Baada ya zaidi ya miongo miwili ya
kujitolea, uongozi na harakati za kutetea haki za wanawake, watoto na uhuru wa
vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, Tawi
la Zanzibar (TAMWA–ZNZ), Dk. Mzuri Issa Ali ameaga rasmi waandishi wa habari
kutokana na kuondoka katika wadhifa wake, akiacha taasisi imara yenye mifumo
thabiti na mafanikio yanayotambulika kitaifa na kimataifa.
Akizungumza mbele ya waandishi wa
habari, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wanachama wa TAMWA–ZNZ,
Mkurugenzi huyo amesema waandishi wa habari ndio nguzo kuu ya taasisi hiyo
licha ya changamoto kubwa wanazokumbana nazo lakini bado waliendelea
kushirikiana na Tamwa Zanzibar katika kutumia kalamu zao kuelezea harakati za
shughuli za Tamwa Zanzibar.
“Kama kuna kundi la watu wanaojua
kuuliza maswali magumu, kufuatilia ukweli bila kuchoka, na bado malipo yakawa
madogo au hakuna kabisa, basi hao ni waandishi wa habari. Na cha kufurahisha
zaidi, hao ndio nguzo kuu ya TAMWA–Zanzibar,” alisema.
Alisema kuwa katika kipindi cha kuwa
mtendaji mkuu wa Tamwa Zanzibar alifarijika sana na waandishi wa habari kutokana
na kutumia vyema kalamu na vipaaza sauti katika kueleza changamoto za kijamii
hususan masuala ya haki za binaadamu pamoja na vitendo vya udhalilishaji vya
wanawake na watoto.
“kalamu za waandishi ilikuwa ndio
nguzo kuu ya kutegemea katika kipindi cha uongozi wangu nikiwa mkurugenzi
kalamu zilipaaza sauti za wasio na sauti pamoja na kueleza changamoto za
kijamii hususan katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binaadamu”, alifafanua
mkurugenzi.
Akieleza kuwa mashirikaino hayo ya
karibu yameweza kwa kiasi kikubwa kusaidia jamii na kupungua changamoto za
wanawake na watoto pamoja na makundi mengine ya pembezoni kama walemavu na
wazee.
“Nguvu yetu ilikuwa ni ya waandishi
wa habari tukiamini kuwa nguvu ya habari inaweza kuleta mabadiliko chanya
katika jamii lakini pia kuibua kero za wananchi pamoja na kuizundua serikali”
alisisitiza.
Kupitia miradi mbalimbali, TAMWA–ZNZ
imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake na watu wenye ulemavu 11,120 kupitia
vikundi 572 vya kuweka na kukopa, kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa
kijinsia, na kuchangia mabadiliko ya sheria muhimu ikiwemo Sheria ya Ushahidi,
Sheria ya Mahakama ya Kadhi na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Leo, TAMWA–Zanzibar ina wanachama 82
waandishi wa habari kutoka Unguja na Pemba, wafanyakazi 23 wenye weledi, mifumo
imara ya kifedha inayoendeshwa na wahasibu wenye ithibati ya CPA, pamoja na
ukaguzi wa hesabu unaofanywa na kampuni zilizosajiliwa kitaifa. Taasisi hiyo
pia inamiliki majengo yake yenyewe ambayo yameanza kuchangia mapato ya ndani.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo
alitangaza rasmi kukabidhi majukumu kwa Bi. Nairat Abdulla Ali,
aliyekuwa Meneja wa Programu, akimtaja kuwa kiongozi mwenye maadili, uwezo na
maono thabiti ya kuiendeleza taasisi hiyo.
“Nawaomba wanachama, waandishi wa
habari na wadau wote kumpa ushirikiano mkubwa. Taasisi imara haijengwi na mtu
mmoja, bali hudumu pale uongozi unapobadilika na dira ikibaki ile ile,”
alisema.
Katika hafla hiyo waandsihi wa
habari waliohudhuria waliishukuru kwa dhati Tamwa Zanzibar kwa kuwa nao karibu
pamoja na kuwajengea uwezo katika kuimarisha weledi na umahiri katika taaluma
ya habari.
Khatib Suleiman kutoka Habari leo
amesema kuwa Tamwa imetusaidi kutujengea uwezo hususan katika kuandika kwa
weledi na kuimarisha uwezo wetu katika namna ya kuripoti masuala ya haki za
wanawake na watoto pamoja na haki za binaadamu kwa ujumla.
“Tamwa Zanzibar imekuwa ni chuo
katika kuimarisha taaluma ya uandishi na tumeweza kuandika kwa weledi na
umahiri huku tukizingatia maadili ya wanahabari”, alifafanua.
Berema Suleiman kutoka Zenji Fm
alisema kuwa tamwa Zanzibar imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha taaluma
lakini pia katika kuwapatia mafunzo waandishi chipukizi katika kuimarisha
utendaji wa kazi zao.
“Mafunzo tuliyoyapata yamesaidia
katika kuimarisha taaluma na kutujengea uwezo hususan katika kufuatilia habari
zetu pamoja na kuwa na vyanzo tofauti na kuwapa nafasi makundi ya wanawake na
vijana pamoja na walemavu”, alifafanua.
Wafanyakazi wa tamwa Zanzibar
walishukuru kwa uongozi wa Dk. Mzuri hususan katika kuimarisha utendaji wa kazi
zao huku wakizingatia weledi na umahiri katika kuandika ripoti na pia kufanya
kazi kwa kuweza kupata matokeo
Zaina Mzee Afisa mwandamizi wa Tamwa Zanzibar alisema kuwa ulipokuja
kuongoza taasisi hii, hukurithi tu ofisi na majukumu, bali pia changamoto
nyingi. Kwa busara, maono na uongozi wako thabiti, uliweza kuibadilisha taasisi
yetu na kuifanya kuwa mfano wa uwajibikaji, mshikamano na utendaji bora. Chini
ya uongozi wako, tulijifunza kuwa kazi si wajibu tu, bali ni wito na dhamana ya
kulitumikia taifa kwa uadilifu.
Akitoa
neno la shukurani mkurugenzi mpya wa Tamwa Zanzibar Nairat Abdulla amesema kuwa
napokea
dhamana hii nikiwa na ufahamu kwamba uongozi si kauli, bali ni vitendo;
si ahadi, bali ni uwajibikaji. Ninapokea nafasi hii nikitambua kuwa taasisi
huimarika si kwa mipango iliyoandikwa vizuri pekee, bali kwa utekelezaji
thabiti, wenye nidhamu na mwelekeo unaofahamika.
Ninawaahidi kushirikiana nanyi kwa
karibu, kusikiliza kwa makini, na kuchukua hatua kwa wakati. Milango yangu
itakuwa wazi kwa hoja, mawazo na suluhisho, kwa sababu uongozi wa pamoja na
mashirikiano ni muhimu katika kuimarisha kazi zetu, alisisitiza.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kutoa
zawadi mbali mbali kwa mkurugenzi aliyemalaiza muda Dk. Mzuri Issa ikiwa ni
sehemu muhimu ya kutunza kumbukumbu ya utumishi wake uliotukuka.
End.
Comments
Post a Comment