NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WACHEZAJI wa timu ya mchezo wa Pete ya Wanawake ya Mchanga mdogo wilaya ya Wete, wamesema wanatamani kushiriki, ligi kuu ya mchezo huo, ili kukuza vipaji vyao.
Walisema, wameamua kuchagua kuanzisha timu ya mchezo huo, wakiamini kuwa wanaweza kusonga mbele kwenye eneo hilo kupitia ligi kuu ya Zanzibar, itayoanzishwa.
Hayo yameelezwa na wachezaji na viongozi wa klabu hiyo leo Machi 24, mwaka huu wakati wakizungumza na waandishi wa habari, kufuatilia tathmini ya mafanikio ya mradi wa āāmichezo kwa maendeleo,āāuliokuwa ukitekelezwa na TAMWA, ZAFELA na CYD.
Walisema, baada ya kupewa mafunzo na TAMWA ya umuhimu wa kushiriki kwenye michezo, kwa maendeleo wamehamasika kuanzisha timu ya mchezo wa pete.
Walisema, wanazotaarifa kuwa, kwa upande wa Pemba, mchezo huo haujawahi kuanzishiwa ligi kuu, iwe ngazi ya wilaya au mkoa, jambo linalotishia ndoto zao.
Mchezaji wa timu hiyo Zainab Rashid Said, amesema ni wakati sasa kwa viongozi kuhakikisha ligi ya mpira wa pete, unaingia kisiwani Pemba.
āāSera ya michezo ya mwaka 2018, inaelekeza michezo kwa wote, inahimiza kuimarisha miundombinu, ikiwemo kuwa na ligi maalum ambayo, itatuwezesha kuonesha vipaji vyetu,āāalieleza.
Nae mchezaji Amina Kudra Ali, alieleza kuwa ili michezo iwe kivutio kwa wanawake, lazima wawekezaji wajitokeza, ili iwe sababu ya kupata ajira kupitia sekta hiyo.
āāTumeamua kujiingiza kwenye mchezo wa pete, ingawa changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa ligi maalum, ambayo ingekuwa kichechezo kwetu,āāalieleza.
Kwa upande wake, Katib wa klabu hiyo Bimkubwa Maulid Othman, alikiri kuwa, mafunzo waliopewa na TAMWA, yamewasaidia kukusanyana na kuanzisha klabu hiyo.
āāNi kweli timu hii imeasisiwa baada ya mafunzo ya michezo kwa wote, kutoka TAMWA, ingawa tokea zamani suala la uwepo wa ligi ni ngumu,āāalieleza.
āāKwa mfano mwaka jana, tulianzisha bonanza la shehia, na kucheza na timu mbali mbali, lakini yakimalizika timu inakosa motisha wa kuiendeleza,āāalieleza.
Hata hivyo alisema wamekuwa wakiwaomba viongozi wao wa Jimbo la Kojani, kuwaanzisha ligi maalum, kama ilivyo kwa mpira wa miguu, ingawa matokeo sio mazuri.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha net ball wilaya ya Wete Idrisaa Maulid Othman, alikiri kuwa kwa upande wa Pemba, hakujawahi kufanyika kwa ligi maalum, ya mpira wa pete.
āāFedha huwa ndio kikwazo, hata tunapowasiliana na viongozi wa juu, na hii ni changamoto ya kuukosesha nguvu na uhai mchezo huu,āāalifafanua.
Hata hivyo Makamu huyo Mwenyekiti wa CHANEZA wilaya ya Wete, amewataka wachezaji walioweka nia kwenye mchezo huo, kuendelea kufanya mazoezi, na kuahidi kuwaombea katika mabonanza mbali mbali.
Afisa Mawasiliano, kutoka TAMWA Zanzibar, Khairat Haji Ali, alisema kazi yao kubwa ni kuwahamasisha wanawake kuingia katika michezo.
Alisema, jamii haikuwa ikiwaangalia vizuri wanawake kwenye kukuza vipaji vyao, hivyo suala la kuanzishwa la ligi maalum, inaweza kufanya na mamlaka nyingine.
Hata hivyo alisema kupitia mradi huo, wanajivunia kwa timu ya Mchanga mdogo center, kuamua kujikusanya baada ya kupata mafunzo.
āāHata vifaa kama jezi na mpira, tukipata uwezo wa kifedha tutaziwezesha, ili ndoto zao zifikie mbali, kama ilivyo kwa wanamichezo wingine,āāalifafanua.
Hata hivyo, amewaomba viongozi kuwaunga mkono wanawake waliojiekeza kwenye michezo, kwani wana haki kama ilivyo kwa wanaume.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, akisoma hutuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025, alisema mradi wa uimarishaji wa viwanja vya michezo, unatekelezwa ndani ya programu ndogo ya uendeshaji na ukuzaji wa michezo.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, wizara iliidhinishiwa kutumia shilingi mlioni 34.278 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbali mbali za ujenzi wa viwanja vya wilaya na ukarabati wa viwanja vya michezo.
Alisema mradi mwingine uliotekelezwa ni mradi wa āāSports for Development in Africaāā ambao unafadhiliwa
na Shirika la Kimataifa la GIZ kutoka Ujerumani.
Mwaka 1978, Shirika la Umoja wa Mataifa, Sayansi na Utamaduni āUNESCOā lilitoa tamko la kila mtu kupata fursa ya kufanya mazoezi na kucheza.
Hali ya ushiriki wa makundi yote katika baadhi ya michezo, haijawa ya kuridhisha ni kutokana na tathmini ya sera ya michezo iliyofanyika 2013, ambayo inaonesha asilimia 23 ya watu wote ndio wanaoshiriki michezo.
Sera ya Michezo ya Zanzibar ya mwaka 2018, ibara ya 3.5.1 imeelezea, serikali itahakikisha watu wote wanapata fursa ya kushiriki michezo, kwa kuwekewa miundombinu bora.
Aidha sera hiyo ibara ya 3.5.2, imelezea kuwa, mkakati mwingine wa sera hiyo, ni kuandaa kampeni maalum (mabonanza), zitakazowahamasisha watu wote wa rika zote na makundi yote kushiriki michezo.
Kifungu (d) ikafafaua kuwa, ni lazima kuwashajiisha wanawake kushiriki michezo na kuwawekea mazingira mazuri, ikiwemo viwanja, vifaa na mafunzo.
Aidha dira ya sera hiyo, imeeleza kuwa, ifikapo mwaka 2030, Zanzibar kuwa kitovu cha michezo kwa ubora wa maendeleo ya michezo kitaifa, kikanda na kimataifa.
Zanzibar ilianza michezo mwaka 1875 kufuatia ziara za manuwari za waengereza, wajerumani na zile kutoka Sweeden.
Michezo ilishika kasi zaidi kwenye miaka ya 1879 hadi 1898, na kabla ya vita vikuu vya dunia 1914 na 1918, baada ya vita vikuu vya dunia na miaka ya 1926 na 1942 wakati wa kipindi cha Ukoloni.
Mwisho
Comments
Post a Comment