Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA limesisitiza kuwa madai ya wafanyakazi iliyowasilisha serikalini ni halali na litaendelea kufuatilia ili wahusika wapate stahiki zao.
Akizungumza jijini Arusha Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya amesema wamesikitishwa na kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali ya kutaka madai ya wafanyakazi yapuuzwe na kwamba kauli hiyo haikuwa na busara yoyote.
Nyamhokya amesema kwamba madai yao wameyafanyia utafiti wa kina na wanaendelea kusisitiza kuomba serikali itekeleze ahadi zake za nyongeza ya mshahara, upandaji wa madaraja kwa wafanyakazi, nyongeza ya mshahara ya kila mwaka ambayo ipo kisheria na madai ya wafanyakazi yatokanayo na mishahara na yasiotokana na mishahara.
"Tuna madai halali yaliyofanyiwa utafiti wa kina na bado tunahitaji utekelezaji wake kwa haraka ili kuleta nafuu ya wafanyakazi nchini," amesema.
Nyamhokya amesema TUCTA inaendelea kutambua dhamira ya kweli ya Rais John Magufuli katika kutatua changamoto za wafanyakazi nchini na hawataki malumbano na Serikali zaidi ya kushirikiana kutatua kero zilizopo.
Amesema hawahitaji malumbano na serikali na wao kazi yao ni kufuatilia maslahi ya wafanyakazi na sio chama cha siasa kama ilivyodaiwa karibuni na msemaji wa serikali Dk.Hassan Abasi kuwa madai yao yapuuzwe na kwakuwa TUCTA wanafanyasiasa
Amesema si sahihi kuhusisha TUCTA na wanasiasa kwa kuwa wao jukumu lao kubwa ni kutetea masilahi na haki za wafanyakazi tofauti na ajenda za vyama vya siasa kutaka kushika dola.
Comments
Post a Comment