NA MARYAM NASSOR, PEMBA @@@@
HUKUMU ya rufaa ya dawa za kulevya inayohusisha kete 1,678 iliyowasilishwa mahakama kuu Zanzibar, kanda ya Pemba, imekataliwa na Jaji wa mahakama hiyo, Ibrahim Mzee Ibrahim, baada ya kubaini kuwa, upande wa mashtaka tokea awali, ulithibitisha kosa pasi na shaka yoyote.
Jaji Ibrahim akitoa uamuzi wa rufaa hiyo na baada ya kujiridhisha, aliamuru
mshtakiwa huyo Zubeir Jerad Said wa Bopwe Pemba, kutumikia chuoa cha mafunzo,
kwa muda wa miaka 10, kama alivyohukumiwa awali mahakama ya mkoa.
Alisema kuwa, mahakama yake
imeitupilia mbali rufaa hiyo, kutokana na kuwa upande wa mashtaka, ulikuwa na
mashahidi ambao walitoa ushahidi wa wazi na wakuaminika, hivyo hawezi kuipindua
hukumu hiyo.
Jaji
huyo alisema kuwa, mshtakiwa alikamatwa na na dawa hizo na kupewa jina la
kielelezo ‘pw3 na pw4’, ambacho ni mfuko wa dawa za kulevya aina ya heroin kete
uliokuwa na 1, 678 zenye uzito wa gramu 41.53.
Alieleza kuwa, wakili wa utetezi Abeid Mohamed
Said wakati anaomba rufaa, aliieleza mahakama sababu ya rufaa, kuwa mteja wake,
hakupatiwa haki kutokana na ushahidi uliyotolewa na kumtia hatiani, haukufikia
kiwango au ulichezewa.
Wakili
wa utetezi alidai kuwa, ukamataji wa mteja wake, haukufuata sheria na ulikuwa
kinyume na kifungu cha 35 (1) na (4) cha sheria namba7 ya mwaka 2018.
Alidai
kuwa, mteja wake alikamatwa hadharani na askari waliokuwa kwenye doria, lakini
hawakuita shahidi huru hata mmoja, ili
kushuhudia kitendo hicho, hivyo inaoneshaa askari Polisi hao walikuwa na nia
mbaya.
“Mteja
wangu alikamatwa hadharani na Polisi waliyokuwa doria, lakini baada ya
kumkamata hawakuita shahidi huru ambae angeshuhudia tukio hilo,” alidai wakili
huyo.
Aidha, alidai kuwa, pia mnyororo wa kesi ulikatika,
hiyo inathibitishwa na kuwa vielelezo vilivyopewa majina ya ‘pw3 na pw4’ kwani
kulikuwa hakuna ushahidi wa maelezo wapi kielelezo hicho kilihifadhiwa, mara baada
ya kufikishwa kituoni.
Hivyo,
kwa mantiki hiyo, wakili Abeid, aliiomba mahakama hiyo, itupilie mbali hukumu hiyo, adhabu ibatilishwe na mteja wake
achiwe huru.
Akijibu,
tuhuma hizo, Mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Ali, alisema kuwa ni kweli
mshtakiwa alikamatwa hadharani, ingawa ilikuwa ni usiku majira ya saa 4:00 hivyo,
ilikuwa vigumu kumpata mtu huru kwa wakati huo.
Alidai
kuwa, muomba rufaa huyo, ushahidi ulimtia hatiani moja kwa moja, kutokana na
kuwa alikamatwa na mfuko wa kete 1,678, aliyokuwa kautia ndani ya fulana yake.
Aidha
alidai kuwa, mnyonyoro wa kesi haukukatika, mara baada ya mtuhumiwa kukamatwa
na kufikishwa Polisi, pamoja na kielelezo chake, alikabidhiwa askari
aliyekuwepo na ilipofika asubuhi, alikabidhiwa mtunza vielelezo na kupewa namba
WIR2008/2021.
Alidai,
kuhusiana na kukiukwa kwa kifungu cha 35(4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2018 alidai
kuwa, kifungu hicho hakijakiukwa, kwani mara nyingine sio lazima kufuatwa kwa
kifungu hicho, hasa kutokana na mtuhumiwa hakubainisha ni watu wapi wapewe
taarifa, kuwa yeye yupo kituoni.
Baada ya kuupitia ushahidi huo, Jaji Ibrahim
alisema kuwa, ameupitia kwa umakini mkubwa
ushahidi huo na kujiridhisha, kwa kuona upande wa mashtaka, ulifanikiwa kuthibitisha
tuhuma hizo pasi na shaka, kwani ulikuwa na nafasi nzuri ya kuwaona mashahidi
katika mazingira hayo.
Kwa
mantiki hiyo, rufaa hiyo imekataliwa na mshtakiwa anatakiwa kutumikia kifungo
chake cha miaka 10 chuo cha mafunzo, alichohukumiwa na mahakama ya Mkoa hapo
awali.
Shauri
hilo lilifunguliwa Juni 16, mwaka 2021, katika mahakama ya mkoa na mshtakiwa ni
Zubeir Jerad Said (30) mkaazi wa Bopwe wilaya ya Wete Pemba.
Mshitakiwa
huyo, alipatikana na dawa hizo, Juni 6, mwaka 2021 eneo la Bopwe majira ya saa
4:00 usiku, ambapo bila ya halali, alipatikana na kete 1,678 zenye uzito wa gramu
41,53.
Kupatikana
na dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 21 (1) (d) cha sheria za Mamlaka ya
kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Zanzibar, cha sheria namba 8 ya mwaka
2021, sheria za Zanzibar.
MWISHO
Comments
Post a Comment