BARAZA la watoto la shehia ya Wawi wilaya ya Chake
chake, limesema bado hawaridhishwi na hukumu nyepesi zinatolewa mahakamani, kwa
washtakiwa wanaowabaka watoto na wanawake.
Walisema, bado hukumu zinazotolewa na mahakma maalum za kupambana
na udhalilishaji, zinawafaidisha wabakaji, jambo ambalo, linatishia kuendelea
kwa matendo hayo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shehiani hapo,
walisema, Baraza la Wawakilishi mwaka 2018, lilipitisha sheria kali kwa
watakaotiwa hatiani kwa udhalilishaji, ingawa bado mahakimu hawaitumii
ipasavyo.
Walisema, wamesomeshwa kuwa, mahkama ikimtia hatiani
mshitakiwa kwa makosa ya ukatili na udhalilishaji, adhabu yake ni kuanzia
kifungo kisichopungua miaka 30 au maisha, ingawa hakuna aliyetekelezewa adhabu
hiyo.
Mjumbe wa baraza hilo Aisha Mohamed Juma, aliema anashangaa
kuona washtakiwa wanafungwa miaka kati ya 10 au 15 tu, jambo ambalo anashindwa
kuwaelewa mahakimu.
Alieleza kuwa, hajaona wapi mahakimu na majaji hao, wanapita
na kutafsiri na kuacha kuwafunga washtakiwa kifungo cha kuanzia miaka 30 au
maisha, na badala yake hutoa raia nyingine.
‘’Kama sheria imeshapitishwa kwamba, atakaetiwa hatiani afungwe
kuanzia miaka 30, nini kinawatia hofu mahakimu na majaji wetu,’’alihoji.
Nae mjumbe wa baraza hilo Omar Haji Omar alisema, serikali kwa
upande wake, imeshaongeza adhabu kwa wabakaji, ili kukomesha vitendo hivyo,
ingawa bado kuna ukakasi wa sheria kutumika.
‘’Kama Majaji wanatafsiri nyingine ya sheria ya Adhabu nambari
6 ya mwaka 2018 kwenye vifungu vyake ya 108 na 109 watueleze, ili tuilalamikie tena
serikali, kinyume chake watekeleza kama ilivyo,’’alifafanua.
Mratibu wa wanawake
na watoto ambae ni Mratibu wa baraza la watoto shehia ya Wawi Fatama Kassim
Mohamed, alisema watoto, wamekuwa wakihoji katika mkutano mbali mbali, juu ya adhabu
nyepesi zinazotolewa mahakamani.
‘’Tulipiga kelele kwa
muda mrefu, juu ya marekebisho ya sheria, kwamba ziongezewe makali, lakini sasa
zimeshaongezewa, hatuoni matunda yake,’’alilalamika.
Nae Mwenyekiti wa baraza
hilo Abuu-bakar Massoud Juma, alisema kama sheria haikutumika kama ilivyo, watoto
wataendelea kudhalilishwa hapa Zanzibar.
‘’Tulitarajia kuwa,
kuanzia mwaka 2018 baada ya sheria mpya kupita, wabakaji wataingia woga, kwani
sheria hiyo ni kali, lakini cha kushangaaza wanafungwa miaka 10 au 15 na sio 30
kama sheria ilivyo.
Msaidizi wa sheria wa
shehiya ya Wawi Fatma Hilali Salim, alisema kua, wimbi la ubakaji, lilionekana
kubwa hapo zamani na kukaandaliwa mipango kadhaa, ikiwemo kurekebishwa sheria, ili
kupunguza matendo hayo.
‘’Ni kweli huskii
kutokana mahkamani kuwa, kuna mshtakiwa amefungwa maisha au kifungo kisichopungua
miaka 30, kama sheria ilivyo, hili ni tatizo upande mmoja,’’alieleza.
Akizungumza kwenye
moja ya makongamano ya kupinga ukatili na udhalilishaji, Hakimu wa mahakma maalum
ya kupinga udhalilishaji Mkoa wa kaskazini Pemba, Muumini Ali Juma, alikiri
kuwepo wa tasfsiri tofauti.
Alisema, mahakimu wamepewa
nguvu kisheria, baada ya kufungwa kwa ushahidi na kumalizika utetezi, kuangalia
ukubwa wa adhabu, kwa mashtakiwa.
Alifahamisha kuwa,
sheria huja kama muongozo wa kutoa adhabu na inaweza isilingane baina ya mshatikiwa
mmoja na mwingine, hata kama kosa ni la aina moja.
‘’Mahakimu na Majaji
ipo sheria yetu inayotuongoza, ambayo imetuwekea utaratibu wa kuendesha
mashauri hadi utoaji wa adhabu, katika mahakma husika,’’alifafanua.
Mkurugenzi Idara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Siti Abassa Ali, amewataka
watoto kuendelea kuwaibua wanaotaka kuwadhilishaji, ili sheria ichukue mkondo
wake.
Mratibu wa Chama
cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya
Mussa Said, alisema adhabu ndogo zinazotolewa, ni chanzo cha kuongezeka kwa
matendo hayo.
Juni 13, mwaka jana
mahkama ya Mkoa Wete ilimuhukumu mshitakiwa Ali Sharif Ali, wa Pandani,
kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 20, baada ya kupatikana na hatia
ya kumlawiti mtoto mwenye miaka 15.
Aidha Disemba mwaka
2022, mshatakiwa Said Abdalla Issa, wa Chanjamjawiri na Kengeja,
alifungwa miaka saba, baada ya, kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kulea
mwenye miaka 14.
Mahakama maalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji
Mkoa wa kusini Pemba, Disemba 2m mwaka 2022, limswekwa chuo cha mafunzo kwa
muda wa miaka 10, mshitakiwa Khamis Juma Chumu ‘soda’ (76) wa Mtoni
Chake Chake, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 13.
MWISHO
Comments
Post a Comment