NA SAIDA ALI, PEMBA@@@@
SERA
ya Elimu ya Zanzibar, imetaja elimu mjumuisho, ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu
wanapata haki sawa kama ilivyo wingine.
Sera hiyo ya mwaka 1991 ya Zanzibar, kipengele cha elimu
ya watu wenye ulemavu, ibara 4.9 kimeainisha kuwa hakutokuwa na kikwazo wala
sababu ya kumnyima haki yake hiyo.
Imezungumzia Wizara ya Elimu na tasisi husika, itashirikiana
ili kuhakikisha elimu inatolewa kwa misingi bora kwa watu wote.
Hapa nayo Sheria ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar nambari 8
ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (1), kimesisitiza haja kwa watu wenye ulemavu,
kupewa haki zote za msingi za kibinaadamu sawa na watu wingine.
‘’Watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu wote
watachanganywa, ili tu kupatiwa elimu bora,’’ilifafanua shehemu ya sheria hiyo.
Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa wenye ulemavu nambari
19 ya mwaka 2024, inaelezea waraka wa Baraza la Mawaziri kuwapa
huduma bora kupitia serikali, mamlaka husika na tasisi binafsi.
Nayo sheria ya mama ya nchi, katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984 kifungu 10 (f), kinasisitiza kuwa serikali, inawapa huduma za kutosha kwa
watu wote, fursa za kielimu katika madaraja yote.
Mkataba wa
kimataifa wa haki za watu mwenye ulemavu mwaka 2006, ibara ya 24 imeeleza kuwa
nchi wanachama zilizoridhia
Mkataba huu, wanawajibu wakuhakikisha kuwa haki za watu wenye ulemavu
zinasimamiwa ikiwemo elimu.
‘’ Mfumo wa elimu hauwatengi watu wenye
ulemavu na kwamba watoto hao hawabaguliwi, kwenye elimu kuanzia ya msingi hadi sekondari
kwa mfumo jumuishi,’’unafafanua mkataba huo.
Aidha
mkataba huo wa mwaka 2006 ukaenda mbali zaidi, kwa kufafanua kuwa watu wenye
ulemavu, wahakikishiwe kuwa wanapata usaidizi unaohitajika ndani ya mfumo wa
elimu, ili kuwawezesha kuelimika.
WANAFUNZI WENYE ULEMAVU
Hanifa Hemed Abdalla ni mwanafunzi anasoma skuli ya Michakaini
darasa la nne, anasema ingawa skuli hiyo wapo walimu wenye uwezo wa kuwafundisha,
bado skuli haijazingatia miundo mbinu.
Anasema skuli yao limekuwa kikwazo kwao ya kushindwa
kufika madarasa ya juu, kwani hakuna usaidizi ‘lift’ wala kisaidizi chingine hapo.
‘’Skuli yetu bado imekuwa kikwazo, hatuwezi kufika juu ya
ghorofa wala hakuna kisaidizi cha aina yoyote, tunaishia madarasa ya chini,’’anasema.
Nae Sumaiya Saleh Juma ambae ni mwanafunzi wa darasa la
kwanza skuli hapo, mwenye ulemavu wa viungo, anasema skuli yao imekuwa na vifaa
vya kufundishia kwa watu wenye ulemavu.
‘’Ndani ya skuli yetu kuna vifaa vya kutosha vya
kufundishia mpaka vya kuchezea, tunavyo na vyoo maalumu, ingawa kikwazo ni kwa
wale wenye ulemavu wa viungo kufika umbali wa jengo,’’ anasema.
WAZAZI
Asha Khamis Faki wa kijiji cha Bomani shehia ya
Mchangamrima mwenye mtoto mlemavu, anasema kukosekana kwa miundo mbinu ya elimu
mjumuisho skulini hapo, haikuwa kikwazo cha kumpeleka mtoto wake.
‘’Nafahamu kuwa skuli ya Jonwe, anayosoma mtoto wangu
hakuna mpango jumuishi wa elimu, vifaa ingawa niliona nisimfungie ndani, ajumuike
na wenzake katika kutafuta elimu iliyozungurukwa na changamoto,’’ anasema.
Nae mzazi Salama Haji Mohamed, anasema haki ya kupata
elimu kwa mtoto wake mwenye ulemavu, alihisi iko mbali kwa kutokuwepo mpango
elimu jumuishi skulini hapo, ingawa hilo hakuliangalia.
Anasema mtoto wake anaesoma darasa la pili, ni mithili ya
mwamanafunzi anaewapeleka na kuwarudisha wenzake, kutokana na uwezo wa ufahamu
wake kuwa mdogo ukichangiwa na miundo mbinu hafifu jumuishi.
