NA HAJI NASSOR, PEMBA::::
MAPUNGUFU yaliyopo katika sheria
mbali mbali Zanzibar, zimetajwa kuwa zinachangia kutokuwepo kwa uwiano wa usawa
wa kijinsia, kati ya wanawake na wanaume katika ngazi mbali mbali za uongozi.
Mapungufu ya sheria hizo yameibuliwa na wanajamii kufuatia
mikutano 41 iliyofanyika katika shehia 44 kisiwani Pemba, iliyoandaliwa na
wahamasishaji jamii kwa kushirikiana na asasi za kiraia kisiwani hapa,
juu ya ushiriki wa wanawake katika kushika nafasi za uongozi na
demokrasi.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya mapungufu
yaliyobainika kwenye sheria kukwaza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za
uongozi, Mkurugenzi wa Jumuiya ya utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO)
Hafidh Abdi August 8, mwaka 2022, alisema miongoni mwa Asasi zilizoshirikiana
kuchambua mapungufu hayo ni pamoja na taasisi ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE),
Nihurumie Foundation, KOK Foundation, PRADO, PACSO, Jumuiya ya Wanawake wa
Kiislamu, pamoja na Kituo cha huduma za Sheria Zanzibar ZLSC kisiwani Pemba.
Alisema hadi sasa nafasi za wanawake ni ndogo kwenye uongozi, na
dhamira ni kufikia usawa wa 50 kwa 50 kwa wanawake na wanaume ili usawa ufikiwe,
inaonekana kuzorota.
“Katika Wawakilishi wa majimbo 50 wanawake ni wanane
(8) tu sawa na asilimia 16, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kutoka
Zanzibar kwenye majimbo 50 wanawake ni wannne tu (4) sawa na asilimia
nane (8), Mawaziri ni sita sawa na asilimia 33 na Makatibu wa kuu ni saba sawa
na asilimia 39.
Kwa upande wa Wakuu wa Mikoa mwanamke ni mmoja tu sawa na
asilimia 20, Wakuu wa Wilaya ni wanne sawa na asilimia 36 na Masheha wanawake
ni 68 sawa na asilimia 17 kwa masheha wote ambao ni 389,” alisema.
Alitaja miongoni mwa sheria zilizoonekana kuwa na mapungufu ni
pamoja na Sheria ya Uchaguzi Nambari 4 ya 2018 ambapo licha ya
kwamba Sheria hiyo inasimamia na kutoa muongozo mzuri wa jinsi ya kupatikana
kwa wagombea na viongozi wa nchi, lakini bado ipo kimya katika kueleza
utaratibu wa kupatikana kwa wagombea katika hatua za awali kupitia vyama vyao
hasa ikizingatiwa kila chama kuwa na utaratibu wake wa upatikanaji wa
wagombea.
Alisema “kutokana na mapungufu katika sharia hiyo, hivyo ni
vyema Sheria ikaweka utaratibu rasmi wa kulazimisha upatikanaji wa wagombea wa
kila chama kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika kila nafasi.”
Pia Sheria ya Utumishi wa Umma
Na. /2011 ambayo inayosimamia haki na wajibu wa watumishi wa Umma katika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo kifungu cha 18 cha kimeanzisha
Kamisheni ya utumishi wa Umma itayoongozwa na Mwenyekiti atakayechaguliwa na
Rais pamoja na wajumbe wengine sita watakaochaguliwa na Rais kwa mapendekezo ya
kila wajumbe wawili kutoka kwa Waziri husika, Spika wa Baraza la Wawakilishi na
Jaji Mkuu, kufanya jumla ya watu 7.
“Lakini kifungu hiki hakikuweka uwiyano wa kijinsia, jambo
ambalo ni changamoto inayoweza kusababisha wanaume watupu wakaunda tume hiyo,”
aliongeza mkurugenzi huyo.
Sheria nyingine ambazo zimebainika kukwaza uwiano wa ushiriki wa
wanawake katika nafasi za uongozi ni Sheria ya Watumishi wa Umma
Kushiriki Katika Siasa Sheria Na. 3 ya mwaka 2003, Sheria ya Elimu
ya mwaka 1982, Sheria ya Mahakama ya Kadhi Namba 9/2017, Pamoja
na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama, Na. 11/2018.
