NA MARYAM SALUM, PEMBA
WATU wa zamani walishasema kuwa, maisha ni
kutafuta na sio kutafutana.
Wengine wakaibuka wakisema kuwa,
mtafutaji hachoki na mgagaa na upwa hali ugali mkavu.
Hapa walilenga
mbali kuwa, mtafutaji hachoki na mafanikio yanahitaji juhudi binafsi na wala
hayashuki tu kama mvua mawinguni.
Misemo hii
sasa yamesadifu kwa vitendo kwa mjasiriamali Meiye Hamad Juma (47), akiishi kijiji
cha Mavungwa shehia ya Mbuzini nje kidogo na mji wa Chake Chake Pemba.
ALIPOANZIA UJASIRIAMALI
Mwaka 2016,
ndio bisummillah, mjasiriamali huyo alipofunuka macho yake mawili, na kuanza
kama mchicha kwenye ujasiriamali wake.
Kwa wakati
huo akiwa ni mmoja wa wanachama wa ushirika wa “Tupate Sote” na kujiunza
shughuli mbali mbali za utengenezaji bidhaa.
Lakini 2018,
Meiye alipoamua kuanzisha kikundi chake, kwa kutengeneza bidhaa mbali mbali
ambazo kwa sasa zimemkomboa kimaisha.
‘’Bidhaa
ambazo kwa sasa natengeneza baadhi ni zile nilizoziona kule kwenye ushirika
wangu wa awali, kama vile sabuni ya maji, unga wa lishe unaotokana na mchanganyiko wa nafaka
na mbegu za boga.
Kwake bidhaa
hizo zinampa mafanikio makubwa, ikiwemo kujiamini katika maisha, kupatikana kwa
ada na kuendesha shughuli za familia yake.
Baada ya
kuwiva kiujasiriamali, aliamua kusomesha wajasiriamali wa wengine kisiwani
Pemba, ili waweze kutengeneza bidhaa zao zikiwa kwenye ubora zaidi.
Kumbe Meiye,
ni wale wanaoitekeleza kwa vitendo, ile aya inayomtaka kila mmoja kufikisha aya
japo moja kwa wenzake, na yeye aliamua kuwasomesha wengine.
“Nafasi hiyo
ya kusomesha Wajasiriamali wenzangu nilipatiwa na watendaji wa TAMWA, kwa lengo
la kuwaendeleza zaidi kiutendaji na kuboresha bidhaa zao”, aliongeza.
KUKUA KWA MIEYE KIUJASIRIAMALI
Mwaka 2017
alifanikiwa kutumia taaluma yake kwa kubuni mradi wa kupanda alizeti, na kwa
bahati, walifanikiwa na kujipatia mafanikio makubwa.
“Baada ya
kuvuna alizeti na kuuza, pia tulipatiwa mashine kutoka TAMWA ili kuendeleza
mradi huo na tunajivunia kwa hilo”, anasema.
Mwaka mmoja
baadae, alianzisha ushirika wake rasmi, unaojumuisha wanaume watatu na wanawake
sita, kutoka maeneo tofauti kisiwani Pemba.
Mradi huo aliuanzisha
kwa mtaji wa shilingi 40,000 baada ya kukosa kwenye kisanduku (hisa) na kwa
sasa yupo na mtaji wa shilingi 4,000,000.
Ushirika
aliouanzisha unajishughulisha na utengenezaji wa skrabu ya mwani, mafuta ya
mwani, unga wa lishe kwa kutumia bidhaa tofauti, majani ya chai pamoja na karafuu
za singo.
“Kipaji
changu cha ujasiriamali kumenyanyua maisha yangu na familia pamoja na watu
wengine, na hasa baada ya kuanzisha ushirika wangu mwenyewe,’’anasema.
MAFANIKIO
Moja kuhwa ni kufanikiwa kujenga nyumba ya
kisasa yenye miundombinu yote ikiwemo umeme na maji pamoja na kumiliki vifaa
kama friji pamoja na majiko ya umeme.
Anayoma maduka
mawili moja lipo kijijini kwao Mavungwa, na moja lipo eneo la Machomane kituo
cha Boda boda wilaya ya Chake chake Pemba.
Safari za
mikoa mbali mbali ya Tanzania, na kubwa zaidi na mshiriki wa zaidi ya miaka
saba ya maonesho yanyofanyika Tanzania bara.
“ Mwaka huu
nimempeleka kijana ambae nimemuajiri ili
apate kuona mengi, na kupata uzoefu
zaidi na kutangaza biadhaa zake”,alisema.
