Na Najjat Omar – Unguja.
Wadau wa masuala ya kijamii na kijinsia wamekutana kwa pamoja kuzungumzia sera na sheria zinahusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na mapungufu yake.
Mkutano huo ambao umeendaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Zanzibar –TAMWA uliokutanisha wadau kutoka katika Taasisi mbalimbali za kijamii na kiserikali kujadili juu ya ufuatiliaji,utekelezaji na kutoa maoni juu sera na sheria zinahusu masuala ya udhalilishaji wa kijinsia kwa jamii hususan watoto.
Takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaonesha matukio hayo yameongezeka kutoka matukio 1,222 mwaka 2021 hadi matukio 1,360 mwaka 2022, ongezeko ambalo ni la matukio 138.
Takwimu hizo zinaonesha kwamba kwenye matukio 1,361 yaliyotokea mwaka 2022, matukio 1,173 yalijumuisha watoto, 185 yalihusu wanawake na matatu yalihusu wanaume. Kwenye matukio 1,173 ya watoto, 889 walikuwa ni wasichana, huku 284 walikuwa ni wavulana.
Akifungua mkutano huo Afisa miradi kutoka TAMWA –Pemba Fathiya Mussa amesema lengo la kukutana hapa ni kufahamu na kutambua masuala juu sheria na sera mbalimbali ambazo zinakwamisha harakati za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwenye ngazi zote za kijamii.
“Matukio kama haya ya udhalilishaji kuendelea kuyasikia ni jambo linaloumiza kichwa sana,ukizingatia Zanzibar watu wake wanaoamini dini hivyo lazima kuwepo kwa jitihada za pamoja kupinga vitendo vya udhalilishaji” Amesema Fathiya huku akiwakaribisha wadau katika mkutano huo.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar SUZA kitengo cha Sheria na Sharia – Daktari Sikujua Omar alikuwa mmoja kati ya wawasilishaji mada ambapo yeye alijikita zaidi kwenye kuziangalia na kuzifafanua Sera 11 huku akiigusia Seraya watu wenye ulemavu ya mwaka 2018 ambapo moja kati ya kipengele chake ni kuwaepusha watu wenye ulemavu na hatari ya unyanyasaji wa kingono.
“Kwenye sera zote hizi zinamgusa mtoto kwenye kila hatua ,ila jee zinatekelezwa kwa ukubwa gani katika kumlinda mtoto wetu na masuala yote ya udhalilishaji ambayo yanaendelea hivi sasa hapa Zanzibar,licha ya kuwa na miongozo na wadau ambao wanasimamia masuala ya udhalilishaji?” Aliuza Daktari Sikujua.
Usimamizi wa sheria katika ngazi za Mahakama ni moja kati ya kipengele ambacho kimekuwa kwenye mijadala ya wahanga,wadau na waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Mohammed Saleh Idd Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka amewasilisha mada kwa upande kwa kisheria huku akitoa ufafanuzi wa jinsi sheria zinavyofanya kazi kwenye kesi za udhalilishaji kwa watoto .Amesema “ Sheria ambazo zinasimamia masuala ya udhalilishaji zinatakiwa kuthibitisha tukio ya binti au kijana kuingiliwa kwenye sehemu zake za siri, jambo ambalo linaweza kuzua taharuki kwa mhanga au pale ushahidi unapotakiwa ila ndio sheria inavyotaka” Amemalizia Mohammed.
Akichangia hoja kwenye mwenendo wa Mahakama Hakimu wa Mkoa wa Vuga Khamis Ali Simai amesema masuala ya udhalilishaji sio tu ubakaji na ulawiti sheria zinatambua masuala ya makuzi,malezi,lishe na mengine yakikosekana kwa mtoto ni udhalilishaji pia.
“Kwa mfano utasikia kesi au taarifa kuhusu mtoto kupigwa,kuchoma moto au hata kutelekezwa ila kesi hizo hazipo kwenye mahakama kwa wingi wake,sheria pia iangalie suala ya kuwapatia adhabu wote maana kesi zinazohusu watoto ambao wana umri wa miaka 18 kwenda juu zinakuwa na changamoto ya ushahidi na upande mmoja tu wa kiume ndio unatiwa kutiwa hatiani hivyo kama sheria ikabadilishwa na kuwaweka wote kifunguni haya mambo yanaweza kupungua” Amemalizia Hakimu Khamis.
Shadida Omar ni mwanasheria kutoka THRDC amesema suala la elimu kwa jamii kuhusu uelewa wa sheria na usimamizi wake ni jambo ambalo serikali na wadau wote wanatakiwa kulisimamia na kulipa kipaombele.
“Elimu ni muhimu sana ,maana kwa mfano suala la dhamana lipo kisheria ila jamii inapoona mtu aliyeshukiwa amefanya kitendo hicho yupo nje anaona hakutendewa haki na mamlaka husika hivyo suala la elimu kwenye sera na sheria kujulikana lazima wananchi wapatiwa elimu “ Amemalizia Shadida.
Wadau kutoka katika Taasisi zote wamekubaliana kwa pamoja suala la kuwepo kwa marekebisho ya baadhi ya sheria pia kusimamia na kufuatilia sera zote zinazogusa masuala ya mtoto kwa ujumla.
Mkutanao huo wa majadiliano juu ya sera na sheria zinazosimamia masuala ya udhalilishaji Zanzibar amefanyika katika ukumbi wa Kariakoo ulipo kisiwani Unguja.
Comments
Post a Comment