NA HAJI NASSOR, PEMBA:::::
KATIBU Tawala Wilaya ya Mkoani Pemba
Miza Hassan Faki amewakumbusha wakulima wa zao la karafuu Wilayani humo
kutokuzichanganya karafuu zao na takataka nyengine ikiwemo makonyo kwani
kufanya hivyo kunaweza kulipoteza ubora zao hilo.
Alisema
karafuu za Zanzibar zina ubora wa aina yake kuliko maeneo yote Duniani hivyo,
ni wajibu kwa wakulima hao kulifahamu hilo na kuenzi ili liweze kubakia katika
ubora wake.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mkoani alisema, ubora wa zao hilo ni
vyema ukaanzia kwa wakulima iwe katika kulianika kwenye vyombo vinavostahiki.
Alieleza
kuwa, uwanikaji wa karafuu katika saruji, lami, bati na katika vyombo sehemu
inayoanza kupoteza ubora na kuanza kuingia takataka nyengine.
Katibu
Tawala huyo alieleza kuwa, ubora wa zao hilo baada ya kuvunwa kwake hutakiwa
kuanikwa katika vyombo maalumu kama vile majamvi na mikeka ili kudhibiti mafuta
ya karafuu hizo yasipotee kabla ya kufikishwa kituoni kwa ajili ya kuuzwa.
“Niwakumbushe
wakulima wa zao la karafuu waacha kuanika karafuu sehemu za ovyo ovyo na
wahakikishe wanazifanyia usafi wa kina ikiwemo kutoa makonyo na taka nyengine
kabla ya kufikishwa sokoni ili kudhibiti ubora wake,” alisema.
Katika hatua
nyengine Katibu tawala huyo aliwataka wananchi kutoa taarifa wakati wowote
wanapoona viashiria vya usafirishaji wa zao hilo kwa njia ya magendo.
Alisema,
serikali imeweka bei muafaka ya zao hilo ili wakulima na wananchi wengine wauze
katika vituo vya shirika la biashara la taifa la ZSTC hivyo kusiwe na sababu ya
kusafirishwa kwa njia ya magendo.
“Maana kuna
baadhi ya wananchi bado hawajakubali kuuza karafuu katika vituo vilivyowekwa
hivyo ni vyema wakauza kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kwani sheria
zitachuliwa kwa watakaobainika,” alisema.
Wakati huo
huo Katibu tawala huyo aliwataka masheha wa Wilaya hiyo kuendelea kutoa taarifa
ya upigaji marufuku kwa baadhi ya wananchi kujihusisha na ununuzi wa zao la
karafuu kwani ni kichocheo kikubwa cha wizi.
Wakulima wa
zao hilo Wilaya ya Mkoani wameiomba serikali kuendelea kusimamia uuzaji wa zao
hilo ZSTC na sio kwa wananchi waliomitaani kwani husababishwa kwa kiasi kikubwa
wizi wa karafuu.
Mmoja kati
ya wakulima hao Seif Salim Seif mkaazi wa Kengeja alisema, uwepo wa wanunuaji
wa karafuu kiholela ndio moja ya sababu ya kuchangia kuibiwa kwa karafuu zao.
“Moja ya
sababu inayochangia wizi wa zao hilo ni uwepo wa wanunuzi wasiokuwa ZSTC jambo
ambalo hutupa wakati mgumu sisi wakulima wa zao la karafuu,” alieleza mkulima
huyo.
Nae Mkulima
Issa Mohamed Othaman mkaazi wa Kengeja aliwaomba masheha kuwashughulikia
kisheria wananchi wanaonunua zao hilo ili kupunguza wimbi lililoibuka katika
kipindi hichi.
Kwa upande
wake Sheha wa shehia ya Ngwachani Mkoani Issa Ismail Juma alisema, ununuzi wa
zao kwa wananchi ni kinyume na utaratibu uliopangwa na serikali hivyo aliwataka
wananchi wafuate sheria zilizoekwa na sio kufanya wanavotaka wao.
Agosti 17
mwaka huu Waziri wa Biashara na maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaban
alifanya uzinduzi wa uvunaji wa zao la karafuu katika mashamba ya zao hilo
Wilaya ya Mkoani Kisiwani hapa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment