WANANCHI wa kijiji cha Majenzi
shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani, wameamua sasa kuyarejesha malezi ya pamoja,
ili kuwa na taifa la sasa na baadae, lenye malezi, makuzi na maadili mema.
Wakizungumza kwenye kikao cha
pamoja kilichofanyika leo Juni 8, 2025 kijijini hapo, wameamua kuanzia sasa malezi ya vijana wao,
yawe ya pamoja, ili kuona wanakuwa na taifa lenye viongozi wenye maadili.
Walisema, kwa sasa vijana
waliowengi kijijini hapo, wamekuwa na malezi yasioendana na maadili, jambo
ambalo linahatarisha usalama wao na wazazi wao.
Mmoja kati ya wazazi hao
Habib Mohamed Habib, alisema ni jambo jema kuona wazazi kuanzia sasa
wanakusudia kusaidiana malezi, maana mzazi mmoja pekee ni vigumu kufanikisha
malezi.
‘’Mimi naunga mkono suala la
malezi ya pamoja, katika kijiji chetu, maana hali imekuwa mbaya ya maadili ya
vijana wetu, na kusababisha uwepo viashiria vya uhalifu kama wizi,’’alisema.
Nae mzazi Bashiru Mohamed Omar,
alisema katika kufanikisha malezi hayo ya pamoja, suala la ukweli na umoja ni
jambo la lazima.
‘’Kwenye malezi ya pamoja,
lazima tuwe na wivu wa maendeleo, na hili litapelekea kufanikiwa kwa kuwa na
watoto wenye maadili, kwa ajili ya sasa na baadae,’’alifafanua.
Nae mzazi Abdalla Omar Mohamed,
ameshauri kuwa suala la kuanza kwa malezi, lisisubiri wiki tatu zijazo, bali lianze
sasa, kwani uharibifu na mporomoko wa maadili ya vijana unaendelea.
Mapema Mwenyekiti wa kamati
ya maadili, elimu na ushauri ya kijiji cha Majenzi Mohamed Ali Hassan, alisema
wameamua kuwaita wazazi wenzao, ili kutafuta dawa ya malezi ya watoto wao.
‘’Ni kweli mzazi mmoja pekee
yake halei, lazima sasa tushirikiane, maana uovu wa watoto wetu umekuwa mkubwa
na kuhatarisha wingine,’’alisema.
Nae Katib wa kamati hiyo
Hassan Ali Said, alisema maandalizi ya kesho mbele ya Allah, yanaandaliwa leo
tena hapa hapa duniani, kupitia vijana na wazazi.
‘’Kila mtu ni mchunga na
ataulizwa kwa alichokichunga, hivyo tuanze hapa duniani kuwaelekeza watoto wetu
tabia njema na kuachana vitendo viovu,’’alifafanua.
Hivi karibuni Mkuu wa wilaya
ya Mkoani Dk. Hamad Omar Bakar, aliwakumbusha wazazi na walezi kusaidiana malezi,
ili kuwa na watoto wenye maadili.
Mwanaharakati wa haki za
wanawake na watoto Pemba, Sifuni Ali Haji, amesema wakati umefika kwa sasa,
jamii kuwa pamoja katika malezi.
Mwisho
Comments
Post a Comment