WANAMTANDAO wa kupambana na vitendo vya
udhalilishaji kisiwani Pemba, wamelaani kitendo cha watu wazima, kukimbilia kwa
watoto wachanga, kuwadhalilishaji, kwani husababisha athari
zaidi kwao.
Walisema, miongoni mwa athari hizo ni kuwasababisha
kukosa kizazi, kuwatishia masomo, athari za kisaikolojia jambo ambalo linatajwa
kuzima ndoto zao za maisha.
Wakizungumza kwenye kikao cha kuwasilisha ripoti za
kazi zao, kilichofanyika ofisi ya TAMWA Pemba, walisema, sasa vitendo hivyo
wadhalilishaji wameelekeza nguvu zaidi kwa watoto wadogo.
Walieleza kuwa, zipo kesi kadhaa zinazowahusu watoto
wenye umri kati ya miaka mitano hadi 10, wakifanyiwa udhalilishaji na wanaume
wenye umri kuanzia miaka 40 hadi 50.
Mwanamtandao kutoka wilaya ya Mkoani Haji Shoka
Khamis, alisema sasa wabakaji wameelekeza nguvu kwa watoto wadogo, jambo linalokuwa
gumu wanapofika mahakamani.
‘’Wadhalilishaji sasa wamehamia kwa watoto wadogo,
na kisha huwapa lugha za vitisho, kwamba wasitowe taarifa kwa familia zao, jambo
linalokuwa gumu mbele ya vyombo vya sheria,’’alieleza.
Kwa upande wake Rashid Hassan Mshamata mwanamtandao
kutoka Wete, alieleza kuwa wamekuwa wakiziibua kesi hizo, ingawa changamoto ni
baada ya kuzifikisha mahkamani.
‘’Ukishafika mahkamani, kesi za watoto hukataa
kusema jambo lolote, hii inatokana na kupewa lugha za vitisho na wabakaji na
wadhalilishaji,’’alifafanua.
Nae mwanatandao Rehema Mjawiri, alisema wapo baadhi
ya wazazi wanaendelea kutafunwa na muhali, jambo ambalo hukosa nguvu wa kuziendelea
kesi za watoto wao.
Aidha Seif Mohamed Abdalla, alisema pamoja na kuendelea
kutoa elimu ya kupingana na vitendo hivyo, bado hali ya udhalilishaji inazidi
kunawiri.
‘’Tunajipa moyo kuwa, kadiri vitendo vinavyoripotiwa,
hutokana na jamii kupata uwelewa na kujua wapi sasa waende, kuripoti matendo
hayo yanapotokezea,’’alifafanua.
Mtendji kutoka TAMWA Zanzibar Mohamed Khatib
Mohamed, alisema TAMWA imefurahishwa kuona kazi za wanamtandao zinaendelea
kufanywa, hata baada ya kumalizika kwa miradi.
‘’Suala la kutoa elimu kwa jamii ya kupambana na
vitendo vya udhalilishaji, ni jambo la kila siku, sasa TAMWA inawapongeza kuona
mnaendelea,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, mtendaji huyo, aliwasisitiza
kuendelea kufanya kazi hiyo, kwani jamii bado inahitaji uwelewa na hasa suala
la muhali wa kutoa ushahidi mahakamani.
Akizungumza hivi karibuni, Mkuu wa mkoa
wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema suala la kushirikiana na
vyombo vya sheria ni jambo jema.
‘’Zipo kesi hufutwa mahakamani, kwa kule
mashahidi kutofika mahakamani, jambo ambalo huvizisha kesi za udhalilishaji,’’alieleza.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wilaya ya
Chake chake Salma Khamis Haji, alisema njia ya kutokemeza matendo hayo, ni kwa
watendewa, kutoa taarifa, pindi wanakapoona viashiria vya ukatili na
udalilishaji.
Sheikh Abdalla Nassor Mauli, alisema kama jamii itaamua
kukifuata kitabu cha Allah kwa vitendo, matendo hayo yatapungua, hata kabla ya
kufanyika kwa utafiti wowote.
Matukio ya ubakaji, ulawiti ambayo
huwakumba wanawake na watoto hapa Zanzibar, yameripotiwa kupungua kiduchu kwa
mwezi Machi, na kufikia 125, upungufu wa matukio 50 kwa mwezi Febuari mwaka
huu.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya Mtakwimu mkuu
wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaonesha kuwa mwezi Febuari pekee kuliripotiwa
matukio 175, sawa na matukio sita kwa siku.
Ingawa kwa mwezi Machi, kumeripotiwa
wastani wa matukio manne kwa siku, ambapo ikaelezwa kuwa, kwa miezi hiyo mwili,
kuliripotiwa matukio 300, ambayo ni wastani wa matukio 28, kwa kila wilaya,
kati ya zote 11 za Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment