TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI WANAWAKE WAMEJITOKEZA, VYAMA VIWATEUE.TAREHE: 27/07/2025.
Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi wanaviomba vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawateua wanawake waliokidhi vigezo, kugombea nafasi za uongozi ndani ya vyama vyao kwenye uchaguzi wa ushindani ndani ya nafasi za uwakilishi, ubunge na udiwani.
Kwa muda mrefu wanawake wamekuwa nyuma katika siasa na kuelekezwa kugombea tu katika nafasi za viti maalum ambapo vinahusisha wanawake wenyewe kwa wenyewe na hivyo kutokuonesha uwezo wao halisi katika siasa za ushindani.
Katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa mbali mbali viko katika mchakato wa chaguzi za ndani za vyama kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025, wanawake wengi wamejitokeza katika siasa hizi za ushindani pamoja na kwamba bado ni kidogo kulinganisha na wenzao wanaume.
Taarifa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizotolewa hivi karibuni kwa Zanzibar zinaeleza kuwa, jumla ya wanachama 1,640 wameweza kurejesha fomu kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani katika majimbo na wadi za uchaguzi Zanzibar, ambapo kati ya hao wanawake ni 406.
Hii ni karibu asilimia 24.7 ya wagombea wote ndani ya chama hicho kikuu nchini. Kwa upande wa taarifa kutoka chama cha (ACT) Wazalendo iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kuwa jumla ya wanachama 435 wamejitokeza kuchukua fomu kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani katika majimbo na wadi za uchaguzi Zanzibar.
Taarifa hizo kutoka kwenye chama cha upinzani kikuu nchini kinaeleza kuwa kati ya hao wanawake ni 40 sawa na asilimia 9.2.
Kwa pamoja vyama hivyo vinasubiri kamati maalum na kamati kuu za vyama vyao kupitisha rasmi idadi ya watia nia hao hasa wabunge na wawakilishi, michakato ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi huu na kumalizikia mwezi ujao.
Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi wanawapongeza wanawake kwa ujasiri huo na kusisitiza kuwa hawapaswi kuishia kwenye hatua ya kuchukua fomu tu lakini wanastahili kupewa nafasi halisi ya kushindana majimboni.
Katika uchaguzi uliopita wa 2020 Zanzibar ilipata wawakilishi wa nane tu katika Baraza la Wawakilishi sawa ana asilimia 16 na wabunge wanne sawa na asilimia 8 kupitia siasa hizi za kiushindani kwenye majimbo yake 50.
Tunawashauri na kuwaomba wajumbe wa vikao vya uteuzi kuwapigia kura wanawake wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea wa mwisho na kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko katika kujenga Zanzibar njema inayofuata misingi ya heshima na usawa wa kijinsia.
Kuwepo wanawake katika nafasi za uongozi ni dalili kubwa kuwa nchi inaweza kusonga mbele vizuri kimaendeleo ya kiuchumi, kijamii na kidemokrasia kwa vile tafiti nyingi ulimwenguni zimeonesha kuwa wanawake ni viongozi wanaoweka mbele zaidi maslahi ya familia na nchi pia ni waadilifu, wasikivu na wenye kujitoa na kujitolea zaidi.
Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1979 katika kifungu cha pili kinahimiza kutetea haki za wanawake ambapo kinazitaka nchi wanachama ikiwemo Tanzania kuchukua hatua zote za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo kuwa na michakato maalum ya kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway wanawahamasisha wanawake wote waliotia nia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, wasikatishwe tamaa na wendelee kuwa na nia njema ya uongozi kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Imetolewa na: JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA ZNZ xxxxcxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Comments
Post a Comment