CHANGAMOTO.
Moja ya
changamoto kubwa ni ukosefu wa mashine ya kutengenezea mafuta, kwani hutumia
sufuria kwa kutumia na mikono, jambo ambalo
linaweza kuathiri afya yake.
Jengine ni
kuingia gharama za kuvifuata vifungashio nje ya Zanzibar, kutokuwa na soko la
uhakika la kuuzia bidhaa zake, usafiri wakusambazia bidhaa.
“Hutembea
kwa miguu hadi kwenye maofisi, jambo ambalo linanipa wakati mgumu,’’alisema.
Anasema
baada ya kuuliza bei mashine hizo, zinauzwa kati ya shilingi milioni 18, na
nyengine ni shilingi milioni 4 ya kupikia mafuta na shilingi milioni 3.5 mashine
kwa ajili ya kusagia.
Hata hivyo
amewakumbusha wanawake wenzake, pamoja na vijana kujiunga na vikundi vya
miradi ya maendeleo, ambavyo
vitawasaidia katika kujiinua kiuchumi.
MUME WA MJASIRIAMALIA
Hamad Bakari
(Meja), anasema, alianza kumsaidia na kumpa ushirikiano mke huyo, tokea anaanza
sasa, ingawa kutokana na hali yake sasa amebaki kama mshauri.
Uamuzi wake,
anasema ulitokana na kuogopa mke wake, kukata tamaa mapema, katika kuendeleza
mradi wake, ambao kwa sasa anakiri umempa uhakika wa maisha.
“Kwanza mke wangu tumeaminiana namuamini
ananiamini popote anapokwenda, maana alianza kwa kasia na sasa anaiendeleza
ambayo imenipa heshima mimi hapa mtaani,’’anasilimulia.
Mume huyo
tokea mwanzo na hasa alipokuwa mazima wa miguu, alikuwa ndio msambaazaji mkuu
wa bidhaa zinazozalishwa na mke wake.
‘’Sikuwa
naona haya wala aibu kusambaaza bidhaa na kuwaeleza wateja hata wanaume
wenzangu, kuwa hizi zimezalishwa na mke wangu,’’anaeleza.
Kwa sasana
kutokana na kupevuka kwa mjasiriamali huyo, changamoto kubwa ni usafiri wa
kusambaazia bidhaa zake na soko lisilo la uhakika.
WALIOPATIWA MAFUNZO NA MEIYE
Bikombo
Abdalla Hamad, mkaazi wa Micheweni, yeye alimuelezea Meiye kwamba ni
mjasiriamali mkubwa anayejulikana kwa kila sekta kwenye maeneo mbali mbali
ndani ya nchi na nje ya nchi.
“Meiye hana
roho mbaya katika kuwapatia mafunzo wengine kwenye ujasiriamali, lengo ni kuona
wanatengeneza bidhaa zao kwa weledi na viwango na sio kimazoea,” alimsifia.
Alisema Meiye
alipata mafunzo kutoka kwenye taasisi mbali mbali, lakini baada ya kupata
mafunzo hayo, akaona ili elimu ifanye kazi ni vyema kuwapatia na wengine.
Mjasiriamali
Bikombo alisema faida aliyoipata kutoka
kwa Meiye ni kupata elimu zaidi ya kusarifu zao la
mwani katika kutengeneza sabuni, mafuta ya aina mbalimbali.
MTEJA WA BIDHAA ZA MEIYE
Fatma Juma
Kombo, mteja maarufu wa kununua bidhaa
za Meiye kama sabuni, anasema hupendelea bidhaa zake kwasababu ni nzuri, hazina
kemikali.
Anasifia
akisema kuwa, bidhaa za Meiye ikiwemo unga wa uji unamsaidia katika makuzi ya watoto wake,
mafuta anayotumia huondoa maradhi kama mba, fangasi na kuzifanya nywele zake
kupendeza na zenye kuvutia.
“Meiye ni
mjasiriamali anaejali na kuipenda kazi yake na wateja wake, kwani hufuata mteja
popote, ili kumfikishia bidhaa anayohitaji bila kujali changamoto anazopitia,”
alisema Fatma.
TAMWA
Fat-hiya
Mussa Said, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzani TAMWA-Zanzibar,
Ofisi ya Pemba anasema Meiye ni miongoni mwa wajasiriamali, ambao wamewawezesha kitaalamu katika kubuni,
kuanzisha na kuiendeleza miradi yao kiuutalamu zaidi na yenye ubora.
MWISHO.
Comments
Post a Comment