NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amewataka walimu wakuu wa skuli zote kisiwani
Pemba kusimamia uwajibikaji na nidhamu kwa walimu wao, ili wafanye kazi kwa
ufanisi na kuleta maendeleo kwa wanafunzi.
Alisema kuwa, kuna baadhi ya walimu
hawafundishi vizuri, wanaingia na kutoka kazini muda wanaotaka, jambo ambalo
linasababisha kudumaza maendeleo ya wanafunzi na hatimae kuwa na ufaulu wa
kiwango cha chini.
Akizungumzia mara baada ya
kusikiliza changamoto za walimu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Makamu huyo alisema,
wasiende kuchafua mafaili yao kwa chuki binafsi, bali wawape miongozo
inayotakiwa kwa mujibu wa Sheria, ili kufikia yale yanayoitaka Serikali.
"Nawasisitiza kutimiza wajibu
wenu kisheria na sio kwa chuki, kwa sababu kuna walimu hawasomeshi vizuri,
wanaingia na kutoka kazini muda wanaotaka lakini kwenye taarifa zao zote
zinazotetwa ni nzuri kwenye mafaili yao", alisema.
Alisema kuwa, Serikali ya awamu ya
nane kupitia Dk Mwinyi imekusudia kuweka mkazo kwenye Elimu, kwani wanaamini
kwamba kuekeza kwenye sekta hiyo ni mafanikio katika sekta zote nchini.
"Tuanze kufanya vizuri kwenye
skuli za maandalizi, tutakuwa na wanafunzi bora na wenye uwezo wenye kiwango
kinachokubaliwa, tunataka wanafunzi wawe na uwezo mzuri wa kufanya kazi",
alieleza Makamu huyo.
Aidha Mhe. Hemed aliitaka Wizara
hiyo kuhakikisha inawapa maslahi yote walimu, ili waendelee kufanya kazi vizuri
na kuwanasihi kufanya kazi kwa amani kwani hakuna haki ya mtu ambayo itapotea.
"Natoa angalizo na muwape
taarifa vizuri kwa kila alieomba ajira za uwalimu Pemba ajue anakuja kufanya
kazi hapa hapa, kila mmoja aomba katika makaazi husika, Wizara izingatie hilo
hakuna kupewa uhamisho, kwani ndio inayochangia uhaba wa walimu", alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa alisema, lengo la mkutano huo ni
kusisitiza uajiwajibikaji kwa walimu pamoja na kumaliza changamoto
zinazowakabili, ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Waziri huyo alimshukuru Dk. Mwinyi
kwa kuithamini sekta ya elimu ili kuona kwamba inaboreka zaidi katika visiwa
vya Zanzibar kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Alisema kuwa, ni wazi kwamba
Serikali ya awamu ya nane imewekeza katika elimu kwani kupitia fedha za UVUVO
19 wamepatiwa bilioni 68 ambazo ni sawa na bajeti ya miaka 11 ya Serikali
ambayo inaipa Wizara kila mwaka.
"Mjitahidi kuzisema changamoto
zenu zinazowakabili hapa, lengo letu ni kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha
tunapata wanafunzi bora watakaofaulu vizuri ", alisema.
Nae Afisa Mdhamini Wizara hiyo
Mohamed Nassor Salim aliishauri Wizara hiyo kuajiri waalimu ambao ni wakaazi wa
maeneo husika, ili wapate fursa sambamba na kuepuka uhamisho kwa walimu.
"Wanapoajiriwa walimu wanaotoka
eneo lile lile, kutakuwa na walimu wakaazi, kwa mfano Makangale tuna vijana 36
wamesomea fani ya ualimu hivyo tusichukue vijana wa nje", alisema
Alisema, katika kuhakikisha wanaweka
mazingira bora kwa wanafunzi, wanajitahidi kutatua changamoto mbali mbali
ikiwemo kujenga vyoo zaidi ya 300 pamoja kuwaondoa watoto kukaa kwenye sakafu.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba
Salama Mbarouk Khatib alisema, watahakikisha wanaiunga mkono Serikali kwa
kuwapa kipao kwenye ajira walimu wanaojitolea, kwani wamekuwa wakisaidia
maendeleo ya wanafunzi katika skuli mbali mbali.
"Walimu wanaojitolea wanafanya
kazi kwa bidii na kwa nguvu zote, hivyo tutajitahidi kuwapatia ajira
kwanza", alisema Mkuu huyo.
Wakitoa changamoto zao, walimu wa skuli
za Serikali walisema wanahitaji kurejeshewa nauli walizokuwa wakipewa, ili
kufika skuli kwa wakati, kusaidiwa vifaa vya michezo pamoja na kijengewa
madarasa kwa skuli zenye uhitaji.
"Walimu wanaokwenda kusoma
tunaomba wanaporudi wasipelekwe wizarani, elimu watakayoipata wailete kwa
wanafunzi, ili kuongeza kufanisi na ufaulu wa kiwango cha juu", walisema.
Nao walimu wa skuli za binafsi
waliiomba Serikali kuwapunguzia kodi, ili kuendelea kuekeza katika sekta ya
elimu sambamba na kuwasaidia kuwapatia usafiri kwa ajili ya wanafunzi wao,
kwani hawana uwezo na tayari wameshazuiwa kutumia usafiri wa gari za abiria
kusafirisha wanafunzi hao.
"Hatukatai kulipa Kodi kwani
tunajua kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, lakini zimekuwa nyingi kiasi
ambacho tunakaribia kukata tamaa", walisema.
Mkurugenzi Sera na Mipango kutoka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar alisema kuwa, Serikali imejitahidi
kutatua changamoto ya kujenga skuli na madarasa kupitia mradi wa UVIKO 19
ingawa kwa hatua ya awali imeangalia skuli zenye uhitaji zaidi.
"Kazi za ujenzi wa madarasa
zinaendelea hivyo tuwe wastahamilivu Serikali inaendelea kutatua changamoto
hizo, pia tutahakikisha kila Wilaya kunakuwa na skuli zenye dakhalia kadiri
uwezo utakavyoruhusu", alisema Mkurugenzi huyo.
Mkutano huo umewashirikisha walimu
wakuu na wasaidizi wa skuli za Serikali na binafsi, walimu wakuu wa vyuo,
wenyeviti na kamati za skuli, ukiwa na lengo la kutoa changamoto zao
zinazowakabili na kuweza kutafutiwa njia mbadala ya kutatua.
MWISHO.
Comments
Post a Comment