NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@
NOVEMBA 1, mwaka huu Rais mteule wa
Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikula kiapo cha uaminifu cha kushika
madaraka ya urais kwa awamu ya pili.
Sherehe hizo zilifanyika uwanja wa New
Amani Complex, kuanzia majira ya saa 12: 00 asubuhi, huku umati wa wananchi
wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla,
wakijitokeza.
Sherehe hizo, ni ishara ya kumalizika kwa
uchaguzi mkuu, uliopigwa Oktoba 29, mwaka huu na wazanzibari laki 448, 832 kumpa
kura za ushindi, ambayo ni sawa na asilimia 74.8.
Kisha, Rais huyo wa Zanzibar, alimteua
Mwanasheria mkuu wa Zanzibar Mwinyi Talib Haji, hapo ni sawa na kusema, anaanza
kupanga safu yake ya awamu ya pili.
Pamoja na kumtea Makamu wa Pili wa rais akiwa
ndie mtendaji mkuu wa serikali, bila shaka sasa zamu ya baraza la mawaziri linafuata.
WANAHARAKATI WANASEMAJE
Dk. Mzuri Issa Ali, ambae ni Mkurugenzi
wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, anampa heko
Dk. Mwinyi kwa ushindi huo.
Anasema, hilo linatokana na utendaji wake
uliotukuka, kwa awamu ya miaka mitano ya kwanza, huku akisaidiwa kwa karibu na
watendaji wake, wakiwemo wanawake.
‘Nakumbuka vyema kwenye wizara 16, wanawake
walikabidhiwa majukumu kwenye wizara tano, jambo ambalo ni la kupongezwa,’’anasema.
Mkurugenzi anasema, kwa awamu saba zilizopita,
awamu ya Dk. Mwinyi nayo, iliwaamsha wanawake, kwa kukabidhiwa madaraka makubwa,
kwenye wizara tano.
Anakumbuka hata idadi ya wakuu wa wilaya
wanawake, nayo iliongezeka, maana kati ya wilaya 11, wanawake walikuwa kwenye wilaya
nne, ikiwemo ya Micheweni na Magharibi Unguja.
Tatu Abdalla Msellem Mwenyekiti wa Jumuia
ya Tumaini Jipya Pemva ‘TUJIPE’, anasema Dk. Mwinyi, amekuja kuwainua wanawake
kiungozi, na kuwaonyesha watu, kuwa wanaweza.
‘’Kwa mfano hata kisiwani Pemba, walikuwepo
maafisa wadhamani wanawake watatu, jambo ambalo ni la kutia moyo,’’anasema.
Yeye anaona, hata idadi ndogo kiasi
wanawake hawakuwa wakipewa nafasi za kuongoza, maana ilionekana kama vile,
hawana uwezo.
Mohamed Hassan Abdalla, Mkurugenzi wa
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’, anasema, awamu ya
Dk. Mwinyi, ilikuwa na manufaa kwa wanawake na uongozi.
‘’Mimi niliposikia amemteua Katibu Mkuu
Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Said, nilipiga
saluti,’’anasema.
Kumbe nafasi hiyo, tokea yalipofanyika mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ilikuwa haijawahi kukaliwa na mwanamke, hadi alipokuja Dk. Mwinyi.
Ama kweli hawakukosea wahenga, waliosema mgaa
gaa na upwa, hali ugali mkavu, kama vile kugaa gaa ni kule, kupiga kelele kuwa
wanawake wanaweza.
NINI WANASHAURI KWA BARAZA LA MAWAZIRI
LIJALO
Wanaharakati akiwemo Kaimu Mratibu wa
TAMWA-Pemba Amina Ahmed Mohamed, kwamba sasa wakati wa 50 kwa 50 kwenye safu ya
baraza la mawaziri, ionekanake.
‘’Dk. Mwinyi ni kipenzi cha watu, ni mpenda
kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi, na hili sasa ni wakati aone mawaziri
wanawake na wanaume, wanakuwa sawa,’’anashauri.
Halima Haji Msiu wa Chambani Mkoani,
anasema ili safu yake ya uongozi ikae sawa, wakati wa kuzingatia wanawake
kwenye baraza la mawiziri, ndio huu.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba Salama
Mbarouk Khatib, alinukuliwa akisema, wanawake wamepata fursa ya kipekee, ndani
ya awamu ya nane.
‘’Na hili la kuweka idadi sawa ya wanawake
na wanaume, kwenye baraza la mawaziri Dk. Mwinyi ni msikivu mno,’’anasema.
Mratibu wa baraza la taifa la watu wenye
ulemavu, Mashavu Juma Mabrouk, anasema ni vyema kwa Dk. Mwinyi, kuwazingatia wanawake na hasa wale wenye
ulemavu.
‘’Walau kwa awamu iliyopita, alikuwepo
Katibu Mkuu mwenye ulemavu tena mwanamke, ni vyema kwa baraza lijalo,
wakaongezeka,’’anashauri.
Mwanafunzi wa kidato cha sita skuli ya
Kiwani Mkoani Amina Haji Khamis, anasema wziara ikiongozwa na mwanamke, mara
zote hufanya vizuri.
‘’Nani asieoona maendeleo ya sekta ya
elimu, barabara na hata makaazi ni wizara ambazo kwa awamu iliyopita, zilikuwa zinaongozwa
na wanawake,’’anasema.
Issa Haji Mohamed wa Wete, anasema hakuna
kashfa wala kesi kutoka kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchaumi Zanzibar
‘ZAECA’, ikiihusisha wizara inayoongozwa na mwanamke.
‘’Wanawake wamekuwa watii, wachapakazi,
mahodari, wabunifu na wasiotumia vibaya madaraka yao, hivyo ipo haja kwa baraza
jipya lijalo la mawaziri, wakafia idadi sawa,’’anasema.
AWAMU YA NANE ILIYOPITA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikuwa na wastani wa wizara 16, ikiwemo ya
Elimu na Mfunzo ya Amali.
Wziara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, wizra ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Makaazi, Ardhi na Mejenzi
pamoja na ile ya wanawake na watoto, ambazo ziliongozwa na wanawake.
Eneo jingine ni nfasi nyeti ya Katibu Mkuu
Kiongozi na Katib wa Baraza la Mapinduzi, Katibu Mkuu ujenzi na mawasiliano
ambazo zilishikwa na wanawake.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, mkuu wa wilaya
ya Magharibi, Chake na Mkoani na maafisa wadhamini ikiwemo wa Ikulu na uwekezaji
zilishikwa na wanawake kwa ujasiri.
NYARAKA ZA KISHERIA
Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na
kisiasa wa mwaka 1976, ukitaja moja ya haki za kila mmoja ni kushiriki, uongozi
bila ya ubaguzi, wakiwemo wanawake.
Tena hata mkataba wa kimataifa wa kutokomeza aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake ‘CEDW’ wa mwaka 1979, ukasisitiza Ibara ya 7, kwamba lazima hatua zichukuliwe,
kuhakikisha wanawake wanakuwa na ushiriki sawa kwenye ulingo wa siasa.
Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 21(1), kinasisitiza kuwa, watu wote ni sawa
mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi, kupata haki mbele ya sheria.
Mwisho


Comments
Post a Comment