IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@
WANANCHI wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mbinu zinazotumiwa na wahalifu, ili vijiji vyao viwe katika hali ya salama.
Akizungumza wakati wa kampeni yake ya kupita nyumba kwa nyumba juu ya kutoa elimu ya kudhibiti uhalifu katika kijiji cha Mwembe Butu, Mkaguzi wa shehia hiyo Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi alisema, kila siku wahalifu huandaa mbinu mpya, hivyo wawe makini.
Alisema kuwa, ni vyema jamii kuwapa ushirikiano kikosi cha ulinzi shirikishi ili wajue mbinu zinazotumiwa na wahalifu wanaotekeleza uhalifu wao na kuweza kuwadhibiti.
"Kampeni hii ni ya Familia yangu Haina uhalifu, hivyo tunataka tuhakikishe jamii inaishi bila ya kuwepo uhalifu na ndio maana tunachukua juhudi ya kutoa elimu nyumba kwa nyumba," alisema Mkaguzi huyo.
Aidha Mkaguzi huyo aliwataka wanafamilia kuendelea kusimamia maadili mema ya watoto wao ili kujenga familia yenye heshima, huku akisisitiza kuwa suala la malezi sio la mtu mmoja bali ni la jamii nzima, kwani kila mmoja ni mlinzi kwa mwenzake.
"Turudishe malezi ya pamoja yaliyokuwa wakifanya wazee wetu wa zamani, hii itatusaidia vijana wetu wawe na heshima na kuepuka kujiingiza katika makundi hatarishi, alisema.
Mwananchi Said Hamad Said alisema kuwa, kwa ushirikiano wao wameweza kudhibiti baadhi ya mambo ya kihalifu yaliyokuwa yakitokea katika vijiji vyao na kuahidi kufanyia kazi elimu inayotolewa ili uhalifu upotee.
"Tulipokuwa hatujapatiwa elimu tulikuwa tunakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo tulishindwa kuzikabili, lakini kwa sasa tunashirikiana pamoja kudhibiti, tunashkuru tumefikia hatua kubwa," alisema mwananchi huyo.
Kampeni hiyo ya kutoa elimu ya kudhibiti uhalifu inasaidia jamii kuibua changamoto mbali mbali zinazowakabili na kushauriwa njia ya kuzitatua kwa kushirikiana na mamlaka husika.
MWISHO.
Comments
Post a Comment