NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKUU wa Divisheni ya Katiba na Sheria Pemba Bakari Omar Ali, amewasisitiza wasaidizi wa sheria, kukumbuka kuwa, bado dhana ya kujitolea kwa aina ya kazi yao hiyo, itabakia pale pale licha ya changamoto walizonazo.
Alisema, kwa mujibu wa sheria inayowaongoza, ni kosa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria na kisha kuomba malipo kwa mwananchi husika.
Mkuu huyo wa Divisheni, aliyasema hayo leo Febuari 09, 2025 ukumbi wa mikutano wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ wakati akitoa maoni yake, baada ya kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti kwa wasaidizi wa sheria, kisiwani humo.
Alisema, ijapokuwa sasa wapo wanaodai malipo kama baraka ya kufanyakazi zao, lakini bado sheria haitambuwi uwepo wa posho kama motisha wa kufanya kazi zao.
Alieleza kuwa, msingi mkuu wakati walipoomba kazi hiyo na sasa ikiingizwa ndani ya sheria yao, ni kufanyakazi kwa njia ya kutolea, na hasa kwa wananchi wanyonge na makundi maalum.
‘’Kwenye sehemu ya utafiti huu, kumeibua hoja kwa baadhi ya wasaidizi wa sheria, wakilalamikia kukosa posho, wakati wanapotekeleza wajibu wao, wakati kisheria hiyo ni kazi ya kujitolea,’’alifafanua.
Akizungumzia kipengele kilichoibuliwa cha vitendea kazi, alisema tayari hilo serikali kuu inalifanyia kazi kwa vitendo, ikiwemo kukabidhiwa kwa usafiri aina ya bajaji kwa baadhi ya jumuiya za wasaidizi wa sheria wa Unguja na Pemba.
Hata hivyo, aliwataka wakuu wa jumuiya hizo, kuzibeba changamoto zilizomo kwenye matokeo ya awali ya utafiti huo, ili kuziweka hai jumuiya zao.
‘’Kwa mfano kuna suala la kutokuwepo kwa fursa sawa za kimafunzo na safari kikazi, migogoro, kubaguzi na mambo haya ndio yanayoweza kuibua changamoto za kutoelewa baina ya viongozi na wanachama,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Divisheni ya Katiba na Sheria Pemba Bakar Omar Ali, aliwataka wanachama, kujenga utamaduni wa kudumu wa kupita katika taasisi zao, ili kupata taarifa mpya.
Akiwasilisha matokea ya awali ya sehemu ya utafiti huo, Msaidizi wa sheria kutoka wilaya ya Mkoani Saleh Mussa Alawi, alisema kiujumla Jumuiya ziko vizuri hasa katika eneo la upatikanaji fursa sawa.
Alisema eneo jingine, ambalo matokeo yanaonesha liko vizuri ni usahirikishwaji kwa wanachama, wakati viongozi wanapotaka kufanya uamuzi.
‘’Lakini hata la uwiyano wa wanawake na wanaume, katika fursa, nalo linaonesha katika jumuiya zetu, liko vyema ingawa changamoto ni wanachama wenyewe,’’alifafanua.
Akichangia mataokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alisema matokeo hayo, yanahitajika kuwasilishwa mbele ya wanachama wote.
‘’Hii itasaidia kuweka sawa zaidi, maana bado changamoto ipo kwa viongozi wa Jumuiya hasa katika kuifuata katiba kabla ya kufanya uamuzi,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani ‘MDIPAO’ Nassor Hakim Haji, alisema suala la uwiyano sawa kati ya wanachama wanawake na wanaume, linaweza kuwa na changamoto kutokana na idadi kutofanana.
‘’Kwa mfano ‘MDIPAO’ inawezekana wanachama wanawake ni wingi, sasa fursa za watatu watano, inabidi wanawake wawe wingi, sasa hapo lazima shida itajitokeza,’’alifafanua.
Nae Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete ‘WEPO’ Hemed Ali Hemed, alipongeza waliofanya utafiti huo na uandishi wa ripoti, kwani umetoa taswira ya aina ya jumuia zao zinavyoendeshwa.
Mkurugenzi fedha wa ‘CHAPO’ Riziki Hamad Ali, alisema itapendeza kama ripoti hiyo, baada ya marekebisho wanachama watawasilishiwa.
Mkutano kama huyo unatarajiwa kufanyika tena April 12, mwaka huu, kwa ajili ya kuwasilishwa mapendekezo yaliotokana na mkutano wa uliofanyika leo.
Mwisho
Comments
Post a Comment