Katika hatua nyingine alibainisha kuwa mkataba wa Kimataifa wa
kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) wa mwaka 1979
ambapo unazitaka nchi zote wanachama ambazo zimeridhia mkataba huo ikiwemo
Tanzania, kutekeleza wajibu mahsusi katika kuhakikisha wanawake wanapata haki
zote za binadamu kwa usawa, kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake bila
ya kujali hadhi yao kindoa.
Alifahamisha kuwa “sambamba na hilo pia mkataba huo unasisitiza
upatikanaji wa haki za msingi za binadamu kwa usawa katika nyanja za kisiasa,
kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiraia na nyinginezo, pamoja na kuweka usawa
kati ya wanawake na wanaume katika mfumo wake wa kisheria na kitaasisi.”
Aidha kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 11(1)
kinaeleza kwamba binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, kifungu cha
12 kinazungumzia suala la haki ya usawa mbele ya sheria kuwa watu wote watakua
sawa mbele ya sheria na wanazo haki sawa mbele ya sheria bila kubagua jinsi,
dini, rangi na asili ya mtu.
Licha ya changamoto mbalimbali zilizoko katika sheria hizo juu
ya nafasi ya mwanamke, ziko sheria ambazo zimetambua nafasi ya mwanamke katika
mambo mbali mbali kama vile Sheria ya Mahakama ya Kadhi Namba 9/2017 Kifungu
cha 5(1)(f) ambacho kimewapa nafasi wanawake katika kupeleka malalamiko yao juu
ya ugawaji wa mali.
“Hii ingesaidia kuondosha uonevu wa muda mrefu na umasikini kwa
wanawake, ambao mara nyingi huachwa na kunyang’anywa kila kitu, na hivyo inamlazimu
kuanza upya maisha pamoja na nguvu nyingi alizotupa katika kutengeneza utajiri
wa familia,’’alieleza.
Hata hivyo, alisema tunasikitika kuwa manufaa haya hayapati
mwanamke kwani bado utekelezaji wake unafuata matakwa ya kadhi muhusika kwa
vile haijaelezwa bayana kwenye sheria kuwa mchango na siyo lazima wa kutoa pesa
na kuwa na risiti lakini hata ule wa hali na usio wa pesa ukiwemo wa
kushughulikia nyumba, watoto, baba, wazee na wagonjwa wakati mwenza yuko
kazini.”
Pia Sheria ya Ajira namba 11/2005 imetoa ulinzi mzuri
wa wanawake juu ya masuala mbali mbali ya utumishi wa umma kifungu
cha 10 (2) kinaeleza kwamba muajiri analazimika kuchukuwa hatua ya
kutoa fursa sawa katika sehemu ya kazi na kuondoa ubaguzi katika sera yake na
utendaji wake, kuthibitisha kuwepo kwa malipo sawa ya mishahara kwa mwanamke na
mwanamme kwa kazi ya aina moja,
“Suala jengine lililokatazwa na kukemewa katika Kifungu
cha 11 cha sheria hii ni unyanyaswaji wa kijinsia, vitendo vya
kumtaka muajiriwa wa kike kimapenzi, matumizi ya vitisho na lugha inayoashiria
mapenzi (ngono).
Aliongeza, “Sababu moja ya waajiri wengi kukataa kuwaajiri
wafanyakazi wanawake ni kuwa muda mwingi watakuwa hawapo kazini kutokana na
kujifungua. Suala ambalo limekatazwa moja kwa moja na Sheria hii. Katika
kuhakikisha ya kwamba mwanamke anapata nafasi nzuri ya mapumziko na kulea mtoto
wake miezi 3 yenye malipo na akijifunguwa mapacha
atapata likizo ya siku mia moja.”
“Aidha ni marufuku kumuajiri mwanamke katika sehemu ambazo
zinahusika na kemikali za sumu ambazo zitahatarisha uzazi au mimba ya
mfanyakazi huyo kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 84 (4) na
Kifungu cha 85 (1)kinkataza kumpangia kazi mfanyakazi mwanamke
wakati wa usiku katika shughuli zozote za viwanda.”
