NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIAR
JUHUDI za wahariri kutoka vyombo mbali mbali vya habari
nchini zimesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuleta mabadiliko katika
matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu nchini.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo
katika Mkutano wa wahariri wakuu wa vyombo vya habari kuelekea
maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani uliofanyika Ukumbi wa Sheikh
Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema
wahariri wakuu wana jukumu la kupitisha na kuweka sawa maandishi yote
ndani ya Vitabu, Magazeti na majarida hatua ambayo imesaidia kwa kiasi
kikubwa kukuza lugha ya kiswahili .
Aidha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wahariri kulinda Maadili
ya kazi zao katika kuyaibua mambo mbali mbali yasiyoendana na mila,
tamaduni na silka zetu bila ya kumuonea Mtu au Taasisi fulani.
Sambamba
na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana
katika lugha ya Kiswahili na kuwataka wenye ujuzi wa Lugha hiyo
kuchangamkia fursa hizo ikiwemo ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi na
utangazaji wa habari pamoja na ufundishaji wa Lugha hiyo kwa wageni.
Ameeleza
kufurahishwa kwake kwa kuona kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa
(BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuweka mikakati katika
Nchi mbali mbali ya kukizungumza na kukieneza kiswahili ikiwemo
Ujerumani, Uholanzi, Italia, Nigeria, Nchi za falme za kiarabu, Malawi,
Rwanda na Zimbabwe hatua ambayo ni dhahiri ya umahiri wao katika
kutangaza Lugha hiyo.
Ameeleza
kuwa mbali na juhudi hizo tayari Nchi zisizopungua Thalathini na Nane
(38) kupitia Redio na vituo vya Televisheni vinarusha matangazo yake
kwa Lugha ya Kiswahili.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelitaka Jukwaa la wahariri kushirikiana
na Mabaraza ya Kiswahili nchini kuhakikisha vyombo vya habari vinatumia
kiswahili fasaha na Sanifu .
Kwa
kuzingatia upekee wa lugha ya kiswahili Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na
Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeamua kuifanyia marekebisho Sheria ya
Habari ili iendane na Mabadiliko yanayotokezea katika Sekta ya
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nchini.
Kwa
upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia
Maulid Mwita ameeleza kuwa Serikali ina Mkakati wa kukifanya Kiswahili
kuwa ni bidhaa itakayowanufaisha wataalamu na Taifa kwa ujumla ikiwemo
kupeleka walimu kusomesha Kiswahili nje ya Tanzania pamoja na
kuwakaribisha wageni kusoma Lugha ya Kiswahili ndani ya Tanzania.
Aidha
Mhe. Tabia amewataka wahariri wakuu kukemea tabia ya wachache
wanaotumia Misamiati kinyume na maana zilizokusudiwa ili kudhibiti
ufasaha wa Lugha ya Kiswahili.
Nae
Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Khamis Mwinjuma
ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuchukua jitihada mbali mbali katika
kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inakuwa ni Nembo ya Taifa la Tanzania.
Amesema
ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanaitangaza Lugha ya Kiswahili
ikiwemo kuibua Utalii wa Lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha wageni
wanaotembelea Tanzania wanatumia fursa zitokanazo na Lugha hiyo.
Akitoa
maelezo kuhusu Jukwaa hilo Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la
Taifa (BAKIZA) Bi Consolata Mushi ameeleza kuwa Jukwaa hilo litakuwa ni
chachu ya kupunguza changamo to za Kiswahili zinazojitokeza katika
Vyombo mbali mbali vya Habari.
Comments
Post a Comment