IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA @@@@
WAHARIRI kisiwani Pemba wametakiwa kuwasimamia vyema waandishi wao kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, ili habari zao zilete mafanikio katika jamii.
Akizungumza na wahariri katika Ukumbi wa TAMWA Chake Chake Pemba, Afisa Mawasiliano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA), Sophia Ngalapi alisema kuwa, waandishi wengi tayari wameshapewa mafunzo kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa kupitia mradi wa kupambana na Mabadiliko ya tabianchi (ZanAdapt), hivyo ni jukumu la wahariri kusimamia ili ziandikwe habari zenye ubora.
Alisema kuwa, kupitia sauti za wanahabari, wanaamini kwamba zitaisaidia jamii hasa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabianchi ambayo huathiri sana maendeleo katika maeneo wanayoishi.
"Mabadiliko ya hali ya hewa yanaleta athari mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, hivyo kupitia kalamu za waandishi wataibua changamoto na kupatiwa ufumbuzi unaofaa kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla," alisema Afisa huyo
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, mwandishi wa habari mwandamizi Ali Mbarouk Omar alisema, waandishi wa habari wanapaswa kujua nafasi ya mwanamke katika mabadiliko ya tabianchi na athari zinazoweza kuwapata, ili waweze kutoa elimu itakayoisaidia jamii kuzuia athari hizo.
Alieleza kuwa, kuna athari nyingi zinazoweza kujitokeza ikiwemo kupotea viumbe wa baharini na kukosekana kwa mazalio ya samaki, maji kupanda juu ya makazi ya watu, joto kuongezeka na kusababisha maradhi mbali mbali.
"Kupitia vyombo vyetu vya habari tujitahidi sana kuzungumzia hali hii ili wanajamii waielewe, itatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo huathiri pia na kilimo, huku tukijua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa maendeleo yetu," alieleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa Zanadapt Pemba Omar Mtarika Mselem alisema kuwa, bila ya ushirikiano na waandishi mradi huo hauwezi kuleta mabadiliko ya haraka na ndio maana wakaamua kuwa pamoja kwa ajili ya kuleta mafanikio katika jamii.
"Malengo yetu ni kuwafikia watu 4,000 na kati ya hawa asilimia 80 ni wanawake, ambapo asilimia 40 kati ya hao 80 tunataka vijana, lakini pia tunaweza kufikia watu 20,000 kwa sababu tumepanga kuwa ukimuelimisha mmoja basi umeelimisha watu watano," alisema Mtarika.
Alieleza kuwa, mradi huo umelenga katika shehia ya Kiuyu Minungwini, Mchangamdogo, Kambini na Chwale Wilaya ya Wete, ambapo wanawahimiza wanawake kujikita na kilimo misitu, upandaji wa mikoko, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kusema kwamba muitiko wa wakulima ni mkubwa kwa sasa hasa kwenye kilimo misitu.
Nao wahariri walisema kuwa, watahakikisha wanatoa elimu kwenye vyombo vyao vya habari kuhakikisha jamii inakuwa na uwelewa juu ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ili kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa na taasisi ya Community Forest Pemba (CFP) kwa kushirikiana na TAMWA kupitia ufadhili wa Shirika la linaloshughulikia masuala ya wanawake la Canada (Global Afear).
MWISHO.
Comments
Post a Comment