NA ZUHURA JUMA, KU@@@@
WANAWAKE wametakiwa kuacha tabia ya kuweka vitu kwenye sehemu za siri, kwani wanaweza kuathiri mfumo mzima wa viungo vya uzazi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa chama cha Waandishi Tanzania (TAMWA) Mkanjuni Chake Chake Pemba, Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar alisema, kuna baadhi ya wanawake huweka vitu katika sehemu zao za siri, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya uzazi.
Alisema kuwa, ni vyema wakawa wanafika hospitalini na vituo vya afya kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili ikiwa wamepata matatizo waweze kupatiwa matibabu na sio kuweka vitu ambavyo vinaweza kuwapatia madhara zaidi.
"Kuna baadhi yao huweka vitu kama wanajitibu baada ya kupata magonjwa ya kujamiiana na kuna wengine wanaweka vitu hivyo kwa urembo, haya yote hayafai kwa sababu wanaweza kuathirika katika mfumo wa kizazi," alisema Katibu huyo.
Aidha, akielezea kuhusu maambukizi ya magonjwa ya kujamiiana alisema, pia yanasababisha kuathiri kizazi cha mama na kupeleka mtoto anaezaliwa kupata madhara mbali mbali.
"Maradhi ya kuambukiza ikiwemo ukimwi, saratani ya shingo ya kizazi, gonoria, pangusa, kisonono cha usaha ni hatari katika kuharibu mfumo mzima wa uzazi kwa mwanamke, hivyo waache tabia ya kufanya ngono zembe kuepuka magonjwa hayo," alieleza.
Mapema akifungua mkutano huo Afisa Uhusiano kutoka TAMWA Zanzibar Khairat Haji Ali alisema kuwa, elimu ya afya ya ni muhimu sana kuwafikia wanajamii, hivyo ipo haja kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao katika kuielimisha jamii.
Alisema kuwa, wameamua kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kusudi waelewe masuali ya afya ya uzazi, jambo ambalo litawasaidia kutoa elimu kwa jamii wakiwa na ujuzi wa hali ya juu.
"Wanawake wanapata shida kubwa kwenye mfumo wa uzazi bila kujijua, hivyo iwapo waandishi tutaweza kutoa elimu, jamii itaelewa na watakuwa ni wenye kupima afya zao na kuacha Yale ambayo yatawasababishia matatizo," alisema.
Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo walisema kuwa, watahalikisha wanaibadilisha jamii kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi, ili kuondosha madhara yanayowapata wanawake na watoto.
"Tumejifunza mambo mengi ya afya ya uzazi, hivyo kupitia elimu hii, itatusaidia kuielewesha jamii ili wajitunze na kuepuka madhara mbali mbali," anaeleza.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliwahusisha waandishi wa vyombo vya habari mbali mbali kisiwani Pemba ambayo yameandaliwa na TAMWA Zanzibar.
MWISHO
Comments
Post a Comment