WAVUVI wa bandari ya Tanda Tumbi Shehia ya Mjanaza Wilaya ya
Micheweni Pemba, wametakiwa kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka ya Hali
ya Hewa, ili kuweza kujikinga na matatizo yanayoweza kutokea wakati wakiwa
katika shughuli zao za uvuvi.
Hayo yalielezwa na Mkaguzi wa Polisi ambae pia ni Polisi shehia
ya shehia ya Mjanaza Khalfan Ali Ussi, wakati akikabidhi simu kwa wavuvi hao,
ikiwa ni ahadi iliyoitoa kwao hivi karibuni.
Alisema, kwa vile wao ni wavuvu anamatumaini makubwa kuwa, simu hizo lengo lake ni kuwasaidia katika
shughuli zao hizo, pindi wanapopatwa na majanga mbali mbali.
Alifahamisha kuwa, lengo la kutoa simu hizo ni kutokana na maafa
mbali mbali, ambayo yanawapata wavuvi wakiwa katika shughuli zao, na kukosa
chombo cha mawasiliano.
"Leo (jana), nimekuja kwa ajili ya kutimiza ahadi yangu, niliyoiweka
kwenu kuwapatia simu ambayo itaweza kuwasaidia, pindi mnapotokezea kadhia
yeyote ile wakati mkiwa katika shughuli zenu za uvuvi,’’alifafanua.
"Lakini pia niwaombe wavuvi ambao mnafanya shughuli zenu
hapa, muhakikishe mnajisajili katika simu hii, ili pale shida inapowatokezea
huko baharini, muweze kutoa taarifa kwa haraka,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkaguzi huyo wa Polisi, aliwataka wavuvi
hao, kufuata sheria zilizopo, pamoja na kutunza mazingira ya bahari, ili waweze
kunufaika wao pamoja na vizazi vyao.
"Tujitahidini kutunza rasilimali zilizomo baharini, kwa
kufuata sheria na taratibu zote za uvuvi, bahari ni hazina yetu, wenyewe,’’alishauri.
Mapema Mkaguzi huyo aliwataka wavuvi hao kujikusanya pamoja
katika vikundi vya ushirika, ili kupata urahisi wa kutafuta njia ya kupata boti
ambazo zinatolewa na serikalini kwa njia mkopo.
Nao wavuvi hao walimpongeza Mkaguzi huyo kwa kuweza kuwapatia
simu hiyo, ambayo itakayoweza kuwasaidia katika shughuli zao hizo.
Mvuvi Othman Hamad Othman, alimuomba Mkaguzi huyo kupatiwa boti
la uokozi katika bandarini hapo, ili iweze kutoa msaada pale linapotokezea
tatizo
Othman alifahamisha kuwa, boti ipo lakini iko mbali na wao,
hivyo linapotokezea tatizo ni vigumu kufika kwa wakati muafaka.
"Kikweli boti ipo, ingawa shughuli zake ni Msuka, sasa
linapotokezea tatizo kwa huku kwetu ni shida sana, hivyo tunaomba boti moja la
kisasa ambalo litaweza kutusaidia tunapopatwa na shida kubwa baharini,"
alishauri.
Nae mvuvi Kassim Mohamed, alimuomba Mkaguzo huyo wa Polisi,
kuangalia uwezekano wa kuzungumza na mamlaka husika, kwa ajili ya kupatia
huduma ya maji na salama, bandarini hapo.
MWISHO |
Comments
Post a Comment