‘’Anakwenda tu nakurudi kama anaewapeleka wenzake, lakini
bora aende changamoto na misukosuko ya elimu yatamkuta akiwa
darasani,’’anafafanua.
WAALIMU
Mwalimu mkuu wa skuli ya Michakaini Fatma Ali Khamis,
anasema ndani ya skuli hiyo kuna wananfunzi tisa wa madarasa mjumuisho na 24 wa
kitengo.
Anasema wanafunzi wote hao hupewa elimu ya mjumuishi,
pamoja kuwazingati kwa pamoja ili kuhakikisha wanapata haki yao ya elimu.
Aziza Juma Salim ni mwalimu wa skuli ya Michakini anaesomesha
wanafunzi wenye ulemavu, anasema hapo skuli ya Michakaini kipo kitengo maalum
kwa wanafunzi wenye ulemavu wa akili, uoni, hata viungo.
‘’Changamoto kubwa ni jengo kumekuwa hakuna visaidizi
hawawezi kufika umbali wa madarasa ya juu kwa wale wanaohitaji japo kwa
kutembea,’’anasema.
Amekuwa akiwasomesha wanafunzi hao, kwa hatua ya kwanza
mpaka pale atakapopata uelewa wa kutosha, humpeleka darasa la elimu mjumuisho,
kwa yule ambaye anauwezo wa kufikia na ikiwa changamoto kwa kutoweza kufikia humuacha
madarasa ya hapo chini.
Zulekha Ali Rashid ni mwalimu wa skuli ya Jonwe anasema
darasani mwake, kuna wanafunzi wenye ulemavu amekuwa akiwasomesha kibubusa, kwa
kutokuwepo miindumbinu jumuishi.
Anasema hana uelewa wala ujuzi wa kuwasomesha wanafunzi
wenye ulemavu, maana skuli yao bado sera ya elimu hajafikiwa, hakuna vifaa vya
kuwasomeshea wala mkalimani wa lungha ya alama.
‘’Kwakweli skuli yetu bado, maana hapana mahitaji ya
wanafunzi hawa, nimekuwa nikiwasomesha tu kibubusa na kiishara mpaka nikafikia
pale nilipokusudia,’’anasema.
Fatma Mabrouk Khamis ni mwalimu wa skuli ya Michakaini
elimu mjumuishi anasema sera ya elimu imefikiwa kwa kiasi, wamepata mafunzo
kutoka kwa walimu wenzao, ya kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu.
WIZARA YA ELIMU
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim anasema, wapo katika mikakati ya kuwasaida wanafunzi, katika skuli za elimu mjumuisho kwa kuwapatia mafunzo walimu wa ukalimani wa lugha za alama.
‘’Niwatoe hofu wanafunzi, waalimu na jamii, tupo katika
mchakato wa kubadilisha sera ya elimu, ili iweze kunufaika kwa watu wote.
Waziri Ofisi ya Makamu Kwanza wa Rais Zanzibar Harusi
Said Suleiman, amenukuliwa akisema kuwa, wapo waalimu 40, waliokwishapewa
mafunzo ya lugha ya alama.
‘’Hizi ni moja ya juhudi za kuhakikisha wanafunzi wenye
ulemvu, wanapata haki ya elimu, kama walivyowingine katika skuli zetu za Unguja
na Pemba,’’anasema.
Anasema, juhudi nyingine zinazofanywa na serikali ni
kufanya ziara katika majengo mbali mbali zikiwemo skuli, na yapo 22
yalishatembelewa, ili kubaini changamoto.
JUMUIA ZA WATU WENYE ULEMAVU
Mashavu Juma Mabrouk ni Mratibu wa Baraza la watu wenye
ulemavu, anasema jamii jumuishi ni watu wote wasaidiwe wenye ulemavu, kwa kila
kitu kinachofanyika wajumuishwe kupitia skuli wanazosoma.
Wamekuwa wakishajiisha masuala ya miundombinu rafiki,
majengo yawe na ramsi, vyoo jumuishi hata wakalimani wa lugha za alama, ni
jambo la lazima.
Mkurugenzi Mtendaji shirikisho
la watu wenye ulemavu Ali Machano, anasema ni kweli mifumo ya elimu
haijazingatiwa, katika skuli za mjumuisho na majengo ya kisasa hayapo katika
mazingira wezeshi kwa wanafunzi.
MWISHO.





Comments
Post a Comment