Skip to main content

WANANCHI KASKAZINI PEMBA, ZITUMIENI SIKU 3 ZA KAMBI YA KISHERIA

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI wa mkoa wa kaskazini Pemba, wametakiwa kuzitumia siku tatu za kambi ya kutoa masaada wa kisheria, ili kufikisha malalamiko yao ya kisheria, na kupatiwa ufumbuzi papo hapo.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 17, 2024 na Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, katika hutuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari, kwenye uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, iliyozinduliwa uwanja wa Majengo Micheweni Pemba.

Alisema, siku tatu hizo watakuwepo wanasheria, Jeshi la Polisi, wasaidizi wa sheria, mahakim na mawakili, ili kusikiliza changamoto za kisheria na kuzitolea ufumbuzi papo hapo.

Alieleza kuwa, kuwapata wanasheria wakati mwingine huwa ni vigumu, ingawa kufuatia uzinduzi wa kampeni hiyo, wanapatikana papo hapo bila ya malipo.

‘’Niwatake wananchi wa mkoa wa kaskazini Pemba na hasa wa wilaya ya Micheweni, kufika hapa Micheweni majengo, ili kupata elimu na msaada wa kisheria tena bila ya malipo,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Idara ya Katiba na Msaasa wa kisheria, katika kufanikisha kampeni hiyo.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisema kampeni hiyo ni matokeo ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, juu ya upatikanaji wa haki kwa wote.




Alieleza kuwa, kampeni hii inawafikia wananchi moja kwa moja, ili kuhakikisha wanafikisha malalamiko yao ya kisheria na kupatiwa ufumbuzi bila ya malipo.

Aidha, aliwataka wananchi ambao hawatabahatika kufika Micheweni, kuendelea kuwatumia wasaidizi wa sheria waliomo katika shehia zao, ili kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria.

Mapema Mwakilishi wa shirika la UN-Women Racho Ngoma, alisema uhitaji wa elimu ya msaada wa kisheria, umekuwa ikiogezeka siku hadi hapa Tanzania.



Katika hatua nyingine, Mwakilishi huyo wa UN-Women, alisema bado suala la ukatili wa kijinsia, limekuwa kubwa, na kusababisha wananchi 1,954 kwa mwaka 2023 kwa Zanzibar pekee kupewa msaada wa kisheria.

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, kwa kampeni hiyo ndani ya wilaya yake.

Alikiri kuwa, ndani ya wilaya hiyo ipo migogoro ya ardhi, matunzo ya watoto, utelekezaji, migogoro ya ndoa ambayo wananchi wanahitaji kupewa elimu na usaidizi wa sheria.



Afisa Mdhamini wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali, alisema aliwataka watoa msaada wa kisheria, kuzingatia viwango wakati wanapowahudumia wananchi.






Awali Mkuu huyo wa mkoa, aliyapokea matembezi ya wananchi, wasaidizi wa sheria na wanasheria yalioanzia kijiji cha Chamboni hadi uwanja wa majengo, ambapo ujumbe wa mwaka huu ‘Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo’.

Imefahamika kuwa, kuanzia leo Oktoba 17 kutakuwa na kambi ya utoaji wa msaada wa kisheria bila ya malipo hadi Oktoba 19, katika eneo hilo.

         Mwisho

 

 

Comments