WANANCHI wa shehia ya Dodo wilaya ya Mkoani
Pemba, wamesema njia moja ya kupunguza matendo ya udhalilishaji ndani ya jamii,
ni wakati sasa kwa sheria kubadilishwa, ili mwanamke naye aliyechangia kutokea
kwa tendo hilo, atiwe hatiani.
Walisema, wapo wanawake wameshasababisha kufungwa kwa
wanaume wengi, nae akiendelea na shughuli zake mtaani, jambo ambalo linaweza
kuwapoteza wanaume hapo baadae.
Wananchi hao, waliyasema hayo leo Juni 24, 2024 Dodo Pujini, wakati wa
mkutano, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa kushirikiana
na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, kwa ufadhili wa ‘UNDP’ kupitia mradi wake
wa upatikanaji haki Zanzibar.
Walisema, bado makosa ya ubakaji yanawaelekea wanaume
pekee, hata kama mwanamke mwenye umri unaopindukia miaka 18, nae alichangia kwa
njia moja ama nyingine.
Haji Shaibu Hamad miaka (70), alisema ubakaji ambao uko wazi ni ule wa mwanamme kumtumia nguvu mwanamke, lakini ule wa kuridhiana ni vyema
sheria ikawaangalia wote.
‘’Mwanamke anatoka Wete zaidi ya kilomita 40 anamfuata
mwanamme Pujini, kisha wanapokosana kibei, huchukuliwa mmoja na mwanamke
kuachwa, hapa hatutofika,’’alifafanua.
Nae Tatu Juma Othman (60), alisema kama wanawake nao
hawakutiwa hatiani kwa ubakaji, makosa hayo yataendelea kutoka siku hadi siku.
‘’Kama ni mtoto wa kike, au mwanamke amebakwa kwa nguvu,
au ameleweshwa ni kesi nyingine, lakini kwa hawa wanaokubaliana, na kisha
mwanamke kugeuza kibao, wanaume wote wataishia kufungwa,’’alilalamika.
Kwa upande wake Sahiya Abdalla Khamis (50), alieleza
kuwa, wapo wanawake wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kujipatia fedha kiholela,
akisingizia kubakwa.
Nae Juma Ali Juma, alisema bado tafsiri ya maana ya
ubakaji, haijaeleweka vyema ndani ya jamii, na ndio maana, walioko chuo cha
mafunzo wengi ni wanaume.
Mwananchi Ambari Khamis Ambari na mwenzake Adam Said
Omar, walisema kama kwenye vituo vya mapunziko vya askari na Jeshi ‘mesi’ havikuwekewa
udhibiti, vinaweza kuchangia kutokea kw amatendo hayo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwanasheria wa serikali
Mohamed Ali Juma, alisema wazo la mwanamke nae kutiwa hatiani, linahitaji
marekebisho ya sheria.
Alieleza kua, njia nyingine ya kutokomeza matendo hayo,
ni wananchi kufika mahkamani na kutoa ushahidi wao.
‘’Hakuna hatia katika kesi yoyote pasi na sisi wananchi
kutofika mahkamani kutoa ushahidi, na zipo kesi kadhaa zimeshafutwa kwa
changamoto hiyo,’’alieleza.
Nae Mwanasheria wa serikali Mussa Ali Khamis, alisema kwa
eneo kubwa kisheria, mwanamme ndio anayeingia kwenye kosa la ubakaji.
‘’Kisheria mwanamme ndie anaebaka, maana hicho cha
kubakia anacho, ingawa mwanamke anaingia, ikiwa amechangia tendo la ubakaji
kutokea, kwa mfano kutoa nyumba yake,’’alifafanua.
Mapema Mkuu wa Divisheni ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Pemba, Bakar Omar Ali alisema, mkutano huo ni kwa ajili ya wananchi, kutoa
maoni yao.
‘’Wananchi leo, tumekuja kukutana na nyinyi, mtueleze ni
kifanyike ili kuondoa matendo ya udhalilishaji, na pale yanapotokezea ni kuyaripoti,’’alifafanua.
Akifungua mkutano huo, Naibu sheha wa Dodo Abdalla Mkubwa
Mohamed, alipongeza hatua ya taasisi hizo, kuichangua shehia yake, kupewa elimu
hiyo.
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana na
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa
ufadhiliwa UNDP inaendelea na mikutano ya wazi kwa wananchi, ili kuwahamasisha
kutoa ushahidi na kuyaripoti matendo ya udhalilishaji.
Tayari wananchi wa shehia Ukutini, Dodo wilaya ya Mkoani wameshafikiwa, na kesho Julai 25, itakuwa ni zamu ya wananchi wa Gando wilaya ya Wete na Micheweni.
Mwisho
Comments
Post a Comment