Skip to main content

CHILO: WAGOMBEA CCM MTAMBILE KULIBADILI JIMBO

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmshauri kuu ya CCM taifa Khamis Hamza Chilo, amesema wateule waliopewa ridhaa na chama hicho, wanatosha kulibadili jimbo la Mtambile kimaendeleo.

Chilo, aliyasema hayo Septemba 27, 2025 uwanja wa mpira Kengeja jimbo la Mtambile, wilaya ya Mkoani, kwenye uzinduzi wa kampeni kwa nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani wa jimbo hilo.

Amesema, CCM haijawi kufanya kosa katika kuteua wagombea, iwe ngazi ya udiwani, uwakilishi, ubunge na urais, kwani huwa tayari wameshaandaliwa kiutumishi.



Alieleza kuwa, wananchi wa Jimbo la Mtambile, wahakikishe kura zao ikifikapo Oktoba 29 mwaka huu, wanawapa kura za ndio wagombea hao, ili kuja kuwalipa maendeleo.

Chilo alifahamisha kuwa, wagombea wote hawana shaka, na suala la kushirikiana na wananchi, katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030.

‘’Mimi nawahidi wananchi wa Jimbo la Mtambile kuwa, wagombea mlioletewa sio maji taka, ni wapambanaji, wapiganaji na wenye uchu wa maendeleo,’’alifafanua.

Aidha Chilo, aliwakumbusha wananchi hao wa Jimbo la Mtambile kuwa, ili wagombea hao watekeleza vyema Ilani ya CCM, wawape kura wagombea urais wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha alisema, tayari CCM imeshatekeleza mambo kadhaa ndani ya Jimbo la Mtambile, ikiwemo ujenzi wa soko, hospitali ya kisasa na barabara kadhaa za ndani.

Alifahamisha kuwa, CCM imekuwa ikiyatekeleza hayo kwa nia thabiti, ya kuhakikisha inazidi kuwapa neema bila ya ubaguzi wowote wananchi.

‘’CCM imeshatekeleza miradia kadhaa ya kimkakati ikiwemo ujenzi ambao umeshaanza wa uwanja wa ndege, bandari ya Shumba, upanuzi wa bandari ya Mkoani pamoja na hospitali za rufaa,’’alifafanua.



Akiwanadi wagombea hao, alisema mgombea Mwakilishi Ali Suleiman Juma, ana sifa za utumishi na anamfahamu vyema, hasa kwa usikivu wake.

Kuhusu mgombea Ubunge Mohamed Abdalla Kassim, anasema ni mtu sahihi kwa wakati huu sahihi, kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Awali Katibu wa CCM mkoa wa kusini Pemba Kajoro Vyohoroka, aliwapokea wanachama kadhaa, kwa niaba yao 10, kutoka chama cha ACT-Wazalendo jimbo la Mtambile.



Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwanachama huyo Seif Khalfan ‘mkongwe seif’ alisema waliamua kutoka, huko baada ya kuona chama cha ACT-Wazalendo kukosa mwelekeo.

Mapema Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mkoani Ali Juma Nassor, alisema chama hicho, hakina sera za porojo na ubishi, bali ni nidhamu na heshima kwa watu wote.

Aidha, aliwaomba wananchi wa kukumbuka kuwa, ahadi zilizoahidiwa kwa miaka mitano iliyopita, CCM imevuuka lengo, na kuwaomba tena kuwapa ridhaa tena.

‘’Kwanini tunaomba muwachaguwe wagombea wa CCM, maana tulishatekeleza ahadi kwa miaka mitano iliyopita, tupeni tena ridhaa tuendeleze na kuanzisha mingine,’’alifafanua.

Nae mbunge mteule kwa nafasi ya vijana kanda ya Pemba, Zainab Abdalla Issa, aliwaomba wananchi hao, kura zao, wasijewakazipoteza kwa kuvipa vyama visivyo na dira.



‘’Wagombea waliomo ndani ya CCM na wenye hadhi na haiba na wale wa vyama vingine, ni wapita njia na msibabaike nao,’’alisema.

Aliongeza kuwa, akishirikiana na viongozi wa jimbo hilo, watahakikisha kila kijana anakuwa na usafiri wa kazi wa piki piki, pamoja na kuwepo kwa miradi mkakati.

‘’Kwanini vijana na mama mtilie, wapite wakilalamika juu ya namna ya kujiwezesha, wapeni kura wagombea wote wa CCM, waliomo ndani ya Jimbo la Mtimbile,’’alifafanua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na uslama ya wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, amewakumbusha wananchi, kutokubali kushawisha kuvuruga amani, iliyopo.

‘’Wananchi wote washiriki kupiga kura kwa amani na utulivu, na mkimaliza mrudi nyumbani, kuendelea na shughuli zenu, msikubali kuzilinda kura, vipo vyombo maalum,’’alifafanua.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtambile Mohamed Abdalla Kassim, amesema ameamua kugombea nafasi hiyo, ili kulibalisha jimbo.




Alieleza kuwa, vijana na wananchi wingine, akipata ridhaa hawatojuta, maana ana hamu kubwa ya kuhakikisha, anawafariji.

‘’Kupitia Ilani hii ya CCM ya miaka mitano ijayo, mnaweza kutulaumu ikimalizika, kama hatujafanikiwa kuwaletea maendeleo, kama yalivyoahidiwa,’’alisema.

Kwa upande wake Mgombea uwakilishi wa jimbo hilo, Ali Suleimana Juma, amesema nia yake ni kuona, jimbo hilo linang’ara kimaendeleo.





‘’Kama niliaminiwa kuongoza wilaya na mkoa, siwezi kushindwa kuongoza Jimbo la Mtambile, maana miundombinu ipo ikiwemo Ilani ya CCM,’’alifafanua.

Uzinduzi huo wa kampeni, uliambatana na shamra shamra za wasanii kadhaa, akiwemo Mboso, Mashauzi na wasanii wingine.

         Mwisho

Comments