NA ZUHURA
JUMA, PEMBA::::
WIZARA ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imewajengea uwezo washauri wa masomo, ili
kuboresha zaidi katika kufanya ufuatiliaji, ushauri katika ufundishaji pamoja
na upimaji kwa wanafunzi.
Akifungua mkutano kwa washauri hao, leo August 8, 2022 Kaimu Mratibu Idara ya Mafunzo ya Ualimu WEMA Pemba, Mzee Ali
Abdalla alisema mafunzo hayo yatasaidia kuboresha kiwango cha ufaulu kwa
wananfunzi.
Alisema kuwa, katika ufuatiliaji imeonekana kuwa kuna
changamoto kwenyea kutunga maswali yenye umahiri katika pimaji na mitihani,
hivyo Wizara imeona kwamba ipo haja ya kuliomba Baraza la Mitihani Tanzania
kuwapa mafunzo washauri wa masomo, ili na wao waweze kuwajengea uwezo walimu.
‘’Kutokana na changamoto hiyo, tumeona kwamba tutumie fursa
hii, kwani Baraza la mitihali limekuwa likitoa mafunzo haya kwa maafisa
mitihani katika halmashauri na skuli mbali mbali’’, alisema Kaimu huyo.
Alieleza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kwamba baada ya
mafunzo wawe na uwezo wa upimaji unaozingatia umahiri, utungaji maswali,
maswali ya kuchagua, kuoanisha, ya majibu mafupi, ya kweli au si kweli, insha,
muundo wa mitihani na jeduweli la mtihani.
Alieleza kuwa, wanatumai kwamba kila mmoja atashiriki
kikamilifu katika mafunzo hayo na kupata umahiri uliokusudiwa, ili kuweza
kuutumia katika kazi za kila siku zinazohusu maswala ya upimaji na utahini.
‘’Tunategemea kuwa mtatumia ujuzi na maarifa mtakayoyapata,
ili kwenda kuwajengea uwezo walimu na kufanya ufuatiliaji ili kuona namna
wanavyoandaa mitihani ya ndani kama inavyotakiwa’’, alieleza.
Kwa upande wake muwezeshaji kutoka NECTA Beata Xavery alisema
kuwa, suala la elimu katika Taifa ni la msingi sana kwa sababu fani zote
zinatoka katika elimu, hivyo jukumu la kusimamia utoaji wa elimu na upimaji ni
suala nyeti katika Taifa lolote lililopiga hatua.
‘’Nimeona fahari kutokana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia
viongozi wa Wizara hii kuona umuhimu wa mafunzo haya ya upimaji unaozingatia
umahiri kwa lengo la kuimarisha elimu katika skuli kwa ajili ya watoto wetu’’,
alieleza.
Alifahamisha kuwa, upimaji bora katika skuli ndio unachochea
ufundishaji, hivyo aliwaomba kuitumia fursa hiyo watakayoipata kwenye mafunzo
hayo kwa ajili ya kujenga Taifa bora la baadae.
Mkuu wa Seksheni ya Mafunzo ya ualimu Kazini Fatma Ali Salim alisema
kuwa, mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwawezesha washauri wao wa masomo katika
vituo vya walimu (TC), ili kuweza kwenda sambamba na mtaala mpya wa CBC ambayo
itawafanya walimu kuwa na umahiri mkubwa katika kufundisha na kuwatathmini
wanafunzi.
‘’Baada ya mafunzo haya tunatarajia kwamba washauri wetu wa
masomo watakuwa wanajengeka kiuwezo na kiumahiri zaidi kuwapitia walimu
kuwafundisha namna bora ya utungaji mitihani na namna gani wataweza kuwapima
wanafunzi kwa hatua tofauti’’, alisema.
Nae Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Idara ya Mafunzo ya Ualimu
Pemba (DTA) Khamis Adam Suleiman alieleza kuwa, mafunzo hayo yataongeza ufanisi
kwa walimu ambao utafanikisha kuwaboresha wanafunzi na kufaulu vizuri katika
mitihani yao kwa kiwango cha juu.
Mafunzo hayo ya siku tano kuhusu upimaji unaozingatia umahiri,
yamewashirikisha washauri wa masomo na maafisa kutoka Idara ya Elimu Pemba.
MWISHO.
Comments
Post a Comment