NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI
wa shehia ya Shungi wilaya ya Chake chake Pemba, wameikumbusha serikali, kuwajengea
barabara yao ya Chanjamjawiri- Tundaua kwa kiwango cha lami, ili wapate kuitumia
kwa utulivu.
Walisema,
kwa sasa imesambaa mashimo na msingi yenye kina kirefu, jambo ambalo haliwapi
utulivu, wakati wanapokwenda kwenye shughuli zao za kimaisha.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi shehiani hapo, walisema barabara hiyo ambayo awali ilikuwa
na lami, kwa sasa zaidi ya miaka minne imekuwa ikihataraisha waenda kwa miguu,
achia mbali wanaotumia vyombo vya moto.
Mmoja kati
ya wananchi hao Moza Suleiman Mohamed wa Misooni alisema, hasa wao akinamama wamekuwa
wakipata usumbufu mara pale wanapokuwa wajawazito.
‘’Hutokezea
sisi kutakiwa kuripoti hospitali ya Chake chake kwa huduma na uchunguuzi zaidi,
lakini tunapoitumia barabara kutokana na mashimo yaliomo, hupata mtikisiko,’’alieleza.
Nae Asma
Said Abdalla wa Chanjamjawiri, alisema barabara hiyo ndio wanayoitumia
wanapotaka kwenda kwenye vijiji kadhaa vya shehia hiyo, ingawa hali yake imeshachakaa.
Nae Mbarouk
Idrissa Omar, alisema kutokana na kuchakaa kwa barabara hiyo, imekuwa ikiwawiya
vigumu wafanyabiashara pale wanaposafirisha bidhaa zao, kutoka kijijini kwao kwenda
mjini.
‘’Kwa mfano,
siku nyingine husafirisha ndizi, muhogo, matikti au nyanya, lakini hata
zikifika sokoni zimeshashuka thamani, kwa kule kuvurugika kutokana na mashimo
makubwa,’’alieleza.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia kero za watu wenye ulamavu shehiani humo,
Khadija Mohamed Suleiman, alisema uchakavu wa barabara hiyo, huwa ni kikwazo kwa
wenye ulemavu, wanapokuwa kwenye shuguhuli zao.
‘’Kwa mfano,
hata wanafunzi wenye ulemavu wa viungo na wale wasioona, wamekuwa wakipata usumbufu,
kuanzia wanapotoka nyumbani hadi skuli, kwa kule kuwepo miundombinu isiyorafiki
barabarani,’’alieleza.
Nae mzazi Zulekha
Nassor Hilali, alieleza kuwa ni vyema kwa serikali, kupitia wizara husika,
kuangalia uwezekano wa kuwajengea kwa kiwango cha lami barabara yao, ili iwasaidie
katika shughuli zao.
Sheha wa
shehia ya Shungi Hamad Ramadhan Soud, alisema taarifa alizonazo kuwa, ni kuwa
wakati wowote serikali, itaanza upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa barabara hiyo.
‘’Kwa hakika
taarifa za moja kwa moja kuwa ujenzi wa barabara hii utaanza lini sijaambiwa,
lakini tunaambiwa kuwa bado serikali inayo nia ya kuijenga barabara hiyo, kwa
kiwango cha lami,’’alieleza.
Afisa Mdhamini
wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema
barabara hiyo, imo kwenye mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami.
Alieleza kuwa,
katika mpango mkuu wa wizara unaojumuisha kilomita 371, na barabara za ndani zimo
ikiwemo hiyo ya Chanjamjawiri-Shungi hadi Tundaua wilaya ya Chake chake.
Alieleza,
kwa sasa hawajaanza hata mpango wa tathmini kwa wananchi wanaoishi pembezoni wa
barabara hiyo, ingawa wakati ukifika, wahusika wa zoezi hilo wataarifiwa
mapema.
‘’Ni kweli barabara
hiyo imeshachakaa na zipo nyingi kama hizo, lakini ipo kampuni imeshateuliwa
kwa ajili ya ujenzi, na wakati ukifika wananchi wataarifiwa, ili watoe ushirikiano,’’alifafanua.
Akizungumza hivi
karibuni kwenye ufunguzi wa barabara ya Kijangwani-Birikau, Waziri wa wizara
hiyo Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema baada ya muda mfupi, miundombinu ya
barabara za ndani kisiwani Pemba, zitang’ara.
Shehia ya Shungi iliyopo wilaya ya Chake chake Jimbo la Chonga, inao wananchi 3,884 ambapo inaundwa na vijiji vya Missoni, Shungi, Kiziwani, Chanjamjawiri, inayo miundombinu ya elimu, afya, maji safi na salama na barabara.
Mwisho
Comments
Post a Comment