NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
TUME ya Kurekebisha
sheria Zanzibar, imesema itaangalia kwa kina, juu ya mifumo ya sheria, ili
isiwaweke nje ya utaratibu watu wenye ulemavu, katika mapambano dhidi ya
udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu
wa Tume hiyo, Mussa Kombo, wakati akikikfungua kikao kazi, cha kupokea maoni ya
wadau wa haki jinai, kuelekea marekebisho ya Sheria ya Adhabu nambari nambari 6
ya mwaka 2018 na ile ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai nambari 7 ya mwaka 2018,
kilichofanyika ukumbi wa wizara ya Fedha Gombani.
Alisema, ni kweli watu wenye
ulemavu wanaonekana kuwekwa nyuma kwenye mifumo ya haki jinai, kuanzia kuchukuliwa
maelezo vituo vya Polisi, ushahidi mahakamani, kujitetea jambo ambalo, linaweza
kuwa chanzo cha kuwakosesha haki zao.
Alieleza kuwa, kupitia marekebisho
hayo na kwa kuzingatia maoni yaliotolewa, watahakikisha kundi hilo sasa
linawekewa kifungu maalum ndani ya sheria hizo, ili iwe sababu ya kuunga mkono
mapambano hayo.
‘’Ni kweli kama kuwepo mkalimani wa
lugha ya alama katika mahakama zetu halipo moja kwa moja kisheria, ni changamoto,
ambayo inahitajika kuangaliwa upya,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo
wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, alisema wakati umefika sasa, kwa
taasisi zinazoshughulikia kesi za udhalilishaji kujenga umoja wa kikazi, ili
kukomesha matendo hayo.
‘’Kwa mfano, ikiwa hakimu mmoja aliyemtia
hatiani mshitakiwa wa kosa la ubakaji, anamfunga miaka 20 na hakim mwingine kwa
kosa kama hilo anamfunga miaka 15, hapa ipo shida,’’alifafanua.
Aidha Katib huyo, aliitaka jamii
kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali, katika kupambana na kudhibiti
matendo ya ukatili na udhalilishaji.
‘’Moja ya wajibu wa jamii, kwanza
ni kufika Polisi na mahakamani kutoa ushahidi kwa kile walichokiona, kusikia,
kushuhudia katika mtiririko wa kosa ambalo, limeshafikishwa mahakamani,’’alieleza.
Baadhi ya washiriki hao, wakitoa
maoni yao kwenye kikao hicho kazi, walisema moja ya eneo ambalo linatakiwa
kutiliwa mkazo, ni usimamizi wa sheria, ambazo zimekubaliwa kutumika.
Mratib wa Chama cha Waandishi wa
habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ Ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema ni mapema
mno, kuurejesha umri wa mtoto, kutoka miaka 17 ya sasa na kuweka miaka15.
Nae mjumbe wa Jumuiya ya wanawake
wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Hidaya Mjaka Ali, alisema lazima mifumo ya
haki jinai, iwe jumuishi kwa makundi kadhaa ya watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Maryam Mohamed Muhene,
alisema ni vyema sheria ikaweka kifungu kinachozuia mtu kumtumia mtoto kama mfanyakazi
wa ndani.
Nae mshiriki Rashid Abdalla
Mshamata, alisema bado elimu inahitajika kwa jamii, juu ya athari ya kuendelea
kufanya matendo ya ukatili na udhalilishaji.
Hata hivyo mwakilishi wa Dawati la
jinsia na watoto la Wete Said Mohamed Ali, alisema uwepo wa mahakama maalum ya
kupambana na udhalilishaji, imesaidia kupunguza, kwa matendo hayo ndani ya
jamii.
‘’Lakini changamoto ambayo
inajitokeza na huenda ikaathiri kama haikufanyiwa kazi, ni baadhi ya mahakimu
kuchelewa kusoma hukumu na wakati mwingine hadi kufikia mieizi miwili,’’alieleza.
Nae Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi
wa habari Pemba ‘PPC’ Bakar Mussa Juma, alisema yapo mazingira ya mtoto anayafanya
na kisha kubakwa, ingawa wazazi na walezi huwa chanzo.
Kikao hicho kazi, ni muendelezo wa
mikutano inayofanywa na Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, ya kukusanya maoni
ya kiutafiti juu ya sheria za Adhabu na ile ya Mwenendo wa Makosa ya jinai,
zote za mwaka 2018.
Tume ya Kurekebisha sheria,
imeanzishwa kwa sheria ya Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, nambariu 16 ya
mwaka 1986, na kupewa jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote za Zanzibar au
eneo fulani la sheria husika.
Mwisho
Comments
Post a Comment