NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAUMINI wa dini ya
kiislamu kisiwani Pemba, wametakiwa kuzitumia kimipango, siku zilizobakia za
mwezi mtukufu wa Ramadhan, ili kujikurubisha kwa Muumba na kupata fadhila zake.
Hayo yalielezwa na Msaidizi wa
Katibu wa ofisi ya Mufti Zanzibar, ofisi ya Pemba Sheikh Said Ahmad Mohamed,
wakati alipokuwa akitoa shukran kwa waumini, walioshiriki sawala wa Ijumaa, na
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, Machomanne Chake chake Pemba.
Alisema, sio sahihi kuwa mwezi mtukufu
wa Ramadhan umekwisha, bali siku zilizobakia zinaweza kumkomboa muumini na
kupata malipo makubwa, iwapo atajipangia ratiba nzuri.
Alieleza kuwa, kwa fadhali za mwezi
huu, muumini hawezi kupoteza jambo hata kwa siku moja, ikiwa ataamua
kujikurubisha kwa vitendo Muumba, kama wanavyofanya baadhi yao.
Sheikh Said alieleza kuwa, siku
moja katika mwezi mtukufu wa Ramadhan inathamani zaidi ya mara moja, kuliko
siku nyingine, hivyo sio sahihi kuwa Ramadhan imekwisha na hakuna muda wa
kufanya ibada.
‘’Kama Khatib wa swala ya Ijumaa
alivyosema, kwenye hutuba zake, kuwa muda wa kufanya ibada bado upo ndani ya
mwezi huu, na wala sio sahihi kuwa siku za Ramadhan zimekwisha,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Msaidizi huyo
wa Katib wa ofisi ya Mufti Pemba sheikh Said Ahmad Mohamed, aliwataka waumini
kuendelea kuombeana mema na kusaidiana miongoni mwao.
‘’Mwezi huu mtukufu hutujia sisi
waumini wa dini ya kiislam mara moja kila mwaka, hivyo inatupasa kuongeza bidii
ya kuombeana na kusaidiana kwa vitendo, ili kufikia malengo yetu,’’alifafanua.
Alieleza kuwa, yapo malipo makubwa
kwa kila muuimini anayefanya mema, ambayo Muumba ameyahidi kwa waja wake, fursa
ambayo huja mara moja kila mwaka.
‘’Mwezi mtukufu wa Ramadhan ni
hidaya kwa waumini wa dini ya kiislamu, kwani wema unaoutenda katika miezi
mingine, malipo yake huwa ya kawaida, ingawa katika mwezi huu huongezeka,’’alieleza.
Baadhi ya waumini wa dini ya
kiislamu waliohidhuria swala hiyo ya Ijumaa, waliwataka waumini wenzao,
kuongeza kasi ya utendaji wa ibada na kusahau michezo isiyo na tija.
Mohamed Khamis Juma, alisema kwa siku
zilizobakia sio za mtu kufanya vitendo vya anasa, kama kushirki michezo ya
karata, bao na kuangalia michezo ya isiyo natija ya tv.
Omar Haji Mohamed, alisema bado
kuna kasi ndogo ya waumini wa dini ya kiislamu, wanaoshiriki katika vikao
vitakatifu vikiwemo vya baada ya swala ya Al-fajiri, Al-aasiri na wanaojitokeza
ni wale wenye umri mkubwa pekee.
‘’Kwenye madarsa ya misikitini iwe ni
baada ya swala za Alf-ajiri, Adhuhuri au ishaa wanaoonekana kwa wingi ni wazee,
lakini vijana wamekuwa wakifanya shughuli nyingine mabadala,’’alieleza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikuwa kisiwani Pemba kwa ziara ya
siku mbili ya futurisho, ambapo tayari wananchi wa mikoa miwili ya kaskazini na
kusini, wameshajumuika nae.
Mwisho
Comments
Post a Comment