NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
IDARA ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar, imewataka wanawake wa Junguni wilaya ya Wete, kutoacha kuzisimamia kasi
za udhalilishaji hata kama mtendaji ni muume wake, kwa hofu ya kutishiwa talaka.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 25, 2024 na Afisa
sheria kutoka Idara hiyo Ali Haji Hassan, wakati akizungumza na wananchi wa
shehia ya Junguni wilaya ya Wete, kwenye muendelezo wa mikutano ya wazi, ya kuihamasisha
jamii, kutoa ushahidi na kuziripoti za kesi za udhalilishaji, ulioandaliwa kwa
ushirikiano na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Alisema, kama muume amebainika kwa kosa ubakaji, mwanamke
lazima ashirikiane na vyombo vya sheria na kuondoa hofu ya talaka, ikiwa ni
njia moja wapo ya kutokomeza matendo hayo.
‘’Hakuna hatia pasi na mwananchi kufika mahkamani kutoa
ushahidi, sasa niwaombe wanandoa, wasiogope kuachika na wasimamie haki ya mtoto
mahkamani,’’alishauri.
Katika hatua nyingine, Afisa huyo sheria, alisema bado
jamii haijakuwa tayari katika mapambani hayo, kwani bado zipo familia,
wanazifanyia sulhu kesi hizo.
Katika eneo jingine, alisema rushwa muhali imekuwa
ikitawala ndani ya jamii, hasa ikitokezea anayeshutumiwa kwa ubakaji ni mwalimu
wa madrassa, sheikh wa mtaani au mtu maarufu.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa serikali Shaame Farhan
Khamis, alielezea kusikitishwa na wananchi wanaoiandikia barua Afisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka kutaka kufutisha kesi za udhalilishaji.
Aidha aliwaeleza wananchi hao kuwa, hadi sasa sheria
nambari 6 ya mwaka 2011, inaendelea kumtambua mtoto kuwa, ni mtu yeyote
aliyechini ya umri wa miaka 18.
‘’Hivyo mwenye miaka 15, 16 na hata 17 hata kama
atamfuata mwanamke masafa marefu, likitokezea tendo la kukutana kimwili, huhesabika
ni ubakaji,’’alifafanu.
Kwa upande wake Mwanasheria wa serikali kutoka Afisi hiyo
Rahima Kheir Iddi, alisema jamii ndio pekee, iliyona nafasi kubwa ya kutokomeza
matendo hayo.
Alieleza kuwa, njia moja ni kufika mahakamani kutoa
ushahidi, pili ni kuanzisha ulinzi dhidi ya watoto pamoja na kuwafichua waliotenda
jinai hiyo.
Akifungua mkutano huo, sheha wa Junguni Hamad Yahya
Hussein, alisema fursa hiyo ni vyema wananchi wakaitumia, ili kutoa maoni yao.
Mwananchi Hassan Kombo Khamis, alisema bado adhabu iliyoandikwa
kwenye vitabu vya sheria, ni ndogo wanayopewa washatakiwa.
‘’Adhabu iliyotajwa ni kuanzia miaka 30 hadi chuo cha
mafunzo maisha, lakini bado mahkama wanawafungwa washtakiwa miaka 15 au 20,
jambo linalochangia, kuendelea kwa matendo hayo,’’alifafanua.
Nae Mafunda Hamad Saleh, alieleza kuwa kama jamii haikukubali
kuyarejesha malezi ya pamoja, suala la udhalilishaji linaweza kuchelewa kupungua
ndani ya jamii.
Mzazi Mmaka Hamad Nassor alisema, vyombo vya habari na hasa
mitandao ya kijamii, kama picha chafu hazikudhibitiwa, mmong’onyoko wa maadili
utaendelea.
‘’Jingine linalokwamisha matendo hayo kutopungua, ni
uwepo wa harufu ya rushwa katika vyombo
vya sheria, jambo linalorejesha nyuma, mapambano hayo.
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar kwa kushirikiana
na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ufadhili wa UNDP, imekamilisha mikutano
ya wazi katika shehia za Ukutini, Dodo, Junguni na Micheweni kisiwani Pemba.
Mwisho
Comments
Post a Comment