pembezoni mwa skuli hiyo, hadi taarifa nyingine itakapotolewa.

                                                Mwisho



Comments