IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAZAZI na walezi wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete Pemba wameshauriwa kujenga tabia ya kuhoji vyanzo vya vipato vya watoto wao, ili kuiepusha jamii kuingia katika vitendo vya kihalifu.
Akizungumza na Kamati ya wazee wa kijiji cha Kwamwewe wakati wa muendelezo wa kutoa elimu ya kudhibiti vitendo vya kihalifu katika jamii, Mkaguzi wa shehia hiyo Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi alisema, kuna baadhi ya wazazi hawawezi kuwauliza kitu watoto wao, jambo ambalo sio jema.
Alisema kuwa, ni vyema kila mzazi kujua tabia ya mtoto wake na kuhoji vitu au vipato walivyonavyo vinatoka kwenye vyanzo gani, hiyo itasaidia kuondoa vitendo vya uhalifu katika jamii kwani kila ambae anajihusisha na tabia mbaya ataweza kuziacha kwa haraka.
"Tusiwagope watoto wetu, kujua vyanzo vyao vya mapato itatusaidia kujua wanafanya kazi gani na pia wenyewe watatafuta kazi za halali kwa sababu watajua tu kama wataulizwa na wazazi wao, hivyo naamini vitendo hivyo vitakuwa havipo," alisema.
Aidha Mkaguzi huyo aliwataka wazazi hao kuacha muhali na mapenzi yaliyopitiliza kwa watoto wao, kwani linaweza kurudisha nyuma juhudi za kuiweka sawa jamii yao dhidi ya uhalifu.
Alisema kuwa, lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hali ya changamoto za uhalifu kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita na kuweza kupanga mikakatiipya ya kudhibiti kwa vipindi vijavyo, ili kuona kwamba vijiji vyote vinakuwa salama.
Nae sheha wa shehia hiyo Khamis Rashid Ali alieleza kuwa, ni vyema kwa wazazi hao kuendelea kukaza kamba katika kudhibiti tabia za watoto wao, ili wawe na maadili mema.
Mapema wazazi hao walisema, vikao wanavyoweka kila baada ya miezi mitatu vinawasaidia kuimarisha shehia yao kutokana na mikakati mbali mbali wanayoiweka, ambapo sasa wanaendelea kufanya shughuli zao kwa kuzingatia maadili.
"Tumefanikiwa kudhibiti changamoto mbali mbali zilizokuwa zikiwakabili na vijana wengi wamehamasika kujiunga kwenye kikundi cha ulinzi shirikishi, haya ni mafanikio makubwa kwetu," walisema wazee hao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment