IJAPOKUWA kuanzia serikali za wilaya, mkoa hadi taifa zimeshapiga marufuku kwa wanawake, watoto na watu wengine kuacha kabisa kuokotoa karafuu zinazoanguka “mpeta” lakini bado wengine wanaendelea kupuuzia agizo hilo.
Wapo wanaoendelea kuokota mpeta wakiwa na watoto wao, ingawa sababu za kuokota mpeta wenyewe huwa wanazo na pengine ukizisikiliza zinaweza kuingia akilini.
Maana wengine husema kama ni vitendo vya udhalilishaji, basi vipo hata kabla ya ujio wa zao hili la karafuu, na ndio maana wanadai kuwa anaetaka kudhalilishwa hata kama hakuna karafuu.
Lakini kubwa na lililonileta mbele yenu leo hii na kuutumia ukurasa huu, ni kuwauliza hawa wanaokwenda kuokota mpeta wakiwa wamejipamba wana ajenda gani huko?
Maana utashangaa wakati ukipishana nao au kama utabahatika kupanda gari moja nao, jinsi walivyojipura kama sio kujiremba.
Kiutamaduni kila mmoja anaekwenda kazini hukoga na kujipura jinsi awezavyo, ingawa kila ina mazingira yake, lakini sio kuokota mpeta na kujipambana mbona kama haifanani hivi.
Kumbe lile wazo na agizo la serikali kupiga marufuku uokotaji mpeta kwamba kunaongeza kasi ya udhalilishaji, inaweza sasa kuiingia akilini, maana iweje mtu anakwenda msituni lakini awe sawa na anaekwenda harusini?
Kwa haraka inawezekana usiamini, kwamba wapo akinamama wajane, wari na hata wake za watu lakini wanapotoka kwenda huko kunakoitwa kuuokota mpeta, basi hutamani kuwapisha.
Sujui niende mbali zaidi, kwamba inawezekana mpeta unaotafutwa ni huu wa udhalilishaji au kujipamba huko ni asili ya mtu kusudi, kama hivyo ndivyo basi punguzeni.
Jengine ambalo naendelea kujiuliza kwa kujipamba huko tena, mtu mmoja hukata kundi kila wanapofika kwenye mashamba ya mikarafuu, akidai kuwa kufuatana na watu huzipati.
Jamani neema hii ya karafuu aliotujaalia Allah, sisi waokotaji mpeta na wachumaji tunataka kuichanganya na uovu wa zinaa, jamani huko sio kwa kwenda maana kuna la leo na kesho.
Akinamama hawa na watoto wenye umri tofauti, unaweza kuwashangaa wanaporudi kuokota mpeta, wakiwa na zaidi ya pishi moja, ambayo kimtazamo hilo kwa mpeta wasasa haliwezekani.
Yote kwa yote, jamani wanawake nyinyi ambao mnafuata misingi na madhehebu ya kiislamu ni sahihi hilo mnalolifamnya la kujipamba kwa rangi, asumini na hali uudi mnapokwenda kuokota mpeta?
Kwa hili sasa lazima wanaume ambao ndio wasimamizi wakuu wa nyumba na familia zetu, lazima tujiridhishe na hili maana tumeshaelezwa kuwa, kila mmoja ataulizwa kwa alilolichunga.
Wanawake wenyewe hebu rudini kwa Muumba wetu na wengine kuheshimu ndoa au dini yetu, maana maandishi yasio na shaka yanaeleza wapi na wakati gani mwanamke ajipambe.
Na nyinyi mnaochuma (vibarua) acheni mtindo na tabia ya kuwamiminia karafuu wanawake ambao wengine wako kwenye ndoa, kisha malipo yawe ya udhalilishaji “mali kwa mali” sio jema hilo.
Lakini viongozi wa dini, serikali wa shehia na taifa endeleeni kulikemea hili la uokotaji mpeta tena usio salama, maana inawezekana baada ya kumalizika watoto wanaoitwa wa mzazi mmoja kuongezeka.
Naamini kila kitu kinawezakana ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake bila ya kusimamiwa na rushwa ikawa mwiko.
Hajinassor1978@gmail.com
Aliislam nadhiiif popote alipo na anapokwenda
ReplyDelete