Aidha Sheria ya
Elimu namba 6/1982 katika kifungu cha 19 inaeleza
“Itakuwa ni lazima kwa kila mtoto aliyefikia umri
wa miaka saba lakini hajafika miaka kumi na tatu kuandikishwa Elimu za msingi”
Alibainisha, “kifungu hiki kinamaanisha kwamba haki ya elimu ni
haki ya jamii nzima bila kujali tofauti ya kijinsia, nah ii inamlinda mtoto wa
kike pia kwani kuna baadhi ya wanajamii wanakataa kuwapeleka watoto wa kike
skuli kupata elimu ambayo itamjenga yeye kuwa kiongozi bora hapo baadae.”
Sheria ya kuwalinda wari na watoto wa mzazi mmoja namba 4/2005
katika Kifungu cha 5 (1) kinaeleza kuwa mwari yeyote, mtoto wa
kike, au mwanamke ambaye hajaolewa akipata ujauzito au akijifungua nje ya
ndoa anaweza kufungua kesi ya madai katika Mahakama ya Wilaya kudai
matunzo ya mtoto kutoka kwa mtu aliyedhaniwa kuwa ni baba wa mtoto au
aliyemsababishia ujauzito, kabla ya kujifungua au wakati wowote kabla ya mtoto
hajatimiza umri wa miaka kumi na nane (18) au kabla ya mtoto kuweza kujitegemea
mwenyewe. Kifungu hichi kinawasaidia wanawake wale ambao walipata ujauzito bila
ya ridhaa yao kama vile kubakwa kuweza kudai haki hizo za mtoto Mahakamani.
“Pia tukiingalia Sheria ya Adhabu namba 6/2018 hii
inatoa ulinzi kwa wanawake au watoto wa kike juu ya vitendo vya ubakaji dhidi
yao ambapo kifungu cha 108 kimeonesha mazingira hayo na
kifungu cha 109 kimetoa adhabu kwa yoyote atakayefanya kitendo hicho kutumikia
kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka thelathini.
Pia sheria imetoa adhabu
kwa kosa la kumtorosha mwanamke au mtoto wa kike ili kumlinda mwanamke na
vitendo vilivyo nje ya maadili,” alieleza.
Sheria ya kuanzisha mabaraza ya Vijana Zanzibar namba 16 ya 2013
katika kifungu cha 33 kimesisitiza kuzingatia uwiano wa jinsia katika muundo wa
uongozi katika mabaraza hayo, vile vile katika kifungu cha 34(2) kimeonesha
uongozi wa baraza la vijana
Ambapo kwa Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti, na ikiwa Mwenyekiti
ni mwanamme basi Makamu mwenyekiti awe mwanamke au ikiwa Mwenyekiti ni mwanamke
basi Makamo mwenyekiti awe mwanamme. Sheria kama hii inapaswa iwe ndio muongozo
kwa nyengine.
Kutokana na mapungufu yaliyobainika katika sharia hizo, wadau
hao wamependekeza mambo mbalimbali.
“Pia sheria ya usajili wa vyama vya siasa zirekebishwe ili
ilazimishe vyama kuweka asilimia maalum ya wanawake katika kugombea.
Aidha pia, “vyama
vya siasa viwazingatie na kuwapa vipaumbele wanawake waliojitokeza katika
kugombea na kushika nafasi ya kuwa mtu wa pili au kupitwa kwa kura moja tu.”
Aliongez, “Tunashauri pia sheria zinazotoa haki kwa wanawake
zieleweke vizuri kwa nchi nzima ili wanawake waweze kuzidai haki hizo ikiwemo
makazini katika kupambania haki zao za kisiasa na kijamii.
Mradi wa kushajiisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na
demokrasia ni mradi wa miaka minne (2020 – 2023) wenye lengo la kukuza
ushiriki wa wanawake katika uongozi ambao unatekelezwa na Jumuiya ya
Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Taasisi ya Pemba Gender Advocacy and
Environmental Organization (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway chini
Tanzania.
Comments
Post a Comment