Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Barick nchini imekubali kulipa fidia ya dola milioni 300 ambazo sawa na bilioni 700 za Tanzania, pamoja na kuweka mgao sawa wa faida wa 50/50 na serikali, kufuatia mazungumzo ya ripoti ya makinikia.
Taarifa hiyo imetolewa leo na serikali wakati ikikabidhi ripoti ya mazungumzo hayo kwa Rais John Pombe Magufuli, na kusema kwamba licha ya makubaliano hayo, pia kampuni hiyo imekubali masharti yote yaliyowekwa kufuatia mazungumzo hayo, ili nchi iweze kunufaika na rasilimali zake.
Pia kwenye ripoti hiyo imekubaliwa kuwa migodi yote itaweka fedha zake kwenye akaunti zilizopo hapa nchini, na serikali kubakia na umiliki wa madini yote yatakayokuwepo kwenye makinikia, ukiondoa dhahabu, shaba na fedha ambayo yatakuwa yanamilikiwa na Barrick kisheria.
Pamoja na hayo makubaliano yaliyofikiwa yameitaka kampuni hiyo kuwapa ajira za kudumu wazawa wa eneo husika, na kuwapa stahiki zote kama wafanyakazi, na wamekubali kulipa kile kinachostahili kwenye halmashauri husika ambako migodi ipo.
Kufuatia ripoti hiyo Rais Magufuli ameipongeza timu iliyohusika kwenye mazungumzo hayo, na kuwataka Watanzania kushirikiana katika kuleta maendeleo ya nchi.
Comments
Post a Comment