NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud
Othman, amevishauri vilabu ya mazoezi nchini, kujitengenezea kanuni, zitakazowavutia
watu wingi zaidi kujiunga kwenye mazoezi, ili kuondoa dhama potofu ya mazoezi
ni uhuni.
Alisema, kama kundi kubwa la watu wanadhana kuwa mazoezi ni
uhuni na kuvunja maadili, ni wakati sasa kwa vilabu vya mazoezi na michezo,
kuwa na kanuni zitakazofuta dhana hiyo.
Makamu huyo wa Kwanza, aliyasema hayo leo Julai 28, 2024 uwanja wa michezo
Gombani Chake chake, kwenye bonanza la miaka 10, tokea kuanzishwa kwa ‘Gombani
Fitness Club’ lilioandaliwa kwa pamoja na TAMWA-Zanzibar na Shirika la Bima.
Alieleza kuwa, kwa vile mozoezi ni jambo muhimu kwa kila mmoja,
ni vyema kuwepo na kanuni ndogo ndogo, ambazo zitawavutia wengine, kushiriki
katika kupata kinga ya miili yao.
Alifahamisha kuwa, ni kweli kama kuna viashiria vya uvunjifu
wa maadili, inaweza kuwa sababu kwa baadhi ya watu, kuona sio sehemu salama,
ingawa zikiwepo kanuni zitawavutia wengi.
‘’Kama mlivyosema kuwa, moja ya changamoto zenu ni kuwepo
kwa dhana potofu, kuwa mwanamke anapofanya mazoezi au kushiriki michezo ni uhuni,
sasa ili kuliondoa hili andaeni kanuni zenu,’’alishauri.
Katika eneo jingine, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman
Massoud Othman, aliitaka jamii kurudi kwenye vyakula vya asili, ili
kujipunguzia magonjwa.
Alieleza kuwa, kwa mfumo wa maisha ulivyo sasa, na aina ya
vyakula vilivyopo, ni lazima sasa jamii irudi kwenye vyakula vya asili, ili
kupunguza ukali wa magonjwa.
‘’Wengi wetu tunavyovitambi sugu, mazoezi hatutaki, basi japo
kurudi kwenye vyakula vya asili, ambavyo kwa kiasi kikubwa, havisababisha
magonjwa ya moja kwa moja,’’alishauri.
Akizungumzia faida za mazoezi, alisema ni kupunguza magonjwa
ambayo pamoja na matumizi ya dawa, lakini yanapungua nguvu, kwa kufanya mazoezi.
‘’Faida nyingine ya mazoezi ni kujenga umoja, mshikamano wa
kweli, baina ya mtu na mtu na hata klabu moja na nyingine,’’alifafanua.
Kuhusu miaka 10 ya ‘Gombani Fitness Club’ Makamu huyo wa
Kwanza, aliupongeza uongozi, kwa kuendelea kuwalea wanachama na kufikia malengo
yao.
‘’Hili mlilolianzisha ni jambo muhimu mno, na mimi nitakuwa
balozi nzuri kwa wenzangu, kuwaelekeza namna ya kuwa na vilabu vingi zaidi, vyema
wanachama wengi,’’alifafanua.
Mwenyekiti wa Gombani Fitness Club Hamad Ali Malengo, alimshukuru
Makamu huyo wa Kwanza, kwa kukubali kushirikiana nao, katika sherehe hizo za
miaka 10 ya taasisi yao.
Aidha, alisema wamekuwa wakishirikishwa na kushirikiana kwa
karibu na serikali za mkoa wa wilaya, katika shughuli kadhaa za kitaifa.
Akisoma risala ya kwa niaba ya Shirika la Bima Zanzibar Afisa
Program wa mradi wa michezo kwa maendeleo kutoka Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Hairat Haji, alisema wamekuwa wakiihamasisha
jamii, kuwa michezo ni kwa wote.
Alisema, mradi huo kwa sasa unatekelezwa na Jumuiya ya
wanasheria wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’ Kituo cha mijadiliano kwa vijana ‘CYD’
pamoja na TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili Shirika la Maendeleo la Kimataifa la
Ujerumani ‘GIZ’
Alifafanua kuwa lengo kubwa, ni kuongeza ushiriki wa
wanawake na watoto wa kike, katika mazoezi na michezo, kwani kila mtu, anayo
haki sawa, hasa katika eneo hilo.
‘’Katika kufanikisha mradi huu, sisi TAMWA jukumu letu ni
kuwawezesha waandishi wa habari kimafunzo, na kisha wawe weledi wa kukuza usawa
wa kijinsia na ujumuishi katika michezo, kupitia kazi zao,’’alieleza.
Aidha alisema, tayari waandishi wa habari 30 wa Zanzibar,
wameshawezeshwa namna bora ya kuandika habari na kutengeneza vipindi, vinavyoelezea
fursa sawa ya michezo na eneo la ujumuishi.
Kuhusu changamoto, alisema zilizoibuliwa ni kuinasibisha michezo na mazoezi kwa mtoto wa kike na wanawake, ni uhuni, jambo ambalo sio sahihi.
‘’Jingine lililoibuliwa na waandishi wa habari, ni ukosefu
wa miundombinu rafiki, ughali wa vifaa vya michezo pamoja na dhana ya utamaduni,’’alieleza.
Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa vilabu vya mazoezi Zanzibar ‘ZABESA’
Said Suleiman Said, alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa, moja
wapo ikiwemo ukosefu wa eneo mahasusi la kufanyia mazoezi.
Awali Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali,
alisema Gombani Fitness Club, imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na
serikali.
‘’Inapotokezea shughuli za kitaifa, hushiriki kwenye usafi,
uchangiaji damu, jambo ambalo linatupa moyo kuona wanajali serikali yao bila ya
ubaguzi,’’alisema.
Awali Makamu huyo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud
Othman, aliungana na vilabu zaidi ya vitano vya mazoezi kutoka Unguja, Tanga na
wenyeji Pemba, katika matembezi ya kilomita tatu, yalioanzia mjini Chake chake
hadi uwanja Gombani.
Mwisho
Comments
Post a Comment